Wafanyabiasha mtandaoni kuanza kutozwa kodi

December 17, 2018 1:40 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Mkurugenzi mkuu wa Clouds Media Group, Joseph Kusaga alipompokea na kumkaribisha  Kamishna Mkuu wa TRA Charles Kichere katika studio za Clouds FM mapema asubuhi ya leo. Picha| Clouds Digital.


  • Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yawataka wajitokeze ili waandikishwe na kuanza kulipa kodi kama watu wengine.
  • Hivi karibuni Rais John Magufuli aliweka wazi mapungufu yanayojitokeza katika mifumo na taratibu za ukusanyaji kodi ikiwemo wigo mdogo wa kulipa kodi usioendana na idadi ya Watanzania.
  • TRA imeahidi kutoa elimu na kujenga urafiki na walipa kodi ili kutatua changamoto za kufunga biashara za watu ambao wameshindwa kulipa kodi.

Dar es Salaam. Katika kuhakikisha inaongeza wigo wa walipa kodi, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kichere amewataka watu wanaofanya biashara mtandaoni wajitokeze ili waandikishwe na kuanza kulipa kodi kama watu wengine. 

Hatua hiyo ya TRA inakuja siku chache baada ya Rais John Magufuli kuagiza mamlaka hiyo iangalie namna ya kuwafikia watu wengi ili kuondoa mapungufu yanayojitokeza katika mifumo na taratibu za ukusanyaji kodi ikiwemo wigo mdogo wa kulipa kodi usioendana na idadi ya Watanzania.

“Taxi base yetu ya makusanyo ni ndogo mno, ikiwa Msumbiji wako milioni 27, walipa kodi ni milioni 5.3. Sisi tuko milioni 55, walipa kodi ni milioni 2.2 lazima tufike mahali tujiulize, kwa hiyo utaona kwamba kuna mahali tumeshindwa,” alihoji Rais Magufuli katika kikao kazi cha TRA na wakuu na makatibu wa mikoa kinachofanyika Jijini Dar es Salaam Desemba 10, 2018.

Kichere aliyekuwa akihojiwa na kituo cha redio cha Clouds FM leo asubuhi (Desemba 17, 2018) kuhusu mbinu watakazotumia kuongeza idadi ya walipa kodi amesema watu wote wanaofanya biashara mtandaoni ni lazima wajiandikishe ili wapewe namba ya mlipa kodi (TIN) kama wamekidhi vigezo.

“TRA tumeanza kuwafuata wanaofanya biashara mitandaoni ili walipe kodi, hivyo niwatake wajitokeze waje wajiandikishe,” amesema Kichere.

Biashara ya mtandaoni huusisha uuzaji na ununuzi wa bidhaa kwa njia ya mtandao ambapo watu hawalazimiki kwenda dukani au sokoni lakini kwa kutumia simu au kompyuta huduma hiyo inamfikia popote alipo. 

Vichocheo vikubwa vya mfumo wa biashara ya mtandaoni ni maendeleo ya teknolojia hususani ueneaji wa mtandao wa intaneti katika maeneo mbalimbali na uwepo wa makampuni ya simu za mkononi.

Maelekezo hayo yanaenda sambamba na kuandikisha wafanyabiashara wakiwemo ambao biashara zao zinazidi mtaji wa Sh4 milioni ili waanze kulipa kodi kama watu wengine.


Zinahusiana: 


Katika hatua nyingine, Kichere amekitumia kipindi hicho kujibu baadhi ya hoja zilizoibuliwa na Rais Magufuli kuhusu TRA kushindwa kutumia vyanzo mbalimbali kukusanya kodi, muamko mdogo wa walipa kodi na baadhi ya biashara kufungwa kwasababu wahusika wameshindwa kulipa malimbikizo ya kodi.

Akizungumzia suala la kufunga biashara, Kichere amesema tayari ametoa maagizo kwa watendaji wa TRA nchi nzima kutofunga biashara za watu wenye changamoto za kodi badala yake wakae nao na kuangalia namna ya kuzitatua.

“Mfanyabiashara mwenye matatizo ya kodi namwambia asifunge biashara yake, aje ofisini kwangu tuongee ili tujue namna gani atalipa kodi huku biashara yake ikiendelea nimeshazungumza na mameneja wa mikoa nimewaambia wafanyabiashara wasifunge biashara zao,” amesema Kichere. 

Amesema wataendelea kutoa elimu kwa wananchi ili waelewe umuhimu wa kulipa kodi na hatakubali kuona walipa kodi wanafokewa hata kama wana makosa ambayo yanaweza kutatuliwa kwa njia ya majadiliano.

 “Tunasisitiza watu walipe kodi kwa furaha, kuna mashine za EFD mfanyabiashara akitumia hizi mashine vizuri utalipa kodi vizuri atalipa kodi kulingana na mauzo yake,” amesema Kichere.

Katika siku za hivi karibuni, viongozi waandamizi wa Serikali wamekuwa wakitoa matamko kuwataka watendaji wa TRA kutengeneza mazingira mazuri ya kuwawezesha wafanyabiashara kulipa kodi na kuacha kuwatoza kodi kubwa isiyoendana na uwekezaji wa biashara zao.

Enable Notifications OK No thanks