Wanafunzi wanavyoweza kusoma wakati wakijikinga na Corona vyuoni

June 1, 2020 5:59 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Serikali za wanafunzi zimesema zimejiandaa na kuweka sheria za lazima ili kuepusha maambukizi vyuoni.
  • Wanafunzi wamesema wapo tayari kuendelea na masomo huku silaha yao ikiwa ni barakoa na vitakasa mikono.
  • Wataalamu wa afya washauli matumizi ya matunda yenye vitamini C yakiwemo machungwa na ubuyu mweupe.

Dar es Salaam. Zimebaki siku chache kwa vyuo vya Tanzania kufunguliwa tena Juni mosi baada ya kufungwa kwa miezi miwili kutokana na janga la ugonjwa virusi vya Corona. 

Kufunguliwa kwa vyuo hivyo ni agizo la Rais John Magufuli alilolitoa Mei 21 jijini Dodoma kufuatiwa kupungua kwa ugonjwa huo nchini. 

Kwa sasa vyuo mbalimbali na wanafunzi wameanza maandalizi ya kuhakikisha wanachukua tahadhari zote za kujikinga na ugonjwa huo wakati watakaporejea masomoni wiki ijayo. 

Kiongozi wa serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini Kampasi ya Dar es Salaam (TUDARCo) Lucas Moreto ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa chuo hicho kimejiandaa kwa kununua vifaa vya kupimia joto na vitakasa mikono. 

“Kila mwanafunzi na mfanyakazi anayeingia chuoni lazima apimwe joto kuanzia getini na pia kutakuwa na vitakasa mikono kwenye kila darasa,” amesema Moreto.

Amesema pia watahakikisha wanafunzi wanapeana nafasi wanapokuwa darasani na kuzingatia umbali unaopendekezwa na wataalam wa afya. 

“Kama Serikali ya wanafunzi tutaanza kutoa matangazo kwa wanafunzi leo kuwakumbusha kujiandaa kwa kuwa na barakoa pamoja na vitakasa mikono,” amesema kiongozi huyo. 

Aidha, watagawa barakoa za kufua kwa wanafunzi wasio na uwezo wa kununua bidhaa hiyo ili kuhakikisha kila mwanajumuiya wa chuo anakuwa salama bila kujali hali yake. 

Wanafunzi wanashauriwa kuendelea kupeana nafasi ya mita moja na kuzowea mazingira mapya kwenye maisha yao ya chuo yanayoanza Juni 1. Picha| The College Planning Center.

Baadhi ya wanafunzi wa vyuo mbalimbali walioongea na Nukta wamesema watahakikisha wanaporudi vyuoni wanazingatia maelekezo ya wataalam wa afya kuhusu kujikinga na Corona.  

Mwanafunzi wa mwaka wa tatu anayesomea shahada ya kwanza ya misitu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) Kennedy Luhende  amesema atahakikisha ananawa mikono mara kwa mara na kufanya mazoezi.

“Nimejipanga kuendeleza na kuimarika katika suala la mazoez ya viungo na kukimbia ili kuuwezesha mwili kupata kinga yake ya asili dhidi ya magonjwa,” amesema Luhende.

Naye Mediatrice Raphael ambaye pia ni mwanafunzi wa SUA amesema hana hofu yoyote na anawekeza nguvu zake katika masomo na kuchukua tahadhari dhidi ya COVID-19 ili akamilishe ndoto zake akiwa chuoni. 

Kwa upande wake Christopher Sise  ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) akisomea shahada ya Uhandisi wa Mazingira amesema kwake kurudi chuoni ilikuwa taarifa njema kwani yupo mwaka wa mwisho na asingependa kuingia mwaka 2021 bila kumaliza masomo yake.

“Nafurahishwa na tamko la Rais wetu kwa kuruhusu shughuli mbalimbali pamoja na vyuo kuendelea. Ni sahihi zaidi kufanya suala zima la elimu ya juu kuendelea,” amesema Sise.


Zinazohusiana


Wataalam wa Afya nao watoa neno

Naye Daktari kutoka Kituo cha afya cha Ngarenanyuki cha jijini Arusha, Jonas Kaguo amesema ni muhimu kwa wanafunzi kuacha kugandana kama walivyozowea na badala yake,  kutazamia tahadhari ya kupeana nafasi ya mita moja baina ya mmoja na mwenzie.

Zaidi, mtaalamu huyo ameshauri wanafunzi hao wapendelee kula matunda yenye Vitamin C yakiwemo mapera, ubuyu mweupe, machungwa na malimao.

“Wafanye mazoezi. Ikiwezekama mara mbili na isipungue mara moja kwa siku. Na wahakikishe wanakunywa maji ya kutosha na matunda. Kuna matunda yanayopatikana kwa bei ndogo kama machungwa na malimao,” amesema Dk Kaguo.

Amesema vyakula vivyo na mazoezi yatasaidia kuimarisha kinga na hivyo kuongeza kinga dhidi ya magonjwa ikiwemo Corona. 

Enable Notifications OK No thanks