Wafanyakazi kituo cha afya watumia mikono kufua mashuka ya wagonjwa
- Ni kituo cha afya Buzuruga wilayani Ilemela.
- Kituo hicho kina mashine ndogo isiyotosheleza mahitaji.
- Serikali yasema itatatua changamoto hiyo mapema.
Mwanza. Kituo cha afya Buzuruga wilayani Ilemela katika Mkoa wa Mwanza kimeiomba Serikali kuangalia namna ya kutatua changamoto ya mashine ya kufulia ambapo kwa sasa mashuka yanafuliwa kwa mkono.
Akizungumza baada ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala kutembelea ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika kituo hicho, Mganga Mfawidhi wa kituo Dk William Ntinginya ameiomba Serikali kuangalia suala hilo kwa kuwa mashine iliyopo kwa sasa ni ndogo na inatumika kufulia nguo za chumba cha upasuaji pekee.
“Kila mwezi wanawake zaidi ya 600 wanajifungua katika kituo hiki, idadi ambayo ni kubwa, mashuka yanayotumika yanafuliwa kwa mikono kitendo ambacho ni changamoto hasa kwenye kipindi cha mvua yanakua hayakauki hivyo tungeomba tupate mashine ambayp ingetusaidia kufua na kukausha,” amesema Dk Ntinginya.
Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilemela, Dk Rukia Edward amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kueleza kuwa tayari wameshaiwasilisha kwa wizara ya afya kwa ajili ya hatua zaidi.
Amesema kituo hicho kina mashine yenye uwezo wa kufua kilo 7 pekee hivyo kulingana na idadi ya wanawake wanaojifungua hapo haiwezi kutosheleza.
“Mahitaji ni makubwa ila mashine iliyopo uwezo wake ni mdogo haiwezi kufua nguo hizo, hivyo tayari tumeshaliwasilisha kwa wizara ili iweze kulifanyia kazi,” amesema Dk Edward.
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Masala amesema amepokea changamoto hiyo na kwamba atakutana na mkurugenzi wa halmashauri waweze kulizungumzia suala hilo.
Amemtaka Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo kuhakikisha wanasimamia kwa karibu suala la utoaji wa huduma za afya kwa kuwa kuna malalamiko yanayoripotiwa ambayo yanatakiwa kuangaliwa kwa karibu.
“Tunapokea wagonjwa wengi hivyo malalamiko yatakuwa mengi, kuna mambo yanaendelea hapa ambayo ni kinyume na utumishi wa umma, tunatakiwa usimamizi wa karibu kwenye suala la huduma, ili wahakikishe wanatoa huduma bora ya afya kwa wananchi,” amesema Masala.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema uwekezaji unaofanywa kwenye taasisi ya afya uendane sambamba na utoaji bora huduma za afya hivyo haipaswi kuwepo malalamiko ni lazima watumishi wajifunze namna ya kuwapokea na kuwahudumia wagonjwa.
Amemtaka mganga mfawidhi huyo kuhakikisha anatatua changamoto hizo na kueleza kuwa atarudi kwenye kituo hicho kwenda kuzungumza na watumishi.
Latest