Waziri Ummy: Kirusi kipya cha Uviko-19 hakijafika Tanzania
- Asema kwa sasa wanapambana na kirusi cha Omicron.
- Baadhi ya nchi zaripoti kirusi hicho chenye muunganiko wa Delta na Omicron.
- Tanzania yaendelea kutoa chanjo.
Dar es Salaam. Wakati Serikali ya Tanzania ikiendelea na zoezi la utoaji chanjo dhidi ya virusi vya Corona (Uviko-19), imesema kirusi kipya cha ugonjwa huo ambacho kimeripotiwa katika baadhi ya nchi duniani hakijafika bado Tanzania.
Waziri wa Afya Umri Mwalimu aliyekuwa akizingumza leo Machi 23, 2022 wakati akipokea dozi milioni 1 za chanjo aina ya Sinovac, msaada kutoka Uturuki amesema taarifa zilizopo katika wizara yake hadi leo asubuhi ni kuwa hakuna kirusi kipya kilichoripotiwa nchini zaidi ya kirusi aina ya Omicron.
“Asubuhi nilikuwa naongea na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu hicho kirusi kipya wakaniambia bado wanaendelea kufanya tafiti kujua kitakuwa kikali kiasi gani na madhara yake yatakuwaje. Habari njema ni kwamba na sampuli nilizoelekeza zichukuliwe kuangalia kama tuna kirusi hicho zimeoonyesha hatuna bado tuna Omicron,” amesema Ummy.
Kwa mujibu wa WHO, baadhi ya nchi zimeanza kuripoti uwepo wa kirusi hicho kipya kinachodaiwa kuwa na muunganiko wa Delta na Omicron.
Zinazohusiana
- Jinsi ya kujikinga na virusi vya Corona kwenye mikusanyiko ya watu
- Magufuli aagiza safari za nje zipunguzwe kujikinga na virusi vya Corona
Utoaji wa chanjo
Aidha, amesema hadi kufikia Machi 21, 2022 jumla ya watu milioni 3.01 wamepata chanjo kamili kati ya watu milioni 30.7 wenye umri wa miaka 18 na kuendelea ikiwa ni sawa na asilimia 9.81.

“Nachukua fursa hii kuendelea kuwasisitiza viongozi na watendaji wa ngazi zote kuendelea kutoa ushirikiano ili wananchi waendelee kuhimizwa kupata elimu ya chanjo ili wapate chanjo wajikinge na maambukizi ya Uviko-19,” amesema Ummy.
Waziri Ummy amesema Serikali inalenga kuchanja asilimia 70 ya Watanzania kuanzia umri wa miaka 18 hadi mwisho wa mwaka 2022.
Wananchi wametakiwa kuendelea kuchukua tahadhari zote ikiwemo kunawa mikono, kuvaa barakoa, kutumia vitakasa mikono na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.
Latest