Vyuo vya Tanzania sasa kufunguliwa Juni mosi

May 21, 2020 8:50 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya Rais Magufuli kusema maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Corona yamepungua.
  • Wanafunzi kidato cha sita nao watakiwa kurudi shuleni. 
  • Michezo nayo kurejea tarehe hiyo.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameagiza vyuo vyote nchini Tanzania kufunguliwa Juni 1, 2020 sambamba na kuruhusu michezo mbalimbali ianze tena siku hiyo.

Sanjari na hatua hizo, Rais Magufuli ameagiza wanafunzi wa kidato cha sita nao kuanza masomo Juni mosi na wapewe mafunzo maalumu yatakayowasaidia kujiandaa vyema na kujiunga na vyuo vikuu. 

Dk Magufuli amesema kwa sasa maambukizi ya virusi vya Corona nchini yamepungua san  hivyo Serikali imeanza kuruhusu shughuli mbalimbali kurejea kama ilivyo kuwa awali. 

“Tumeamua sisi kama Serikali vyuo vyote vifunguliwe Juni 1, 2020,” amesema Rais leo (Mei 21, 2020) wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni akiwemo Naibu Waziri wa Afya Dk Godwin Mollel katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma. 

Amezitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Wizara ya Fedha na Mipango kujiandaa vema ikiwemo kuwapatia wanafunzi mikopo kwa wakati na kutatua kwa haraka changamoto zote kabla ya vyuo havijafunguliwa. 

Sambamba na hilo ameruhusu wanafunzi wa kidato cha sita kurudi shuleni tarehe hiyo ya Juni mosi ili waendelee na masomo na kujiandaa na mtihani wao wa kuhitimu mwaka huu. 

“Wizara ya Elimu ipange mikakati ya crash program (programu za dharura) ili vijana hawa wafanye mtihani wao ya kidato cha sita bila  kuharibu trend (mwenendo) ya wao kuingia vyuo vikuu kama ilivyokuwa imepangwa,” amesema Rais.

Wakati wanafunzi wa kidato cha sita wakiruhusiwa kurudi shule, amesema wale wa shule za msingi na sekondari wasubiri kwanza wakati Serikali ikiendelea kufanya tathmini ya hali ya maendeleo ya ugonjwa huo. 


Zinazohusiana


Michezo rasmi Juni 2020

Wapenda michezo nao wataanza kuburudika kuanzia Juni mosi baada ya mkuu huyo wa nchi kuruhusu michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu iliyokuwa imesimama akisema  ina mchango mkubwa katika kupambana na magonjwa ikiwemo Corona.

“Ni lazima watu waanze michezo, sasa taratibu za watu kushangilia na kuangalia zile zinaweza kupangwa vizuri na Wizara ya Afya pamoja na wizara husika ya michezo ili ile variation ya distance (tofauti ya umbali ya mtu na mtu) ikaendelea kuwepo katika kipindi cha mpito kadiri tunavyoenda,” amesema Rais Magufuli. 

Vifaa vya kupambana na Corona kuthibitishwa

Katika hatua nyingine, Dk Magufuli ameigiza kuwa misaada ya vifaa vyote vinavyotolewa na watu mbalimbali kupambana na Corona ni lazima ipitie kwanza Wizara ya ya Afya ili vithibitishwe kama vinafaa kwa matumizi. 

Amesema kama inawezekana ni vema Tanzania ikatengeneza vifaa vyake ili kuongeza usalama zaidi wakati wa kuvitumia ili kuongeza ajira na kubana matumizi ya kununua. 

“Kwa mtu yoyote atakayepewa vifaa vya Corona halafu mkapima mkakuta yana Corona huyo mtu apelekwe kwenye kesi ya jinai hata ya mauaji kama wauaji wengine,” amesisitiza.

Enable Notifications OK No thanks