Wenje kugombea nafasi ya Tundu Lissu Chadema

August 5, 2024 6:35 pm · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Aeleza kuwa uamuzi huo ni safari ya kuelekea kugombea nafasi ya urais wa Tanzania.

Mwanza. Mwenyekiti wa Kanda ya Ziwa Victoria Magharibi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Ezekiel Wenje ametangaza rasmi kugombea nafasi ya makamu mwenyekiti wa chama hicho taifa katika uchaguzi ujao akilenga kuchukua nafasi inayoshikiliwa na mwanasiasa machachari wa upinzani, Tundu Lissu. 

Wenje, aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo la Nyamagana miaka 10 iliyopita, amewaambia waandishi wa habari jijini Mwanza leo Agosti 5, 2024 kuwa safari hiyo inaweza kuwa maandalizi ya kwenda kuwania kiti cha urais kwa siku za baadae.

Huku akishangiliwa na wanachama waliokuwa wamehudhuria mkutano huo mfupi, amesema lengo la chama hicho cha upinzani ni kushika dola.

“Mimi ninatangaza hapa rasmi naenda kugombea kiti cha umakamu mwenyekiti Taifa, safari hii inaweza kuwa maandalizi ya kwenda kuwania kiti cha urais kwa siku za usoni kwa sababu umri umefika,” amesema Wenje.

Chadema wanatarajia kufanya uchaguzi wa ngazi za juu za viongozi wa chama hicho kikuu cha upinzani Tanzania kati ya Septemba na Oktoba mwaka huu baada ya kukamilisha hatua za uchaguzi wa nafasi za chini ikiwemo kanda. 

Wenje amesema makamu mwenyekiti ni msaidizi wa mwenyekiti katika kumsikiliza, kusaidiana naye majukumu, kuwa pamoja katika shida na raha huku lengo kuu la haya yote ni chama kushika dola.

Kwa mujibu wa Wenje, kwenye chama Mbowe akiwa Mwenyekiti, Mnyika akiwa Katibu Mkuu haimanishi wao wana akili kubwa kuliko wengine badala yake wako kwenye nafasi hizo kutokana na dhamana ya kukisimamia chama walizopewa.

Baadhi ya wanachama wa chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema jijini Mwanza wakimsikiliza Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa, Ezekiel Wenje wakati akizunumzia uamzi wake wa kuwania kiti cha umakamu mwenyekiti Taifa. Picha|Mariam John/Nukta.

‘Sigombei dhidi ya mtu’

“Hatugombei dhidi ya mtu bali tunatafuta nafasi ya kufanya kazi zaidi na kuwajibika zaidi yaani hapa tunagawana majukumu,” amesema Wenje. 

Hadi sasa Lissu ndiye anashikilia nafasi hiyo ya umakamu mwenyekiti kwa upande wa Bara tangu mwaka 2019. 

Alipoulizwa iwapo hatua hiyo imelenga kumng’oa Lissu madarakani, Wenje amesema halengi kupambana na mtu bali uamuzi huo ni utekelezaji wa haki ya kila mwanachama kugombea nafasi yeyote ya uongozi ndani ya chama kwa lengo la kuwatumikia kwa wananchi na kushika dola. 

Uamuzi wa Wenje umepokelewa kwa hisia tofauti na wakazi wa jiji la Mwanza ambapo baadhi wamedai kuwa amefanya uamuzi wa haraka.

Angesubiri kidogo

Mkazi wa Ibungilo Jijini Mwanza Peter Madeleka amesema nia ya Wenje ni njema lakini angesubiri mpaka mwenye nafasi yake kutangaza kama hana nia ya kugombea tena ama la. 

Mkazi mwingine Asia Method amesema uamuzi alioufanya unaweza kutengeneza taharuki zaidi kwa wanachama na wananchi wakiendelea kuamini kuwa ndani ya chama hicho bado kuna fukuto la kutoelewana.

“Yapo mengi yanaendelea ndani ya chama ambayo yanaenda na hakuna kiongozi anayejitokeza kuthibitisha hilo, sasa na linapokuja hili ni dhahiri kuwa kuna kitu bado kinaendelea ndani ya chama,” amesema Asia.

Hadi sasa Lissu hajaweka bayana iwapo atagombea nafasi hiyo ama la ila hivi karibuni alieleza kuwa amepanga kuwania nafasi ya urais kama alivyofanya katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 alipochuana vikali na aliyekuwa mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Hayati Dk John Magufuli. 

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV