Corona inavyoathiri kazi za wanamuziki Tanzania

April 24, 2020 10:21 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Wameshauriwa kuangazia mitandao ya kijamii ikiwemo Youtube na Instagram.
  • Kupitia mitandao hiyo ni rahisi kujiingizia kipato hata kama ni kidogo lakini ni bora kuliko hamna..
  • Wadau wamesema kuendana na wakati ni muhimu kwa wasanii ili kuendelea kupeleka mkono kinywani.

Dar es Salaam. Wanamuziki wa Tanzania ambao shughuli zao zimeathiriwa na janga la virusi vya Corona wametakiwa kubuni fursa za mtandaoni zitakazowasaidia kuendelea kupata ili kuboresha maisha yao.

Kutokana na kuenea kwa virusi hivyo vya COVID-19, mikusanyiko ya watu hasa matamasha ya muziki yamezuiliwa kwa muda ikiwa ni tahadhari ya kuwakinga watu na ugonjwa huo hatari. 

Marufuku hiyo ya mikusanyiko imeleta athari nyingi hasa kwa wanamuziki ambao walikuwa wakitumbuiza katika maeneo mbalimbali na kujipatia kipato kwa ajili ya maisha yao. 

“Siyo rahisi. Mtu akiwa amezoea “show” (kutumbuiza)  za kumpa 100,000 au 150,000 kwa wiki alafu saizi hamna lazima hali iwe tete. Hapo atakayepona ni yule aliyekuwa akijiwekea akiba,” anasema Sharifa Ferouz ambaye ni mtumbuizaji katika hoteli ya Johari Rotana na Serena za jijini Dar es Salaam. 

Ferouz ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa kuna kila sababu wanamuziki wa Tanzania kubuni njia mbadala ya kupata kipato kipindi hiki cha mlipuko wa COVID-19. 

Hata hivyo, katika kila changamoto, huenda inawezekana kutafuta ufumbuzi ili maisha yaweze kuendelea. Ni kipi kinaweza kufanyika ili wasanii wa muziki  waweze kupata hata kama fursa za matamasha na au kutumbuiza mubashara hakupo tena?

Mikusanyiko ya watu hasa matamasha ya muziki yamezuiliwa kwa muda ikiwa ni tahadhari ya kuwakinga watu na ugonjwa wa corona na kubaki ukiwaathiri wanamuziki. Picha| Giphy.

Wadau wa sanaa ya muzikii wameongea kuhusu hali hiyo na hiki ndicho walichosema

Mwanzilishi mwenza wa kampuni ya JamiiForums Mike Mushi ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa kutokuwepo kwa matamasha siyo mwisho wa wasanii kwani kwa ulimwengu wa sasa kuna namna nyingi za kutengeneza pesa mtandaoni.

Mushi ambaye ni mdau wa muziki amesema wanamuziki wanaweza kuangazia fursa za kuonyesha kazi zao katika mitandao mbalimbali ikiwemo Youtube, Spotify na Boom Play.

“Hakuna njia rahisi. Unaweza kutengeneza maudhui na kama maudhui yako ni mazuri kiasi cha mtu kilipia kukutazama, hawezi kushindwa kununua bando ili aangalie maudhi yako kwenye Youtube,” amesema Mushi.

Majukwaa hayo yanatumika kama njia ya kuuza kazi za wasanii na kuwaunganisha na mashabiki wao waliopo katika maeneo mbalimbali duniani. 

Lakini wanaweza kuandaa matamasha ya mtandaoni ambapo watu wanaweza kulipia kiasi fulani cha fedha kuwaona wanamuziki wakiimba mubashara katika nyumba zao. 

Mfano Aprili 18, 2020, Shirika la Afya Duniani (WHO) likishirikiana na Shirika la Utetezi wa Kimataifa la Global Citizen walifanya tamasha  la muziki mtandaoni la  “Together At Home” yaani Pamoja Nyumbani lililolenga kuunga mkono juhudi za watumishi wa sekta ya afya wanaopambana na virusi vya corona.

“Unaweza kutengeneza maudhui na kama maudhui yako ni mazuri kiasi cha mtu kilipia kukutazama, hawezi kushindwa kununua bando ili aangalie maudhi yako kwenye Youtube,” amesema Mushi. Picha| Giphy.

Msanii wa miondoko ya HipHop kutoka kundi la Weusi George Mdeme almaarufu kama G-Nako amesema ni wakati sasa kwa wasanii kutunga nyimbo nyingi na kuweka hadharani nyimbo hizo kwa mashabiki ili wazisiikilize. 

“Kuachia kazi zako ambazo hazikuwa sokoni, itampatia msanii uwezekano wa kuendelea kujiingizia kipato,” amesema G-Nako.

G-Nako ameimabia Nukta kuwa kwa upande wake, kibao cha Trendakee alichoshirikiana na Marissa amekitoa hivi karibuni ili kuendelea kubaki kwenye masikio ya mashabiki wake. 

Amesema wasanii wengine wanaweza endelea kufanya hivyo kwani ni njia moja ambayo itaendelea kuwaweka sokoni.

Zaidi rapa huyo amewashauri wasanii wenzake wanaopitia wakati mgumu kwa sasa kuangazia mitandao mingine ikiwemo ya TikTok ambayo watu wengi wanaitumia kwa sasa wakiwa majumbani kama sehemu ya kupata kipato kuliko kukosa kabisa.

Wakati wasanii wa Tanzania wakiendelea kujiimarisha Youtube, wana kila sababu ya kupanua wigo wa kuyafikia masoko mengine ya mtandaoni zikiwemo programu tumishi za simu ili kuongeza idadi ya mashabiki na kipato pia.


Zinazohusiana


Mwanamuziki Grace Matata, yeye ameelezea njia ya aina yake ya kujiiingizia kipato ambayo inaweza kuwa msaada mkubwa kw awasanii kipindi hiki ambacho Corona inasambaa duniani. 

“Unaweza kwenda na wakati ukatengenza tangazo la kuosha mikono huku ukiingia ubia na mtengenezaji wa sabuni ambaye atakulipa kidogo. Huwezi kukosa pesa za hapa na pale,” amesema Grace.

Zaidi, mwanamuziki huyo amesema kutengeneza maudhui hakutegemei Youtube peke yake. Ni lazima uwe na uwezo wa kuenda na wakati.

Wadau hao wameshauri wasanii kuutumia muda huu vizuri kwa kurekodi nyimbo za kutosha na kuwa waangalifu kwenye matumizi ya fedha ikiwemo kuepuka starehe na kufanya uwekezaji wowote na kujiweka mbali na mikopo.

Enable Notifications OK No thanks