Waziri Kairuki azindua kamati ya kitaifa ya kuongoa shoroba
- Ni utekelezaji wa Mpango wa Kuongoa na kusimamia Shoroba 20 za wanyamapori za Kipaumbele nchini.
- Asema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa uhifadhi kutunza shoroba hizo.
- Asisitiza matumizi bora ya ardhi, kutanua mawanda ya faida.
Dar es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki amezindua kamati ya kitaifa ya kuongoa shoroba(mapito ya wanyama pori) katika kongamano la kwanza la kitaifa la kujadili usimamizi madhubuti wa shoroba ili kuleta manufaa ya kiuchumi huku akiielekeza kamati hiyo kufanya kazi kwa kasi zaidi.
Waziri Kairuki aliyekuwa akizungumza katika kikao cha kwanza cha jukwaa la kitaifa la kuongoa shoroba ikiwa ni utekelezaji wa Mpango wa Kuongoa na Kusimamia Shoroba 20 za Wanyamapori za Kipaumbele nchini, leo Disemba 14, 2023 amewaambia washiriki kuwa dhumuni la kikao hicho ni kuwaleta pamoja wadau wa uhifadhi kujadili mpango huo.
Kairuki amesisitiza Wizara yake kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kufanikisha usimamizi huo, kwa kuwa jambo hilo haliwezi kutekelezwa na wizara pekee huku akiwaomba wadau wa ndani na nje ya nchi kuendelea kujitokeza kuunga mkono juhudi hizo.
“Sambamba na zoezi hilo Serikali itaendelea kutekeleza mpango wa matumizi bora ya ardhi katika maeneo ya shoruba ili maeneo hayo yaweze kutumika kikamilifu katika mawanda mengine kama utalii wa picha hivyo kuinufaisha jamii inayozunguka maeneo hayo na nchi kwa ujumla wake,” amesema Kairuki.
Soma zaidi : Rais Samia ateua, atengua na kuhamisha viongozi wa mikoa, wilaya, halmashauri
Waziri Kairuki ameongeza kuwa, kukamilika kwa matumizi bora ya ardhi kutasaidia kuainisha maeneo yatakayotumika kwa ajili ya huduma za kijamii kama shule hospitali, kilimo na malisho.
Kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Tanzania ina jumla ya shoroba 61 ambapo 41 zipo hatarini kutoweka kutokana na kuvamiwa na shughuli za kibinadamu huku shoroba 20 kati ya hizo zikiwa zimezibwa kabisa.
Miongoni mwa athari za binadamu kuvamia shoroba hizo ni pamoja na kuwepo kwa migogoro ya mara kwa mara kati ya binadamu na wanyama ambapo mara nyingi wanyama huripotiwa kusababisha uharibifu wa mali au vifo kwa wanyama na binadamu.
Aidha, malengo mengine ya kikao hicho kilichowakutanisha wadau mbalimbali wa uhifadhi wakiwemo Nukta Africa wanaotekeleza mradi wa Habari Bora kwa Uhifadhi endelevu unaofadhiliwa na USAID Tuhifadhi Maliasili, ni pamoja na kuainisha wadau na kuweka maazimio ya nani afanye nini na wapi ili kuongoa na kuhifadhi shoroba za wanyamapori, hasa zilizo hatarini.
Mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya kuongoa shoroba, Linnah Kitosi amesisitiza kuwa jambo la kwanza kwa sasa ni kuwaelimisha wananchi waweze kuzitambua shoroba ili wanyama waendelee kupita na wananchi waweze kufanya shughuli zao bila kuleta migongano na madhara.