WHO yaendesha Jukwaa la utafiti na ubunifu kushughulikia mlipuko wa virusi vya Corona
- Limeandaliwa kwa ushirikiano wa Muungano wa taasisi ya GloPID-R
- Linalenga kujadili maeneo kadhaa ya utafiti ikiwemo kutambua chanzo cha virusi vya Corona.
Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) linaendesha jukwaa la utafiti na ubunifu la kimataifa ikiwa ni katika jitihada za kushughulika na mlipuko wa virusi vya corona (COVID-2019) ambavyo hadi sasa watu 42,000 wameambukizwa huku vifo zaidi ya 1000 vikiripotiwa kutokea .
Jukwaa hilo, linafanyika kwa siku mbili (Februari 11 na 12 ,2020) limeandaliwa kwa ushirikiano wa Muungano wa Taasisi ya GloPID-R inayoshughulika na ufadhili kwenye tafiti kuhusu magonjwa yanayo ambukiza.
Kwa mujibu wa WHO jukwaa hilo litawakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wanasayansi nguli pamoja na taasisi za afya ya jamii, mawaziri wa afya na wafadhili wa tafiti ambao kwa pamoja watajadili maeneo kadhaa ya tafiti ikiwemo kutambua chanzo cha virusi hivyo.
Pia kwenye mkutano huo watapeana taarifa za sampuli za kibailojia na mienendo ya viasili nasaba au maumbile.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema mkutano huo utakuwa ukijikita kujadili maswala ya sayansi ili kupata uelewa wa maswala ambayo hawana uwelewa nayo kwa mapana.
“Huu siyo mkutano kuhusu siasa na pesa. Huu ni mkutano kuhusu sayansi. Tunahitaji uelewa wa pamoja, mtazamo na uzoefu, kujibu maswali ambayo hatuna majibu yake, na kutambua maswali ambayo tunaweza hata tusitambue kuwa tunahitaji kuuliza,” amesema Dk Tedros.
Dk Tedros amesisitiza mshikamano miongoni mwa wadau hao ili kukamilisha ajenda zilizowekwa kuhusu utafiti wa kimataifa kwa ajili ya virusi vya Corona na kupata matokeo wanayokusudia kuyapata baada ya kufanya tafiti za kina.
Kwa mujimu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), hadi kufikia Februari 2, 2020, watu zaidi ya 14,500 ameambukizwa virusi vya Corona na kusambaa kwenye mataifa 24 licha ya serikali nyingi kuweka marufuku ya kuingia kwa watu wanaotoka China ambako takriban asilimia 99 ya visa vimeripotiwa .