Idara ya Uhamiaji Tanzania yatahadharisha umma na utapeli wa ajira 

April 2, 2025 12:06 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Yasema haijatoa tangazo lolote la ajira hivi karibuni.
  • Yaanzisha uchunguzi kuwabaini wanaolaghai wananchi.

Dar es Salaam.  Idara ya Uhamiaji nchini  imewatahadharisha Watanzania dhidi ya matapeli wanaotumia mitandao ya kijamii na simu za mkononi kuwalaghai watu kwa ahadi za uongo za ajira ndani ya jeshi hilo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Aprili 2, 2025 na Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Paul J. Mselle, matapeli hao wamekuwa wakituma ujumbe kwa njia ya SMS au kupiga simu kwa baadhi ya wananchi, wakiwataka kutuma fedha kwa madai kuwa watawasaidia kupata nafasi za ajira katika idara hiyo.

Hata hivyo, idara hiyo yenye jukumu la kuwezesha na kudhibiti masuala ya uhamiaji nchini haijatangaza nafasi yoyote ya ajira tangu ilipofanya hivyo Novemba 29, 2024 ambapo vijana wa kitanzania wenye sifa stahiki walitakiwa kutuma maombi kwa mtandao kupitia mfumo wa ajira wa idara hiyo. 

Januari 9, 2025 idara hiyo ilitoa tangazo la wito kwenye usaili kwa vijana wa kitanzania waliokidhi vigezo vya nafasi za kazi liiwataka kufika kweye usaili Januari 25, 2025 ambapo vijana waliofusu usaili walitakiwa kuripoti kwenye vituo walivyopangiwa kwa ajili ya mafunzi Machi Mosi 2025.

Ingawa, Februari 24, 2025 Idara ya Uhamiaji ilitoa tangazo la mabadiliko ya tarehe ya kuripoti kwenye mafunzo na kuwataka vijana hao kuripoti kwenye vituo vya mafunzo Machi 5, 2025 na tangu hapo hakuna tangazo lingine la ajira au wito kwenye mafunzo lililotolewa na Idara ya Uhamiaji Tanzania.

Mselle amesisitiza kuwa mchakato wa ajira katika Idara ya Uhamiaji tayari umekamilika kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizotangazwa rasmi wakati wa kutangaza nafasi hizo. 

“Idara inapenda kuufahamisha umma kuwa ajira zilishatangazwa na mchakato wake ulikamilika kwa kufuata sheria. Wananchi wanapaswa kupuuza taarifa zozote za uongo zinazotolewa na watu wasio waaminifu na badala yake watoe taarifa kwa vyombo vya usalama,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, Idara ya Uhamiaji imebainisha kuwa inaendelea na uchunguzi wa kina ili kubaini wahusika wa uhalifu huo na kuwachukulia hatua za kisheria.

Wananchi wanakumbushwa kufuatilia taarifa rasmi kupitia mifumo ya mawasiliano ya idara hiyo, ikiwemo mitandao yake ya kijamii yenye jina la UhamiajiTz pamoja na vyombo vya habari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks