SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA: Kila mtu awajibike

November 27, 2018 12:45 am · Zahara
Share
Tweet
Copy Link

Ni jukumu la kila mmoja kupinga ukatili wa kijinsia kwasababu unamadhara kwa jamii nzima kwa ujumla.Picha| Sufiani Mafoto.


  • Kampeni hiyo italeta maana ikiwa kila mtu katika nafasi yake atasimama kukemea na kupinga vitendo vyote vinavyohatarisha maisha na ustawi wa wasichana na wanawake katika jamii.
  • Wadau wapendekeza adhabu iongezwe kwa watu wanaotekeleza vitendo vya ukatili katika jamii.
  • Mafataki waonywa dhidi ya kuwarubuni na kukatiza ndoto za elimu za watoto wa kike.

Dar es Salaam: Kila Novemba 25 hadi 10 Disemba ya kila mwaka ni siku 16 za kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia ambayo huadhimishwa kwa maandamano na kampeni mbalimbali kwa taasisi zinazojihusisha na masuala ya kuendeleza usawa wa kijinsia katika jamii.

Mwaka huu kauli mbiu inasema “Hear Me Too” ikimaanisha nisikilize na mimi pia. Katika siku hizi 16 midahalo mbalimbali hufanyika ngazi ya Taifa, mkoa, wilaya pamoja na vikundi mbalimbali vya wanawake katika kuleta hamasa na kufikisha ujumbe kwa jamii kutokomeza vitendo vya ukatili kijinsia.

Rangi inayotumika zaidi ni ya machungwa ikiashiria mtu aliyevaa nguo ya rangi hiyo yuko katika harakati za kuunga mkono juhudi hizo. Rangi hiyo yenye maana ya kuamini kuwa baadaye hakutokuwa na ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.

Ukatili wanaokumbana nao wanawake ni pamoja na kubakwa, kuombwa rushwa ya ngono, kunyanyaswa katika familia zao, kukeketwa na kunyimwa haki zao za msingi kama kwenda shule, kumiliki ardhi au kutoa maoni katika ngazi ya kifamilia na kijamii.

Hata hivyo, bado Serikali kwa shirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo wanaendelea na juhudi za kutoa elimu na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watu wanaotekeleza ukatili wa kijinsia ili kuhakikisha jamii inazingatia na kuheshimu haki za msingi kila mtu katika jamii.

“Nawaagiza wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na viongozi wote, kuhakikisha mnaanzisha kamati za ulinzi za wanawake na watoto kama inavyoelekezwa katika mpango wa kitaifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto,” amesema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa anaongea na wananchi katika maadhimisho ya siku 16 za kampeni ya kupinga unyanyasaji na ukatili wa kijinsia, Jijini Dodoma.


Zinazohusiana: 


Yote hii ni juhudi za kuhakikisha haki za watoto na wanawake zinapewa kipaumbele na Majaliwa akaenda mbali zaidi kwa kueleza kuwa, Serikali itawachukulia hatua kali watakaohusika na kutaka kuwaharibia watoto masomo yao au kuwafanyia ukatili wowote wa kijinsia.

Majaliwa amesisitiza zaidi umuhimu wa kumlinda mtoto wa kike ili atimize ndoto zake kielimu licha kuwepo kwa zuio linalowakataza wanafunzi waliopata mimba wakiwa shuleni kuendelea na masomo.

“Tukikukuta umesimama kwenye kona isiyoeleweka na mwanafunzi, tutakushughulikia. Wale wataalam wa kuwasalimia wanafunzi mara nne kwa siku, ole wako,” amesema Majaliwa.

Ili kuhakikisha ujumbe wa kampeni ya kupinga ukatili unawafikiwa watu wengi, kauli mbiu kama “Usalama Wake Wajibu Wangu” ikimaanisha kila mtu ahakikishe usalama wa mtoto wa kike na mwanamke zimeendelea kutumika na taasisi na mashirika mbalimbali.

Kwa mujibu wa taarifa wa tamko la shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa (UN Women) linaelezakuwa kati ya wanawake watatu duniani basi mmoja amekumbana na ukatili wa kijinsia kwa namna moja au nyingine ambapo ni muda muafaka kwa jamii kubadilika na kuachana na unyanyasaji.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema ukatili wa kijinsia ni kikwazo kwa maendeleo nchini kwasababu pesa ambazo zingeelekezwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo zinatumika kupambana na watu wanaojihusisha kuwafanyia wanawake na watoto ukatili.  

“Mabilioni ya fedha zinazotumika kupambana na ukatili wa kijinsia tungeweza kuziweka kwenye kuboresha sekta ya afya, elimu, na huduma za jamii,” amesema Mwalimu.

Pamoja na hayo wadau mbalimbali wanaona ni muda muafaka wa jamii wa kuishi kwa usawa na kujiepusha na vitendo vya ubaguzi na kuheshimu sheria na haki za binadamu kwa ustawi mzuri wa jamii.  

“Waache kunyanyasa au kubagua wanawake kijinsia ila wajifunze kufuata sheria na haki kwa wote,” amesema Johnson Michael, mkazi wa Sinza madukani Jijini Dar es Salaam.

Enable Notifications OK No thanks