Wenje aonya matusi dhidi ya wagombea Chadema

January 3, 2025 5:16 pm · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Asema kuna maisha baada ya uchaguzi 

Mwanza. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Victoria Ezekia Wenje amewataka wanachama wa chama hicho kuwa watulivu wakati huu wakijiandaa na uchaguzi wa viongozi wa kitaifa unaotarajiwa kufanyika Januari 21, 2025.

Wenje aliyekuwa akizungumza na wanachadema mara baada ya kuchukua na kurejesha fomu ya kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara amesema mitifuano inayoendelea baina ya viongozi wa juu wa chama hicho inasababishwa na wapambe wa viongozi hao ingawa wao hawana tofauti kama inavyotafsiriwa na wengi.

Kauli ya Wenje inakuja wakati ambao kumekuwepo na vuguvugu la kutupiana maneno kati ya wanaoaminika kuwa wafuasi wa Tundu Lissu na wale wa Mwenyekiti wa sasa Freeman Mbowe kuhusu nani anafaa kuwa mwenyekiti mpya wa chama hicho kikuu cha upinzani.

Aidha, baadhi ya viongozi na wafuasi wa chama hicho wamekuwa wakimshutumu Tundu Lissu kukipaka matope chama hicho kwa kutoa siri za chama pamoja na habari zinazoweza kuwagombanisha wanachadema na viongozi wao ambapo Lissu mwenyewe amekuwa akisisitiza kuwa anayasema mambo hayo kwa kuwa ni sehemu ya mabadiliko anayotarajia kuyafanya iwapo atakuwa mwenyekiti.

“Hayo mnayosoma kwenye mitandao ya kijamii yanatolewa na wapambe tu lakini viongozi hawana tatizo lolote na wanakutana kutekeleza shughuli za chama kama kawaida, hivyo tusiyabebe maneno hayo yakasababisha kukigawa chama,” amesema Wenje.

Aidha, Wenje amewasihi wafuasi wake kutumia kauli za staha katika kujenga hoja na siyo matusi kwa kuwa maisha ya kawaida yataendelea baada ya uchaguzi akisisitiza kila mtu ana hadhi sawa katika chama hicho.

“Chama chetu ni kikubwa kuliko mtu yeyote. Hii dunia tunapita, tuweke akiba ya maneno. Kuna maisha baada ya uchaguzi,” amesisitiza Wenje.

Hata hivyo, Wenje amesema licha ya kuonekana kama kuna kutoelewana na Tundu Lissu anayegombea uenyekiti wa chama hicho, ila akichaguliwa na Lissu akachaguliwa, wataangalia namna bora ya kufanya kazi kwa pamoja.

“Mimi Tundu Antipas Lissu ni mtu ninayemuheshimu, amekuja kwetu kijijini, mimi kwao na Tundu Lissu ni sehemu ya familia yangu, tutayavuka salama, lazima niangalie namna gani tutatengeneza mahusiano na kufanya kazi kwa pamoja,” amesema Wenje.

Wenje ameongeza kuwa  miongoni mwa mambo atakayoyafanya atakaposhinda nafasi hiyo ni kusimamia maadili, akieleza siku za hivi karibuni baadhi ya wanachama na makada wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kuwatukana wengine wakidhani ndio siasa kinyume na maadili yao.

Pia amesema atasimamia Chadema Digital kuhakikisha wanakusanya mapato ya kutosha yatakayotumika kuendeleza chama, kutoa mafunzo kwa viongozi na posho kwa makatibu wa chama hicho, akidai wanafanya kazi kubwa ya kukijenga lakini hawalipwi kitu.

Kuhusu kauli yake ya wananchi wasiokuwa na vyeo ndani ya chama hicho kuwa ni wakunja ngumi, Wenje amesema msemo huo umekuwa ukitumiwa kama utani kwa wanachama ndani ya chama hicho ukimaanisha nguvu ya umma kama ilivyokauli mbiu ya chama hicho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks