Wanafunzi zaidi ya 700,000 wachaguliwa kujiunga kidato cha kwanza 2020

December 5, 2019 11:10 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na waziri huyo, zaidi ya nusu au asilimia 57.9 ya wanafunzi waliokosa nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza wanatokea kwenye mikoa minne ya Kigoma, Mara, Simiyu na Dar es Salaam. Picha| Doug/Unsplash.

  • Waliotangazwa ni asilimia 92 ya wanafunzi waliofaulu.
  • Wasichana waongoza kwa idadi ya watakaojiunga baada ya kufikia asilimia 52 ya watoto wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza

Dar es Salaam. Wanafunzi zaidi ya 700,000 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka 2020 ikiwa ni moja ya hatua muhimu katika safari yao ya elimu maishani.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo amewaambia wanahabari  jijini Dodoma leo (Desemba 5, 2019) kuwa wanafunzi hao 701,038 ni sawa na asilimia 92.27 ya waliofaulu mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi mwaka huu. 

Kati ya waliotoboa kwenda kidato cha kwanza, watoto wa kike wanaongoza kwa wingi baada ya Jafo kueleza kuwa wanafunzi 365,525 sawa na asilimia 52.14 au zaidi ya nusu ya jumla ya wanafunzi wote waliochaguliwa kuwa ni wasichana. 

“Jumla ya wanafunzi 58,699 sawa na asilimia 7.73 wakiwemo wavulana 28,567 sawa na asilimia 48.53 na wasichana 30,132 sawa na asilimia 51.33 ya waliofaulu, hawakupata nafasi ya kuchaguliwa kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa,” amesema Jafo.

Mkoa wa Kigoma unaongoza kwa kuwa na wanafunzi wengi watakaolazimika kungojea neema ya kuchaguliwa kutokana na uhaba wa madarasa.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na waziri huyo, zaidi ya nusu au asilimia 57.9 ya wanafunzi hao waliokosa nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza wanatokea kwenye mikoa minne ya Kigoma, Mara, Simiyu na Dar es Salaam. 

Mikoa hiyo minne ni kati ya mikoa 13 iliyotajwa kuwa na wanafunzi waliokosa nafasi kwa uhaba wa vyumba vya madarasa. Mkoa wa Kigoma unaongoza kwa kuwa na wanafunzi wengi 12,092 ikifuatiwa na Mara yenye wanafunzi 9,493.

Mkoa wa Simiyu una wanafunzi 6,616 wasiochaguliwa huku Dar es Salaam ikiripotiwa kuwa na wanafunzi 5,808.

Mikoa mingine yenye uhaba wa vyumba hivyo muhimu ni Iringa, Lindi, Manyara, Mara, Mbeya, Pwani, Rukwa, Songwe na Tanga.


Zinazohusiana


Jafo ameagiza wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kusimamia mapokezi ya wanafunzi waliochaguliwa huku akitoa agizo la vyumba vya madarasa kwenye mikoa iliyobakiza wanafunzi vikamilike ifikapo Februari 29, 2020.

“Makatibu tawala wa mikoa na wakurugenzi wa halmashauri husika wasimamie utekelezaji wa agizo hili ili kuhakikisha wanafunzi wote waliobaki wanajiunga na kidato cha kwanza ifikapo tarehe 02/03/2020,” amesema Jafo.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW