Waliofanya usaili wa maandishi TRA kujua mbivu na mbichi Aprili 25
- Matokeo yatatangazwa baada ya kuwasilishwa na mshauri elekezi, kutoka Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA).
Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imebainisha kuwa matokeo ya usaili wa maandishi kwa waombaji wa nafasi za kazi katika taasisi uliofanyika Machi 29 na 30 mwaka huu, yatatangazwa rasmi Aprili 25, 2025, kupitia tovuti yake ya www.tra.go.tz.
Huenda taarifa ya TRA ikawapa ahueni waoambaji wa nafasi hizo mara baada ya kuanza kusambaa kwa majina yanayodaiwa kuwa ya waliofaulu usaili katika mitandao ya kijamii ambayo hata hivyo mamlaka hiyo iliyakanusha na kubainisha ni ya mwaka 2023.
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala wa TRA, Moshi J Kabengwe, amesema kuwa matokeo hayo yatatangazwa baada ya kuwasilishwa na mshauri elekezi, kutoka Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), ifikapo Aprili 23, 2025.
Kabengwe ameweka wazi kuwa baada ya kutangazwa kwa majina ya waliofaulu usaili wa maandishi, usaili wa vitendo kwa kada za madereva na waandishi waendesha ofisi utafanyika kuanzia Mei 2 hadi 4, 2025 na usaili wa mahojiano kwa kada nyingine utafanyika kwa siku tatu kuanzia Mei 7 hadi 9, 2025.
“Baada ya usaili wa mahojiano, majina ya waliofanikiwa yatatangazwa Mei 18, 2025, na mafunzo elekezi yataanza Mei 22 hadi Juni 2, 2025, ambapo baada ya hapo waajiriwa wapya wataanza kazi rasmi,” amesema Kabengwe.
Katika mchakato wa usaili, TRA ilipokea jumla ya maombi 112,952, ambapo baada ya maombi 71 kukata rufaa, idadi hiyo ilifikia 113,023.
Waombaji waliokidhi vigezo walikuwa 86,314 na kati yao, 78,544 walihudhuria usaili wa maandishi, sawa na asilimia 91, huku waombaji 7,770 wakishindwa kufika kwa sababu mbalimbali.
Latest



