Heche agombea umakamu uenyekiti Chadema akimuunga mkono Lissu, ataja sababu
- Asema ni wakati wa Mbowe kukaa pembeni atizame matunda ya vijana aliowalea
Mwanza. Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Heche amechukua fomu ya kugombea nafasi ya makamu mwenyekiti wa chama hicho Bara, huku akibainisha kuwa anamuunga mkono Tundu Lissu anayewania nafasi ya uenyekiti wa Chadema Taifa.
Uamuzi wa Heche umehitimisha minong’ono ya chini chini iliyokuwepo kuhusu yeye kuwania nafasi hiyo, tangu Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara Tundu Lissu atangaze kutaka kurithi nafasi ya mwenyekiti wa sasa Freeman Mbowe Desemba 5, 2024.
Heche aliyekuwa akizungumza na Wanachadema jijini Mwanza leo Januari 5, 2024 amesema chama hicho kinahitaji watu waadilifu watakao timiza malengo ya kuanzishwa kwake na anaamini kwa sasa Lissu ndiye anayeweza kuyasimamia malengo hayo.
“Leo tuna watu wachache kwenye chama ambao wamepotoka wameshindwa kutambua kwanini chama hichi kilianzishwa…
…na leo nasema rasmi kwamba Mwenyekiti, Freeman Mbowe kwa heshima tutakwenda kwenye uchaguzi, tutakushinda uchaguzi, namuunga mkono Tundu Lissu na nimeamua kuchukua fomu baada ya kutafakari,”amesema Heche.
Heche amekuwa mwanachama wa pili kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo zikiwa zimepita siku mbili toka mwanachama na Mwenyekiti wa Kanda ya Victoria, Ezekia Wenje ambaye anamuunga mkono Freeman Mbowe kuchukua fomu hiyo.
Heche ameongeza kuwa sababu nyingine iliyomsukuma kuwania nafasi hiyo ni pamoja na malengo makuu ya kuanzishwa kwa chama hicho ambayo ni kukiondoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani kwa hiyo anakusudia kutumia uwezo na uzoefu wake kutimiza hilo.
“Hii taasisi ni tegemeo kwa Watanzania…Mimi John Heche nina uzoefu, nina uwezo, nina nguvu, nina maarifa ya kuwa makamu mwenyekiti wa hiki chama wa Taifa, tuunde sekretarieti mpya ya chama chetu, tuunde na tuuhishe majimbo, tusimamie usajili wa chama na twende kwenye slogani inayosema ‘no reform no election na tutakavyosema hivyo hatutosema kwa maneno tu tutasema kwa vitendo na Watanzania watatuunga mkono,” amesisitiza Heche.
Ni muda wa Mbowe kukaa pembeni
Akimzungumzia Mwenyekiti wa sasa Freeman Mbowe, Heche amesema licha ya kuwa anamheshimu kwa kumjenga kisiasa muda wake wa kukaa pembeni umefika ili atazame matunda ya vijana aliowalea.
“Mimi nina mheshimu mwenyekiti na ninampenda..kwangu ni baba wa siasa ambaye amenifikisha hapa, siwezi kusema baya kuhusu Mbowe,” amesema Heche.
Hata hivyo, Heche ametumia sehemu ya hotuba kuelezea msimamo wake juu ya namna kampeni za uchaguzi zinapaswa kufanyika, akisisitiza kuepusha matusi kwa wafuasi wa pande zote mbili yaani inayomuunga mkono Lissu dhidi ya ile ya Mbowe ingawa alimtupia lawama Mwenyekiti wa Chadema kanda ya Victoria Ezekia Wenje kuhusika kuchochea migogoro baina yao.
“Kwa rafiki yangu Wenje, kwa kifupi sana tumefika hapa tulipo kwa sababu yako. Mheshimiwa muachie mtu mwingine akuoneshe tunaenda wapi. Hii ni taasisi ambayo inashindana na Serikali kila siku. Hatuwezi kuua taasisi hii (Chadema) hii taasisi ni tegemeo kwa Watanzania. Hata wana CCM hawataki Chadema ife,” amesema Heche.