Wasanii wa Kenya, Tanzania wakutana kujadili suluhu ya Corona
- Walikutana katika mkutano wa pamoja mtandaoni kuangazia athari za Corona katika tasnia ya sanaa.
- Baadhi yao wametoa suluhu ikiwemo kubuni vitu vipya ili kupunguza makali ya athari hizo.
Dar es Salaam. Kuna siku yoyote umewahi kumaliza siku yako bila kusikia muziki? Labda kama hauna redio au kama umejifungia ndani. Lakini hata kwa majirani? Mh! haiwezekani.
Muziki huo unaosikiliza ni ajira za watu. Licha ya kuwepo kwa mlipuko wa virusi vya Corona (COVID-19) bado muziki unatengenezwa na watu wanaendelea kuusikiliza.
Wanachopungukiwa kwa sasa ni kuburudika moja kwa moja katika matamasha na maonyesho mubashara ya majukwaani. Corona imekuwa kikwazo kwa watu kukusanyika, jambo linawanyima pia fursa wanamuziki kujipatia kipato.
Njia panda hiyo imetokana na kuzuiliwa kwa mikusanyiko ambayo ni chanzo cha wasanii wengi kupeleka mkono kinywani. Je, ni mambo gani yatakayowasaidia wanamuziki waendelee kuishi kipindi hiki?
Mdau wa sanaa ambaye ni Mwasisi wa kampuni ya Unleashed Academy, Khalila Mbowe amesema ugonjwa wa Covid-19 umeweka nukta kwenye maisha ya wasanii wengi wakiwemo wa muziki, ngoma na hata maigizo.
Binti huyo amesema, kwa wakati huu ni vizuri wasanii wakajikita kwenye ubunifu na kutumia teknolojia ili kuhakikisha wanaendelea kunawiri.
Licha ya kuwepo kwa mlipuko wa virusi vya Corona (COVID-19) bado muziki unatengenezwa na watu wanaendelea kuusikiliza. Picha| GlobalRent.
Baadhi ya wasanii wa Kenya na Tanzania walioshiriki mjadala wa mtandaoni wa kutafuta suluhu dhidi ya athari za COVID-19 katika sanaa hivi karibuni, wameeleza kuwa kwa sasa wasanii wanapaswa kuendelea kuimarisha utambulisho na majina yao (brand) ili wasipotee kabisa katika tasnia hiyo.
Mdau wa masoko ya kidijitali ya sanaa, Semu Bandora amesema kikubwa wanachoweza kukifanya kwa sasa ni pamoja na kuendela kulitunza jina lao kwani hilo ndilo linalowapatia kula.
Bandora amesema brand ya msanii ni zaidi ya mavazi mazuri na gari la kifahari bali ni pamoja na kuwa na uelewa wa mambo yanayoendelea na kuhakikisha thamani yako kwa mashabiki haishuki.
“Ni wakati wa kujiweka kwenye mazingira ambayo watu watahusiana na wewe,” Bandora amesema.
Zinazohusiana
- Kutana na wanasayansi wa kike wanaotikisa mashindano ya ulimbwende Tanzania
- Wanafunzi vyuo vikuu waugeukia muziki kutoka kimaisha
- Jessica Mshama: Mwanamuziki, Mjasiriamali anayebadilisha maisha ya Watanzania kwa biashara
Msanii wa miondoko ya Afropop, Frankie Maston kutoka Tanzania amesema huu ni muda ambao wasanii wanatakiwa kukaa zaidi studio ili kutengeneza kazi ambazo wataziuza kwa mashabiki wao wakati wakisubiri matamasha yarudi.
Maston anayesumbua spika mbalimbali na kibao chake cha Mi na Wewe amewaambia wasanii “hakikisha unatengeneza kitu. Pale Corona inapoisha, anza kusherekea kwa kitu ambacho umekitengeneza.”
Ni wakati ambao wasanii wanatakiwa kuwekeza katika programu za kidijitali za utayarishaji na uuzaji wa kazi zao ili kuifikia dunia kwa urahisi kuliko kutumia mifumo ya zamani ambayo inaweza isilete matokeo.
Mdau wa muziki usiotumia vyombo vya muziki maarufu kama Acapella , Allen Gamba kutoka Tanzania amesema zipo programu za mtandaoni ikiwemo ya “Badlab” ambazo zikiboreshwa zitasaidia kurahisisha kazi zao.