Watumiaji wa intaneti waongezeka kwa kasi Tanzania, wakaribia milioni 26
- Wameongezeka kwa asilimia 11.5 hadi kufikia milioni 25.8 mwaka 2019 kutoka milioni 23.1 waliorekodiwa mwaka 2018.
- Ongezeko hilo linafanya takriban nusu ya watu (asimilia 46) kufikiwa na huduma za intaneti nchini.
Dar es Salaam. Watumiaji wa intaneti Tanzania wameongezeka kwa asilimia 11.5 hadi kufikia milioni 25.8 mwaka 2019 kutoka milioni 23.1 waliorekodiwa mwaka 2018, jambo linalofungua milango kwa Watanzania kufaidika na fursa za mtandaoni ikiwemo kufanya biashara na kupata ujuzi. Â
Kwa mujibu wa Takwimu mpya za robo ya mwisho wa mwaka 2019 za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zilizotolewa wiki hii, ongezeko hilo linafanya takriban nusu ya watu (asimilia 46) kufikiwa na huduma za intaneti nchini ikilinganishwa na mwaka juzi ambapo ilikuwa asilimia 43.
Hata hivyo, ripoti hiyo haijaweka wazi ni aina gani ya intaneti inayotumiwa zaidi na Watanzania kama ambavyo imekuwa ikifanyika miaka iliyopita, ambapo intaneti inayohamishika (mobile wireless) ambayo hutumika zaidi na simu za mkononi, tableti na kompyuta mpakato ndiyo imekuwa ikitumika zaidi na watu.Â
Kwa takwimu za mwaka 2018, watumiaji intaneti inayohamishika walikuwa asilimia 96.2 inayotumika na simu, wakifuatiwa na intaneti isiyo ya waya na isiyohamishika kwa asilimia tatu.
Hiyo ina maana kuwa kila watumiaji 10 wa intaneti basi tisa walikuwa wanatumia intaneti inayohamishika.
Zinazohusiana:
- Ni historia: Watumiaji wa intaneti Tanzania sasa wafikia milioni 23.
- Mbinu tano za kudhibiti matumizi makubwa ya intaneti kwenye ‘smartphones’.
Ikiwa intaneti itatumika kwa usahihi inaweza kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi kwa sababu inawawezesha watu kufanya biashara ya mtandaoni, kurahisisha mawasiliano na utunzaji wa vitu mtandaoni.
Pia inasaidia katika upatikanaji wa maarifa na ujuzi na kuimarisha mahusiano ya watu wanaoishi maeneo tofauti tofauti.
Latest