Ripoti: Athari za Corona kuwatesa zaidi wanawake kuliko wanaume

July 21, 2021 6:43 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Kati ya mwaka 2019 na 2020 ajira kwa wanawake zilipungua kwa asilimia 4.2 duniani sawa na kupoteza ajira milioni 54.
  • Serikali duniani zashauriwa kuandaa programu za kuwainua wanawake kiuchumi.

Dar es Salaam. Utafiti mpya ulifanywa na Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa (ILO) umeeleza kuwa wanawake wachache kati ya wengi waliopoteza ajira kutokana na athari za janga la Corona (Uviko-19) watakaoweza kupata kazi nyingine ikilinganishwa na wanaume. 

Taarifa ya utafiti huo mpya uliofanywa na shirika hilo na kutangazwa Julai 19 huko Geneva, Uswisi imesema kumekuwa na upotevu mkubwa wa ajira na mateso kwa wanawake katika kipindi cha janga hilo na bado wanawake wataendelea kuathirika. 

Utafiti unaonyesha kati ya mwaka 2019 na 2020 ajira kwa wanawake zilipungua kwa asilimia 4.2 duniani sawa na kupoteza ajira milioni 54, wakati wanaume waliathirika kwa asilimia 3 au ajira milioni 60. 

Hii inamaanisha kutakuwa na upungufu wa wanawake milioni 13 katika ajira mwaka huu ikilinganishwa na mwaka 2019, ilihali idadi wa wanaume katika ajira inatarajiwa kuongezeka kwa viwango vilivyoonekana katika miaka miwili. 

Kwa maana nyingine ni kuwa asilimia 43 tu ya wanawake walio kwenye umri wa kuajiriwa ndiyo watakaopata ajira mwaka 2021, ikilinganishwa na asilimia 69 ya wanaume ambao wanatarajiwa kupata ajira mwaka huu. 

Wanawake wamekuwa waathirika wakubwa kwenye ajira na kukosa kipato kwa sababu maeneo wanayofanyia kazi ikiwemo sekta ya malazi, chakula na utengenezaji yameathirika zaidi na janga la Corona.

Kwa upande wa Afrika, ajira kwa wanaume zimepungua kwa asilimia 0.1 kati ya mwaka 2019 na 2020, wakati ajira za wanawake zikipungua kwa asilimia 1.9. 

Wanawake wakiwezeshwa kifedha itawasaidia kupata mitaji na kujiajiri ili kujiongea kipato. Picha| Gift Mijoe.

Suluhu ya kumaliza tatizo hilo 

Nchi ambazo wanawake wameathirika zaidi na janga hilo wanaweza kutumia mbinu zilizotumiwa na baadhi ya nchi kulikwamua kundi hilo.

Kuna baadhi ya nchi ikiwemo Chile na Colombia, ruzuku ya mshahara ilitolewa huku kiwango cha juu ya ruzuku wakipewa wanawake.Colombia na Senegali zilikuwa miongoni mwa nchi zilizotengeneza au kuimarisha usaidizi kwa wanawake wajasiriamali. 

Wakati huo huo, Mexico na Kenya waliweka upendeleo maalum katika kuhakikisha wanawake wananufaika na ajira kwenye miradi ya umma.

Mbinu zingine ambazo ripoti hiyo imependekeza ni kuhakikisha kunakuwa na usawa katika malipo ya kazi, kutengeneza programu za kuwainua wanawake kiuchumi kwa kuwapatia fedha za mitaji na kuwapatia ajira ili wapate kipato.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW