Wanawake sekta ya Afya wanalipwa asilimia 24 pungufu ya wenzao wa kiume

July 15, 2022 8:07 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Muuguzi akijiandaa kutoa chanjo ya COVID-19 katika kijiji cha Kasungu nchini Malawi. Picha| UNICEF/Thoko Chikondi.


  • Hii inamaanisha kuwa wanawake wanalipwa kiwango cha chini zaidi kwenye soko la ajira.
  • Wanawake wanashikilia asilimia 67 ya nguvu kazi katika sekta ya afya.
  • Serikali zatakiwa kuziba pengo hilo na kuongeza usawa katika sekta ya afya.

Dar es Salaam. Ripoti mpya ya mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa (UN), imeeleza kuwa wanawake wanaofanya kazi katika sekta ya afya wanalipwa asilimia 24 pungufu ya wenzao wa kiume hata pale wanapokuwa na vigezo sawa katika soko la ajira. 

Jambo hilo linatajwa kuathiri ufanisi na mchango wao katika kuboresha sekta ya afya. 

Ripoti hiyo iliyopewa jina la  “uchambuzi wa kina zaidi duniani kuhusu ukosefu wa usawa wa kijinsia kwenye mishahara katika sekta ya afya” imetolewa Juni 14, 2022 jijini New York Marekani na mashirika mawili ya UN, lile la ajira duniani (ILO) na afya (WHO).

Ripoti hyo imefafanua kuwa pengo ghafi kati ya wanawake na wanaume ni takriban asilimia 20  lakini likiangaziwa kwa undani zaidi kwenye masuala kama elimu, umri na muda wa kufanya kazi pengo hilo linaongezeka na kufikia asilimia 24.

Hii inamaanisha kuwa wanawake wanalipwa kiwango cha chini zaidi kwenye soko la ajira ikilinganishwa na wanaume, licha ya kushikilia asilimia 67 ya nguvu kazi katika sekta ya afya.

Ripoti hiyo imegundua zaidi kuwa mishahara katika sekta ya afya ipo chini ikilinganishwa na sekta nyingine za kiuchumi. Hii inaenda sambamba na ukweli kwamba sekta za kiuchumi ambazo wanawake ndiyo wengi zinakuwa na mishahara ya chini. 

“Ushahidi na uchambuzi uliomo kwenye ripoti hii lazima utumike kuzijulisha serikali, waajiri na wafanyabiashara kuwa wanatakiwa kuchukua hatua madhubuti.

“Pia kutumia habari njema za mafanikio katika nchi nyingine zilizoongeza mishahara na kuwa na utashi wa kisiasa katika kuleta usawa wa kijinsia kwenye malipo, Mkurugenzi wa kitengo cha nguvukazi wa WHO Jim Campbell amesema wakati akihojiwa na redio ya UN jana.

Sababu za malipo duni

Zilipotafutwa sababu zinazofanya wanawake kulipwa kidogo kuliko wanaume walio na sifa sawa za soko la ajira katika sekta ya afya na huduma kote ulimwenguni kwa kiasi kikubwa ripoti hiyo hiyo imesema sababu hazijaelezwa. 

Mkurugenzi wa Idara ya masharti ya kazi na usawa wa ILO Manuel Tomei amesema  ripoti hii itasaidia kuchochea mazungumzo na hatua zinazohitajika kuleta usawa katika sekta ya afya.

“Hakutakuwa na ahueni jumuishi, dhabiti na endelevu bila sekta ya afya na huduma imara. Hatuwezi kuwa na huduma bora za afya na uangalizi bila mazingira bora na ya haki ya kufanya kazi ikiwa ni pamoja na mishahara ya haki kwa wafanyakazi wa afya,” amesema Tomei.

Amesema wakati umefika wa kuchukua hatua madhubuti za kisera ikijumuisha mazungumzo muhimu ya kati ya taasisi zinazohusika na sekta ya afya.


Tangazo


Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW