Wakulima Tanzania kupata ruzuku ya mbegu na mbolea kidigitali

December 19, 2024 6:24 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Lengo la mpango huu ni kupunguza gharama za uzalishaji, kuongeza tija katika kilimo,
  • Wakulima na mawakala wamehimizwa kufuata taratibu zote za usajili na matumizi ya mfumo wa kidigitali.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema mfumo mpya wa kigitali wa kusajili wakulima uliobuniwa hivi karibuni utasaidia wakulima kupata ruzuku ya mbolea kwa urahisi hivyo kuongeza uzalishaji wa mazao na kuongeza tija katika kilimo.

Zoezi hilo la kusajili wakulima kidigitali ambalo limeanza kufanyika katika baadhi ya maeneo nchini kwenye ngazi ya kijiji na kata linatarajiwa kurahisha uoatikanaji wa pembejeo  na kupunguza ubadhirifu uliokuwa ukifanyika awali uliosababisha baadhi ya wakulima kukosa ruzuku hiyo.

Gerson Msigwa, Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo Disemba 19, 2024, jijini Dar es Salaam, watakaohusika kuwaingiza wakulima katika mfumo huo wa kidigitali ni maafisa kilimo.

“Baada ya usajili, wakulima watapokea ujumbe mfupi kupitia simu zao ukiwapa namba za siri zitakazotumika kununua mbegu na mbolea za ruzuku kulingana na ukubwa wa shamba na aina ya zao walizoanisha wakati wa usajili,” amesema Msigwa.

Mfumo wa ruzuku unaoratibiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) ulianza kutekelzwa mwaka 2003/2004, ambapo Agosti 8,2022, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alizindua rasmi mfumo wa kidijitali wa utoaji wa mbolea ya ruzuku.

Msigwa amewaambia wanahabari kuwa lengo la mpango huu ni kupunguza gharama za uzalishaji, kuongeza tija katika kilimo, kuimarisha usalama wa chakula na kuhakikisha upatikanaji wa malighafi kwa viwanda.

Baadhi ya waandishi wa habari kutoka vituo mbalimbali na viongozi wa Serikali wakimsikiliza Msemaji wa Mkuu wa Serikali leo Disemba 19,2024. Picha/ Fatuma Hussein.

“Utoaji wa ruzuku unazingatia taarifa sahihi za mkulima na bajeti ya Serikali. Tunatoa angalizo kwa wakulima kuepuka kutumia namba za simu za watu wengine wakati wa usajili,” amesisitiza Msigwa.

Kwa mujibu wa Msigwa, hadi kufikia Novemba 30, 2024, wakulima milioni 4.14, kampuni 31, mawakala 2,877 wa mbolea, mawakala 666 wa mbegu na vituo vya mauzo 7,000 vimesajiliwa.

Aidha, Msigwa amethibitisha kuwa katika msimu wa mvua wa 2024/2025, wakulima kutoka mikoa iliyopata mvua tangu Oktoba wameanza kunufaika na ruzuku hiyo kipindi cha Julai hadi Novemba, ambapo tani 253,669.3 za mbegu zenye thamani ya Sh435 bilioni zimenufaisha wakulima, huku ruzuku ya Serikali ikiwa ni Sh90 bilioni.

Mbolea ya ruzuku ikiwa imehifadhiwa katika moja ya maghala ya kuhifadhia mbolea yaliyopo mkoani mkoa wa Ruvuma. Picha/ Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa mkoa wa Ruvuma.

Mbolea ya ruzuku nikiwa imehifadhiwa katika moja ya maghala ya kuhifadhia mbolea yaliyopo mkoani mkoa wa Ruvuma. Picha/ Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa mkoa wa Ruvuma.

Msigwa ameongeza kuwa  kwa mwaka 2024/ 2025 Serikali imepanga kutoa tani 52,000 za mbegu bora ili kuwasaidia wakulima kufanikisha mavuno bora na ya kutosha.

Pia amewahimiza wakulima na mawakala wamehimizwa kufuata taratibu zote za usajili na matumizi ya mfumo wa kidigitali ili kunufaika na mpango huu muhimu kwa maendeleo ya kilimo nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks