Wanne mbaroni kwa kukutwa na kura, vurugu Mwanza
- Miongoni mwa waliokamatwa ni wakala na mgombea wa Chadema huku chama hicho kikieleza kuwa kuna ukiukwaji mkubwa wa taratibu za uchaguzi.
Mwanza. Watu wanne wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za matukio matatu tofauti likiwemo la vijana wawili makada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kukamatwa wakiwa na karatasi za kupigia kura 181.
Kukamatwa kwa watu hao ni mwendelezo wa sarakasi zinazoendelea katika Uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu ambao umefanyika leo na upigaji kura kuhitimishwa Saa 10:00 jioni.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema majira ya saa 1:30 asubuhi katika kituo cha kupigia kura cha Lwanhima B, mtaa wa Maliza vijana wawili ambao ni wakala wa Chadema, Edward Otieno na mgombea wa uenyekiti wa mtaa huo Atanasi Ndaki walichukua sanduku lenye karatasi za kupigia kura na kuondoka nazo.
“Mgombea huyo kwa kushirikiana na wakala huyo walichukua karatasi hizo na kuondoka nazo lakini kabla hawajafika mbali askari waliokuwa kwenye eneo hilo walifanikiwa kuwakamata na baada ya kufanya uchunguzi walibaini wagombea hao wakiwa na karatasi zingine zilizokuwa zimepigwa,” amesema Mutafungwa.
Tukio lingine ni wakala wa kituo cha Lwanhima A, Ally Hussein ambaye naye anashikiliwa kwa kosa la kukimbia na karatasi za kupigia kura 181 zikiwa zimehifadhiwa.
“Watuhumiwa hao wanashikiliwa na uchunguzi unaendelea,” amesema Mutafungwa.
Polisi pia wanamshikilia Katibu wa Chadema wilaya ya Nyamagana Amos Ntobi kwa kosa la kufanya fujo kwenye kituo cha kupigia kura cha Kabengwe mtaa wa Mabatini akidai kuwa kituo hicho kutokuwepo kwenye orodha ya kupigia kura.
“Alikuwa anawaambia watu wasiende kwenye kituo hicho kwa kuwa hakipo kwenye orodha ya vituo vya wapiga kura,” amesema Mutafungwa.
Kiongozi huyo wa polisi amesema wanaendelea kuwashikilia makada wa hao wa Chadema mpaka uchunguzi utakapokamilika. Hata hivyo, hakueleza ni lini wanatarajia kuwapeleka mahakamani.
Awali Chadema iliitaka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kusitisha upigaji kura katika vituo vyote ambavyo wakala wa chama hicho kikuu cha upinzani wamekamatwa.
Chadema wamekosa vikali uchaguzi huo wakieleza kuwa baadhi ya maeneo nchini kuna mawakala wao waliokamata karatasi za kura ambazo zilizokwisha kupigwa jambo linapunguza sifa za uchaguzi kuwa huru na haki.