Wakuu wa mikoa wapewa rungu kuzuia machinga barabarani
- Awataka kuwarudisha machinga katika masoko waliyopangiwa, kutatua kero.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewaagiza wakuu wa mikoa kusimamia zoezi la kuwaondoa machinga barabarani na kushughulikia kero zinazolikabili kundi hilo.
Kauli ya Rais Samia inakuja ikiwa ni miezi sita tangu kuanza kwa utekelezaji wa marufuku ya machinga kutokupanga bidhaa zao barabarani iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila.
Licha ya maagizo ya mkuu huyo yaliyotolewa Machi 4 mwaka huu, utekelezaji wake umekuwa ukisuasua huku baadhi ya machinga wakiripotiwa kurudi barabarani hususani katika baadhi ya barabara za Kariakoo.
Akizungumza katika hafla ya uapisho wa viongozi wapya iliofanyika katika Ikulu Ndogo ya Tunguu, Zanzibar leo Septemba 2, 2026, Rais Samia amewataka wakuu hao kutumia mbinu rafiki kuwarudisha machinga katika maeneo yao.
“Twende tukasimamie hayo si kwa kuwapiga fimbo na wale askari wa akiba sijui mgambo kwenda kuwanyanganya vitu vyao na kupiga mateke,hapana ni kwa mipango mizuri , tuwapangie mipango mizuri watoke waliko warudi kwenye masoko;” amesema Rais Samia.

Dar, Dodoma, Mwanza na Arusha, Mbeya vinara
Aidha, Samia amebainisha kuwa tabia ya wafanyabiashara kurudi kufanya biashara maeneo yasiyoruhusiwa inajurudia kwa kiasi kikubwa licha Serikali kujenga masoko makubwa katika majiji kama Dar es Salaam,Dodoma,Arusha, Mwanza pamoja na Mbeya.
Kiongozi huyo wa nchi amewataka wateule wake ngazi ya mkoa kushughulikia sababu za machinga hao kurudi barabarani ikiwemo kupanua masoko na kuanzisha njia mpya za daladala zinazofika katika masoko hayo.
“Na kama kelele ni daladala hazifiki kule hakuna wateja tengeneza ruti daladala zishushe pale ili wafanyabiashara wapate wateja wa kununua bidhaa zao kuna mambo madogo madogo yanayowafanya watoke warudi mitaani nendeni kasimamie lakini maeneo mengine ni ufinyu wa nafasi katika masoko mapya yaliyojengwa halmashauri jitahidini mjenge masoko mengine;” amesema Rais Samia.