Waziri Mkuu Mstaafu Cleopa David Msuya afariki dunia
- Rais Samia atangaza bendera kupepea nusu mlingoti kwa siku saba za maombolezo.
- Taarifa zaidi kuhusu msiba zitaendelea kutolewa na serikali.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania Cleopa David Msuya amefariki dunia leo katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam alipokuwa anapatiwa matibabu ya maradhi ya moyo.
Taarifa ya kifo cha Msuya imetangazwa leo majira ya alasiri na Rais Samia aliyebainisha kuwa kiongozi huyo amefariki majira ya saa 3 asubuhi leo Mei 07, 2025 katika Hospitali ya Mzena, jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa moyo.
“Hayati Cleopa David Msuya ameugua kwa muda mrefu na amekuwa akipatiwa matibabu ndani na nje ya nchi ikiwemo katika Hospitali ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Mzena na kule jijini London,’’ amesema Rais Samia
Aidha, Rais Samia ametuma salamu zake za pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote kwa msiba na kutangaza siku saba za maombolezo ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti kuanzia Mei 07 hadi 13 mwaka huu.
“Taarifa zaidi kuhusu msiba huu zitaendelea kutolewa na serikali, poleni sana Watanzania,” ameeleza kwa masikitiko Rais Samia.
Marehemu Msuya alizaliwa Januari 4,1931 huko Chomvu Usangi, Wilaya ya Mwanga, mkoa wa Kilimanjaro ambapo alisoma Chuo Kikuu cha Makerere kati ya 1952–1955 na kisha kufanya kazi za maendeleo vijijini hadi 1964.

Kuanzia mwaka huo alihudumu kama Katibu Mkuu katika wizara mbalimbali hadi 1972, alipoteuliwa kuwa Waziri wa Fedha na baadaye kushika nyadhifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Waziri wa Viwanda, Waziri Mkuu (1980–1983 na tena 1994–1995), na Waziri wa Fedha na Mipango hadi 1994. Baada ya uchaguzi wa 1995 alibaki kuwa Mbunge hadi alipostaafu mwaka 2000.
Hata baada ya kustaafu, aliendelea kushiriki katika siasa kupitia CCM na alikuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Maendeleo la Kilimanjaro. Mnamo Oktoba 23, 2019 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo cha Ardhi akiwa na umri wa miaka 88.
Latest



