Wanakijiji wanavyosota kusaka maji usiku Mwanza

May 12, 2023 9:19 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link

Kwa vijana ni fursa kwa sababu husaka maji na kuwauzia watu wanaoshindwa kutembea umbali mrefu kwenda kwenye kisima hicho. Picha | Mariam John.


  • Wakazi wa Misungwi wanamka usiku kusaka maji.
  • Tatizo hilo linarudisha nyuma maendeleo ya wakazi wa Misungwi. 
  • Serikali yasema itawasogezea watu maji karibu na makazi. 

Mwanza.  Ni asubuhi na mapema, Flora Elias, mkazi wa Kitongoji cha Kagera Kata ya Usagara wilayani Misungwi, anafika kisimani kuchota maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

Ni mwendo wa saa 1:30 kwa mguu kutoka nyumbani kwake hadi kufika kilipo kisima hicho katika Kijiji cha Mwasonge ili kupata huduma hiyo ya maji.

Flora (35) hayupo peke yake. Ameambatana na wenzake kutoka maeneo mbalimbali katika vijiji vya Identemya na Nyang’omango ambao nao hutegemea maji hayo.

Kwa wastani kisima hicho huudumia watu watu 1,000 wa kijiji hicho na wengine wa vijiji jirani.

Mbali na kuamka mapema kuwahi foleni lakini kuna wakati hulazimika kukaa kisimani saa 2 hadi 3 wakisubiri maji yaongezeke kwa kuwa huwa yanakatika.

“Tunalazimika kutumia muda mrefu kukaa kisimani kwani kuna wakati maji hukatika na kuamua kusubiri kwa muda yaongezeke ndipo tuchote,” anasema Flora ambaye anajishughulisha na kuuza nyanya kijijini kwake. 

Flora hulazimika kuamka alfajiri kwenda kuchota maji ili kuwahi shughuli nyingine za nyumbani ikiwemo kuandaa watoto kwenda shule na kupikia chakula.

Anasema Serikali ingewasogezea huduma hiyo karibu ingewapunguzia changamoto ya kuamka usiku lakini pia wangetumia muda huo kujitafutia pesa kwa ajili ya kukuza uchumi wao.

Kwa sasa wanapata ahueni kwa sababu mvua zinazoendelea kunyesha zinawawezesha kuhifadhi maji kwa matumizi ya baadaye. Hata hivyo, hawana vifaa vya kuhifadhi maji kwa muda mrefu. 

“Mvua inaponyesha tunapumzika, tunatamani tungekuwa na msimu wa mvua mwaka mzima ili kupunguza adha hii ya kuamka usiku kwenda kutafuta maji, yenyewe si safi na salama ni machafu hayafi kwa kutumia lakini hatuna namna kwa kuwa hatuna maji mengine zaidi ya haya,” anasema Flora.

Mkazi mwingine katika Kitongoji cha Mawematatu, Zainabu Ally anasema maji hayo si salama kwakuwa kisima kipo wazi hivyo wadudu huingia humo na wakati mwingine wanyama hivyo kuwaweka katika hatari ya kupata magonjwa ya mlipuko. 

Zainabu anaiomba Serikali kuwapelekea miundombinu ya maji ili kuwaepushia na changamoto hizo.

Mbali na kuamka mapema kuwahi foleni lakini kuna wakati hulazimika kukaa kisimani saa 2 hadi 3 wakisubiri maji yaongezeke kwa kuwa huwa yanakatika. Picha | Mariam John.

Ni tabu juu ya tabu

Mabula Chebu, mkazi wa Kitongoji cha Usagara, Wilaya ya Misungwi anasema bila kuamka saa saba au nane usiku hauwezi kupata maji kwa kuwa watu ni wengi na hubeba ndoo nyingi za kuchotea.

Chebu ambaye ni mzee wa miaka 78 anasema ameishi katika kijiji hicho tangu alipozaliwa, tatizo la maji linazidi kuongeza kila kukicha tofauti na miaka ya nyuma ambapo watu walikuwa wachache.

“Zamani shida ya maji ilikuwepo lakini haiwezi kulingana na ya kipindi hiki ambapo bila kuamka usiku itakulazimu kwenda kushinda kisimani siku nzima ukisubiri maji,” anasema Chebu.


Ndoa nazo ziko shakani

Anasema wanapata changamoto ikiwemo ndoa kuvunjika ambapo wanawake kwa wanaume hawaaminiani kama wenza wao hufuata maji au kwenda kwa mahawala zao.

Kwa mujibu wa Chebu, viongozi wa Serikali ya kijiji wamekuwa wakisuluhisha migogoro ya ndoa mara kwa mara kutokana na wenza wao kutowaamini kama wameamka kufuata maji.

Anasema changamoto kubwa ni kwa wanawake ambao ni wahanga wa tatizo hilo ambapo pale wanapoamka ugomvi unaibuka wakiwatuhumu kuwa hawaendi kufuata maji isipokuwa wana mambo yao.

“Kumekuwa na changamoto nyingi hasa kwa wanawake wamekuwa wakipigwa na kufukuzwa na waume zao wakiwatuhumu kutoka nje ya ndoa kwani hawaamini kama wanawake hao wanaamka alfajiri kwenda kufuata maji,” amesema Chebu.


Soma zaidi:


Kufa, kufaana 

Pamoja na changamoto hiyo ya maji, kwa vijana ni fursa. Huchota maji katika kisima hicho na kusambaza mitaani.

Rashid Kanyabali, mkazi wa Kijiji cha Usagara anasema kwa siku anaingiza kati ya Sh10,000 hadi Sh20,000 kutokana na biashara ya kuuza maji kwenye nyumba za watu.

Kwa kutumia mkokoteni au baiskeli, Kanyabali hupanga madumu saba hadi nane na kuwapelekea wateja wake.

Anasema biashara hiyo ambayo huitegemea inamsaidia kukuza uchumi wake na kuhudumia familia.

Maji ambayo huwapelekea wateja wake yapo ya aina mbili ya chumvi na ambayo hayana chumvi na yanategemeana na bei zake ambapo kwa dumu la maji ya chumvi huuzwa Sh300 huku ambayo hayana chumvi ambayo hutumika kwa ajili ya kunywa huuzwa Sh500.

“Tumejipatia ajira kupitia kuuza maji tunapata pesa ya kula na matumizi ya nyumbani, ambapo kwa mteja huwa tunauza kuanzia madumu matano kwa Sh2,000 kama ni ya kunywa huku ya chumvi ambayo hutumika kufulia na kuoga tunauza kwa Sh1,500 kwa madumu matano,” anasema Kanyabali.

Changamoto wanayokutana nayo ni umbali mrefu na kuamka usiku kufuata maji kwani kuna wakati yanakatika hivyo inawalazimu kusubiri hadi yaongezeke ndipo wachote.

“Wasiwasi wangu ni kutembea maeneo tofauti kutafuta maji yakikatika kwenye kisima hiki tunaenda kwenye kisima kingine huko Kijiji cha Fella au Kanyerere ili tu kuhakikisha tunapata maji ya kuuza kwakuwa bila hivyo hatupati fedha ya kutumia,” anasema Kanyabali.

Usikose sehemu ya pili ya makala haya itakayoangazia namna Serikali inavyochukua kukabiliana na tatizo la maji Misungwi.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...