Wananchi jicho la tatu kufuatilia miradi ya maendeleo
- Watakiwa kuwadhibiti viongozi ‘wapigaji’
- hiyo inawezekaan ikiwa watakuwa na taarifa sahihi za miradi katika maeneo yao.
Mwanza. Serikali imewataka wananchi kuhakikisha wanafuatilia kwa karibu miradi ya maendeleo katika maeneo yao ili kubaini kama inatekelezwa kwa ufanisi na kwa kiwango kilichokusudiwa.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Sengerema, Allan Mhina akizungumza leo Novemba 1, 2022 na wakazi kutoka kata nne za wilaya hiyo ya mkoani Mwanza ambao wanapatiwa mafunzo ya kujengewa uwezo wa kufuatilia miradi ya serikali, amesema si dhambi wananchi wakawa sehemu ya ufuatiliaji wa miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao kujiridhisha kama inatakelezwa kwa kiwango kilichokusudiwa.
Amesema katika mwaka wa fedha 2022/23, Wilaya hiyo imetengewa zaidi ya Sh30 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi minne ya maji.
“Miradi ni mingi na inatumia fedha nyingi za Serikali, hivyo ni vyema kuwa na jicho la tatu litakalotumika kufuatilia utekelezaji wa miradi hiyo na kutoa taarifa pale ambapo kuna watu wanaotaka kukwamisha malengo ya Serikali ya kuwahudumia wananchi,” amesema Mhina.
Serikali ina wakaguzi wengi wanaofuatilia mradi miradi ikiwemo Taasisi ya Kupammbana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) na Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) lakini wananchi ni sehemu ya jamii itakayotumika kufanya ufuatiliaji ili kukomesha vitendo vya ubadhirifu vinavyoweza kujitokeza.
Amesema zipo changamoto zinazojitokeza kwenye utekelezaji wa miradi hiyo ikiwemo tabia za watu za udokoaji wa mifuko ya saruji, nondo au misumari, hivyo kuwepo kwa watu wanaofuatilia miradi watakuwa mabalozi wazuri wa kupaza sauti na kutoa taarifa kwa wakati ili Serikali iweze kuchukua hatua stahiki na kwa wakati.
Soma zaidi:
Awali, Mwezeshaji wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa ufuatiliaji matumizi sahihi ya rasilimali za umma kwenye miradi ya maendeleo kutoka Chama cha Watu Wenye Ulemavu Tanzania (Chawata), Adam Ndokeji amesema matarajio yao ni kuona Serikali inaboresha huduma za maji na matumizi sahihi ya rasilimali za umma.
Amesema katika mradi huo wa miezi nane, wananchi watajengewa uwezo wa kubaini miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao na kuifuatilia kwa karibu.
Zaidi ya Sh39 milioni zimetengwa kwa ajili ya kufuatilia miradi ya maji, na kwa Wilaya ya sengerema ni kata nne ambazo ni Katunguru, Nyapande, Igalula na Nyamazuko.
Baadhi ya wananchi wa Sengerema wamesema mradi huo umekuja kwa wakati mwafaka ambapo huko nyuma walikuwa na maswali mengi lakini hawakuweza kupata majibu yake.
Didas Msongareli amesema ipo miradi mingi ambayo mingine ilianza kutekelezwa miaka 40 iliyopita na haijakamilika.
“Wananchi hatukuwa na sauti ya kuisemea kwa kuwa hatukujengewa uwezo wa namna ya kufanya ufuatiliaji hivyo kupitia mafunzo haya sasa tutaanza kufuatilia kwa kina na kuripoti taarifa mbalimbali zinazoweza kupatikana kwenye maeneo hayo,” amesema Msongareli.
Christina Edward amesema watashirikiana kwa karibuni na viongozi wa vijiji na kata ili kusaidia upatikanaji wa maji kwa wananchi.
Latest



