Takukuru yanusa upigaji wa fedha za miradi Mwanza
- Yaagiza marekebisho kwenye miradi minne yenye gharama ya Sh3.3 bilioni
- Ni miradi ya afya pamoja na elimu
Mwanza, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Mwanza imebaini kasoro katika utekelezaji wa miradi minne yenye thamani ya Sh3.3 bilioni ambapo imetakiwa kufanyiwa marekebisho ili kuendana na thamani halisi.
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, James Ruge aliyekuwa akizungumza na wanahabari Ofisini kwake leo Mei 29, 2023 amewaambia kuwa wamebaini kasoro hizo baada ya kufuatilia miradi 42 ya maendeleo katika kada za afya, elimu, na maji yenye thamani ya Sh26 bilioni.
Miradi iliyobainika kuwa na mapungufu ni pamoja na mradi wa ujenzi wa jengo la Wagonjwa wa Nje la zahanati ya Fumagila unaogharimu Sh131.5 milioni pamoja na mradi wa ujenz wa jengo la Wagonjwa wa ndani katika zahanati hiyohiyo wenye thamani ya Sh 122.2 milioni ambapo kulikuwa na ucheleweshaji wa malipo ma ununuzi wa vifaa.
“Tumemebaini usimamizi duni kwenye ujenzi wa shule ya Sekondari mpya ya Buhumbi wilayani Magu, unaogharimu Sh600 milioni ambao ulikamilishwa chini viwango na vifaa kuharibika,” amesema Ruge.
Mwanza inaendelea kukabiliwa na changamoto ya Rushwa katika utekelezaji wa miradi kwani ni miezi niwili tu imepita tangu Takukuru mkoani humo kubaini miradi 22 yenye thamani ya Sh6.5 bilioni kuwa na kasoro za utekelezaji.
Soma zaidi
-
Takukuru yanusa upigaji miradi 22 ya maendeleo Mwanza
-
Rais Samia aziagiza Takukuru, Zaeca kufuatilia na kuichukulia hatua miradi yenye kasoro
Miradi hiyo ni sawa na asilimia 21 ya miradi 130 ya maendeleo katika sekta mbalimbali yenye zaidi ya Sh30.44 bilioni inayotekelezwa mkoani humo.
Hali hiyo inaweza kusababisha wananchi kuchelewa kupata huduma muhimu za kijamii ikiwemo maji kuwawezesha kufanya shughuli za maendeleo na kuinua uchumi wa nchi.
Malalamiko 81 kuchunguzwa.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Takukuru amesema wanachunguza malalamiko 81 kati ya 90 ya vitendo vya rushwa yaliyopokelewa katika kipindi cha Januari-Machi, 2023.
Katika kipindi hicho Jamhuri ilishinda kesi tatu kati ya nne na kesi mpya nne zilisajiliwa mahakamani na kufanya idadi ya kesi 18 zinazoendelea kusikilizwa.
Ruge amebainisha kuwa katika kipindi cha Aprili hadi Juni mwaka huu, wataendelea kuzuia vitendo vya rushwa kwenye miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa kufanya ukaguzi na kusimamia kwa karibu matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali.
Latest