Serikali yawaita wahitimu wa kidato cha nne kubadili tahasusi, chuo
- Yatoa siku 30 kuanzia Machi 31 Hadi Aprili 30.
Arusha. Serikali ya Tanzania imefungua dirisha kwa wahitimu wa kidato cha nne mwaka 2024 kubadili tahasusi na kozi kabla ya kuanza kwa muhula mpya wa masomo wa 2025/26.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa aliyekuwa akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam leo Aprili 2, 2025 amesema kuwa wahitimu hao watapata nafasi ya kubadili tahasusi na kozi kwa mujibu wa ufaulu wao.
“Ni matumaini yangu kuwa wahitimu wote watatumia kwa ukamilifu fursa waliyopewa ya kubadilisha tahasusi na kozi kulingana na ufaulu waliopata pia wataweza kusoma kozi au tahasusi ambazo wamefaulu vizuri ama wana lengo nayo zaidi,” amesema Mchengerwa.
Mchengerwa amefafanua kuwa zoezi hilo litafanyika kwa njia ya mtandao kuanzia Machi 31, 2025 hadi Aprili 30, 2025.

miongoni mwa wanahabari na watumishi wa Serikali waliohudhuria mkutano wa wanahabari jijini Dar es Salaam leo Aprili 2, 2025.Picha/Ortamisemi.
Kwa mujibu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wahitimu hao wa kidato watachagua miongoni mwa tahasusi 65 zilizosajiliwa kutumika katika sekondari ya upili (advanced secondary education) Julai mwaka 2024.
Ili kubadili tahasusi au kozi Mchengerwa amesema mwanafunzi atalazimika kutumia mfumo wa uchaguzi wa wanafunzi (MIS) unaopatikana kupitia kiunganishi cha Selform.Tamisemi.go.tz.
Baada ya kuingia katika kiungo hicho mwanafunzi atahitajika kutumia namba ya mtihani, jina lake la mwisho, mwaka wa kuzaliwa na alama za ufaulu katika somo lolote ambalo mfumo utauliza ili kuanza kufanya uchaguzi wa tahasusi.
Aidha, Mchengerwa amewataka wanafunzi na wazazi kutumia muda uliotolewa vizuri kwa kuwa Tamisemi haitatoa muda wa ziada mara baada ya dirisha la kufanya maboresho kufungwa na ikiwa watakutana na changamoto yoyote watafute ushauri wa kitaaluma au kuwasiliana na kituo cha huduma kwa wateja cha wizara hiyo.
“Endapo mwanafunzi akipata changamoto awasiliane na kituo cha huduma kwa wateja kwa barua pepe huduma@tamisemi.go.tz au kupitia kituo cha huduma kwa wateja kwa namba 255262160210 au 255735160210,” amesema Mchengerwa.
Latest



