Wasichana milioni 2 hatarini kukeketwa ifikapo 2030
- Ni kutokana na athari za Corona ikiwemo kufungwa shule.
- Wadau washauri hatua zichukuliwe haraka kuwanusuru wasichana
- Februari 3, 2022 duniani inaadhimisha siku ya kutokomeza ukeketaji.
Dar es Salaam. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani (UNICEF) limesema kuwa watoto wa kike milioni 2 wanaweza kukeketwa ifikapo mwaka 2030 na kupunguza kwa asilimia 33 harakati za dunia za kuelekea kutokomeza vitendo hivyo, endapo hatua hazitachukuliwa.
Mikakati ya dunia ni kutokomeza kabisa ukeketaji wanawake na wasichana (FGM) ifikapo mwaka 2030.
Hata hivyo, janga la ugonjwa wa Corona (Uviko-19) linaweza kufuta mafanikio yote ya harakati za dunia za kutokomeza ukeketaji wanawake na wasichana (FGM), yameonya mashirika ya Umoja wa Mataifa wakati huu dunia ikijiandaa kuadhimisha siku ya kutokomeza vitendo hivyo haramu Februari 6 mwaka huu.
Kufungwa kwa shule, vizuizi vya kutembea na kuvurugwa kwa huduma za kulinda wasichana, kumewaweka mamilioni yao duniani kote katika hatari ya kutumbukia katika kukeketwa.
“Tunapoteza mwelekeo wa vita vya kutokomeza FGM, na kutakuwa na madhara makubwa kwa mamilioni ya wasichana kule ambako mila hiyo potofu inatekelezwa,” amesema Mshauri Mwandamizi wa UNICEF kuhusu vitendo na mila potofu, Nankali Maksudi na kubainisha kuwa,
“Pindi wasichana hawana uwezo wa kupata huduma muhimu, hawawezi kwenda shule na hawana uwezo wa kutumia mitandao ya usaidizi ya kijamii, hatari ya kukumbwa na FGM ni kubwa zaidi na hivyo kutishia afya yao ya baadaye halikadhalika elimu.
Katika kuadhimisha siku hiyo ya kutokomeza ukeketaji duniani, mashirika ya Umoja wa Mataifa yanataka hatua zaidi za kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa sambamba na afya na utu wa wanawake na wasichana.
Zinazohusiana:
- Uongozi, ardhi kuwatoa kimaisha wanawake vijijini
- Uhaba wa wanawake sekta ya teknolojia wakwamisha utekelezaji wa ajenda za maendeleo
- SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA: Kila mtu awajibike
Waliokeketwa duniani
Takribani watoto na wasichana milioni 200 duniani kote wamekeketwa na hii inajumuisha aina zote za ukeketaji unaofanyika ikiwemo kubadili maumbile ya sehemu zao za siri kwa sababu zisizo za kimatibabu.
Kwa kiasi kikubwa FGM hufanyika kwa watoto wa kike wenye umri wa kuanzia pale alipozaliwa hadi umri wa miaka 15 na kwa sababu tofauti tofauti za kijamii kulingana na eneo na nchi.
Mathalani kwa maeneo mengine wanadai kuwa ni mila muhimu ya kumuandaa mtoto wa kike kwa ajili ya kuingia utu uzima na ndoa.
Katika maeneo mengine, FGM inahusishwa na maadili ya kijamii ya kukamilika kiusichana na kupunguza hamu ya kufanya tendo la ngono.
Wasichana wanaokeketwa hukumbwa na madhara ya muda mfupi kama vile maumivu, mshtuko, kuvuja damu kupita kiasi na kushindwa kutoa mkojo huku madhara ya muda mrefu ni pamoja na kushindwa kufanya tendo la ndoa, kujifungua kwa tabu na madhara kwa afya ya akili.
FGM ni tatizo duniani kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa. Ijapokuwa imejikita katika nchi 30 Afrika na Mashariki ya Kati, inatekelezwa pia barani Asia na Amerika ya Kusini na kwa baadhi ya jamii za wahamiaji huko Ulaya Magharibi, Amerika Kaskazini, Australia na New Zealand.
Katika baadhi ya nchi, inafanywa katika takribani nchi nzima. UNICEF inasema kuwa asilimia 90 ya wasichana Djibouti, Guinea, Mali na Somalia wamekeketwa.
WHO imetoa taarifa juu ya mwelekeo unaotia shaka wa FGM kutekelezwa na wahudumu wa afya ikisema kuwa takribani msichana 1 kati ya 4 waliokeketwa, amefanyiwa hivyo na mhudumu wa afya, idadi ambayo ni sawa na wasichana na wanawake milioni 52 duniani kote.
Latest



