Uongozi, ardhi kuwatoa kimaisha wanawake vijijini

October 15, 2018 7:46 pm · Zahara
Share
Tweet
Copy Link
  • Fursa zinazowazunguka wanawake vijijini ni pamoja na kugombea nafasi za uongozi katika ngazi ya jamii.
  • Uongozi utawafungulia fursa nyingine ya kumiliki mali na kufaidika na sekta ya kilimo.
  • Wadau wapendekeza mabadiliko ya sera na sheria kuwafungulia wanawake mpenyo wa kutoka kimaisha.

 Dar es Salaam. Kwa mujibu wa kalenda ya Umoja wa Mataifa, Oktoba 15 ya kila mwaka ni Siku ya Kimataifa ya Wanawake Vijijini; mahususi kwa ajili ya kutambua mchango wa wanawake katika kilimo na maendeleo duniani.

Siku hii inaadhimishwa ili kuwapa moyo wanawake wa vijijini kuendelea kutoa mchango katika kuleta maendeleo katika ngazi ya familia na taifa kwa ujumla.

Ukiondoa mchango huo bado kuna fursa nyingi za maendeleo kwa wanawake wa vijijini kama wakizichangamkia, basi watapiga hatua kubwa katika kujiimarisha na kujiendeleza kiuchumi.

Fursa zinazowazunguka wanawake vijijini ni pamoja na kugombea nafasi za uongozi katika ngazi ya jamii hasa wakati huu ambao nchi inajiandaa kuingia katika uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika mwaka 2019 nchi nzima.  

Uongozi utawasadia kuwa sehemu za kutengeneza sera, sheria na mipango ya maamuzi yanayohusu maendeleo ya jamii. Lakini ni jukwaa muhimu kutetea haki za wanawake waishio  vijijini ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikandamizwa na mfumo dume. 

“Wanawake wa vijijini kwanza wanahitaji sana kupewa elimu ya kuwajengea uwezo wa kujiamini, kujikubali na kujitoa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi,” anasema Salha Azizi, Mkurugenzi wa taasisi ya Binti Salha Foundation.

Hii ni kwasababu karibu maamuzi mengi yanayohusu safari ya maendeleo vijijini yanailenga moja kwa moja Serikali iliyopo eneo husika, hivyo wanawake wa vijijini wakitaka waanze kuwa na nguvu ya kufanya maamuzi basi hawana budi kuingia katika siasa na uongozi.


Zinazohusiana: 


Hatamu za uongozi zitawafungulia fursa nyingine ya kumiliki mali ikiwemo ardhi ambayo wamekuwa wakiipigania kwa muda mrefu licha ya vikwazo vingi vilivyowekwa mbele yao.  

Rahma Mwita, mdau wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ameiambia Nukta kuwa licha ya wanawake wa vijijini kuchangamkia sekta ya kilimo kama eneo muhimu la kuwaingizia kipato bado kuna  changamoto nyingi zinawakabili katika matumizi ya ardhi ikiwemo elimu na teknolojia duni.

“Wengi wao hawana elimu ya kuwafanya wapate mapato ya kutosha kwa kujihusisha na biashara hiyo,” anasema Rahma. 

Anabainisha kuwa hali hiyo imewafanya wanaume kunufaika na mazao yanayotokana  na jasho la  wanawake ambao wanatumia muda mwingi kulima lakini wanakosa sauti na maamuzi ya kiuongozi katika rasilimali za familia.  Jamii iondokane na mfumo dume, mila na desturi ambazo zinamkandamiza mwanamke. Picha| wandilesihlobo.com

Afisa Programu Msaidizi kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Tito Magoti anasema kuna kila sababu mifumo ya sheria na sera zipitiwe kuhakikisha zinafungua fursa kwa wanawake kufaidika na ardhi iliyopo vijijini ikizingatiwa kuwa wanachangia karibu asilimia 52 ya nguvu kazi katika sekta ya kilimo. 

“Jamii iondokane na mfumo dume, mila na desturi ambazo zinamkandamiza mwanamke,” anasema Magoti.

Hata hivyo, kuzipata fursa hizo sio jambo dogo, inahitajika nguvu ya pamoja ya  wanawake wa vijijini kuanzisha vikundi vya maendeleo ili  kuwaongezea nguvu ya kiuchumi  itakayowasaidia kuwekeza katika miradi ya maendeleo.

Serikali nayo imejipanga kuwafikia wanawake wengi walioko vijijini kupitia vikundi vya kifedha (VICOBA) ili kuwaunganisha na fursa mbalimbali nchini, sambamba na kuzihamasisha Halmashauri zote kutenga asilimia nne ya mapato yake ya ndani ili kuwawezesha wanawake kiuchumi.

Enable Notifications OK No thanks