Si kweli: TRA wametoa matokeo ya usaili wa nafasi za kazi 

April 2, 2025 10:52 am · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • TRA imewataka wananchi kuipuza taarifa hiyo ya upotoshaji.

Dar es Salaam. Huenda wewe ni miongoni mwa watu waliokutana na taarifa zinazosambaa  kwenye mitandao ya kijamii, hususan X (zamani Twitter) zikidai kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa matokeo ya usaili kwa nafasi mbalimbali za ajira. 

Taarifa hii ya upotoshaji huenda imechochewa na tamko la TRA lililotolewa Machi 12, 2025, jijini Dodoma wakati wa kuwasilisha mafanikio yake katika kipindi cha miaka minne ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Katika taarifa hiyo, Kamishna Mkuu wa TRA Yusuph Mwenda, alibainisha kuwa mamlaka hiyo ipo katika mchakato wa kuwaajiri watumishi 1,596 ili kufikia jumla ya wafanyakazi 8,585.

Siku chache  baadaye TRA ilitangaza majina ya walioitwa kwenye usaili wa nafasi hizo ambapo usaili ulifanyika Machi 29 na 30.

Baadhi ya watu wenye nia ovu wameanza kusambaza taarifa kuwa tayari TRA imeshatoa majina ya waliofaulu usaili wa kuandika jambo ambalo si kweli.

Kupitia ukurasa wake rasmi wa Instagram, TRA imeeleza kuwa matokeo yanayozungumziwa ni ya usaili wa mwaka 2023.

Aidha, mamlaka hiyo imewahimiza Watanzania kuwa waangalifu na kujiepusha na taarifa za upotoshaji zinazosambazwa mitandaoni.

Hata hivyo, taarifa hiyo inayosambazwa haina nembo rasmi ya mamlaka hiyo jambo linaloashiria kuwa haijatolewa na chanzo halali. 

Aidha, kwa jambo lenye maslahi makubwa kwa jamii kama hilo taarifa lazima ingetolewa kwenye vyombo vya habari na kuchapishwa kwenye kurasa rasmi za TRA ikiwemo tovuti na mitandao yake ya kijamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks