Dk Mpango kumuwakilisha Rais Samia mazishi ya Papa Francisco, Vatican
- Mazishi kufanyika Jumamosi, Aprili 26, 2025, mbele ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, Vatican.
- Rais wa Marekani, Rais wa Ufaransa, na Prince William wa Uingereza ni miongini mwa wataohudhuria mazishi hayo.
Dar es Salaam. Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango anatarajiwa kumuwakilisha Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika mazishi ya aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francisko.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msaidizi wa Makamu wa Rais, Franco Singaile, Dk Mpango ameanza safari yake jana Aprili 24, 2025 ambapo mazishi yanatarajiwa kufanyika Jumamosi, Aprili 26, 2025, mbele ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, Vatican.
Baada ya misa ya mazishi, mwili wa Papa Francisko utazikwa katika Basilika ya Bikira Maria Majore (Santa Maria Maggiore) mjini Roma kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Vatican.
Papa Francisko alifariki dunia Aprili 21, 2025, akiwa na umri wa miaka 88, kutokana na kiharusi kilichosababisha matatizo ya moyo.
Ushiriki wa Tanzania katika mazishi hayo unadhihirisha uhusiano na ushirikiano wa karibu kidiplomasia kati ya Tanzania na Vatican pamoja na kuthamini mchango wa Papa Francisko katika masuala ya kijamii na kiroho duniani.
Mazishi hayo yanatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kimataifa, wakiwemo Rais wa Marekani Donald Trump, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, na Prince William wa Uingereza.
Papa Francisko, ambaye alichaguliwa kuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki mwaka 2013, atakumbukwa kwa msimamo wake wa unyenyekevu, kujali masikini, na juhudi za kuleta mageuzi ndani ya Kanisa.
Alikuwa kiongozi wa kwanza kutoka Amerika ya Kusini na wa kwanza kutoka shirika la Kijesuiti kuchaguliwa kuwa Papa.
Kwa sasa, Kanisa Katoliki linaingia katika kipindi cha maombolezo na maandalizi ya kumchagua kiongozi mpya kupitia mkutano wa makardinali (Conclave) utakaofanyika kati ya Mei 6 na 12, 2025.
Latest



