Tanzania, Msumbiji kufungua fursa mpya za ushirikiano wa maendeleo
- Ni baada ya Rais Chapo wa Msumbiji kukamilisha ziara ya siku tatu nchini.
Dar es Salaam. Rais wa Msumbiji, Daniel Francisco Chapo ameanza ziara ya kikazi leo nchini Tanzania inayokusudia kudumisha uhusiano wa kihistoria, kindugu na kiuchumi kati ya nchi hizo mbili ili kufungua fursa mpya za ushirikiano wa maendeleo.
Ziara hiyo ya Kiserikali ya siku tatu inayoanza leo Mei 7, 2025 ni ya kwanza kufanya nchini Tanzania kwa Rais Chapo tangu aapishwe kuwa Rais wa Taifa hilo la Kusini mwa Afrika Januari 15 mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Mei 7, 2025 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Sharifa Nyanga, ziara hiyo inalenga kudumisha uhusiano wa kihistoria na kidugu uliopo kati ya Tanzania na Msumbiji pamoja na kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara na uwekezaji.
Nyanga katika taarifa hiyo ameeleza kuwa Rais Chapo anafanya ziara hiyo baada ya kualikwa na mwenyeji wake Rais Samia Suluhu Hassan ambapo kesho wanatarajia kufanya mazungumzo Ikulu ya Dar es Salaam.
Miongoni mwa shughuli za ziara hiyo ni kushuhudia uwekaji saini wa mikataba na hati za makubaliano (MoU) katika sekta kadhaa.
Akiwa nchi, Rais Chapo pia atatembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Afrika, na mradi wa kimkakati wa Reli ya Kisasa (SGR) kwa lengo la kujifunza na kuangalia maeneo mapya ya ushirikiano kati ya Tanzania na Msumbiji.
“Rais Chapo atapata fursa ya kutembelea Zanzibar ambapo atafanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi na kutembelea miradi mbalimbali ikiwemo Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu na Soko la Samaki la Malindi,” imeeleza taarifa hiyo.

Mei 9, 2025, Rais Chapo atakamilisha ziara yake ya kiserikali na kurejea Msumbiji.
Licha ya Tanzania na Msumbiji kuwa na historia muhimu ya ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika, zimekuwa zikifanya biashara ambazo zimekuwa na manufaa kati pande zote mbili.
Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Biashara Tanzania (Tantrade), hadi kufikia mwaka 2021, zilifanya biashara yenye thamani Dola za Marekani milioni 10.8 sawa Sh28.08 bilioni ikiongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 6.6 sawa na Sh17.16 bilioni mwaka 2017
Tanzania inauza zaidi kwa Msumbiji, bidhaa za vinywaji, malighafi za ujenzi kama nondo na saruji. Pia nauza tumbaku, pamba na mafuta. Wataki Tanzania inaingiza zaidi bidhaa za aluminiumu, mbao, vitabu pamoja na sukari kutoka Msumbiji.
Latest



