Sh700,000 yamweka matatani mfanyakazi wa TRA Dodoma

Daniel Samson 0907Hrs   Disemba 03, 2018 Biashara
  • Anatuhumiwa kumtisha na kumbughudhi mfanyabiashara mmoja Jijini Dodoma akimtaka ampatie pesa hiyo ili kulipia mashine ya EFD, la sivyo angefungiwa biashara yake.
  • Hali hiyo imetokea leo baada ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji kufanya ziara ya kushtukiza kwenye mitaa ya Jiji la Dodoma.

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Dodoma kumsimamisha kazi mara moja mfanyakazi wake, Daniel Kingu kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili za kumbughudhi mfanyabiashara mmoja Jijini humo ikiwemo kutishia kufunga biashara yake.

Maagizo ya Dk Kijaji yanakuja siku moja baada ya Rais John Magufuli kuwatuhumu baadhi ya wafanyakazi wa TRA kuwa hawakusanyi kodi badala yake wanajenga uadui na walipa kodi kwa kuwatengenezea mazingira ya rushwa. 

"Kuna muda mwingine chanzo cha Serikali kupoteza mapato ni TRA wenyewe kwa kuweka viwango vikubwa vya kodi ili kutengeneza mianya ya rushwa na wanatumia vibaya kauli ya 'Hapa Kazi Tu'. Serikali inataka mapato lakini sio yasiyo ya halali," alisema Rais Magufuli akiwa wilayani Arumeru mkoa wa Arusha.

Katika ziara ya kushtukiza kwenye mitaa ya Jiji la Dodoma, Dk Kijaji amepata malalamiko kutoka kwa mfanyabiashara mmoja kwamba amekuwa akipokea simu za vitisho kutoka kwa mfanyakazi huyo akishirikiana na watu wengine akimtaka ampelekee Sh700,000 za kulipia mashine ya kutolea stakabadhi za kielektroniki (EFD Machine) la sivyo angefungiwa biashara yake.

"Mteja wetu awe salama na nitaendelea kufuatilia lakini kuanzia muda huu Kingu aondoke ofisini, hatuwezi kuwavumilia watu wa jinsi hii hata kidogo kwa sababu kazi ya kuuza mashine za EFD  si yake. Anamwambia mteja aende ofisini kwake chumba namba fulani, anafanya haya mambo ndani ya ofisi ya Serikali, akitoka nje inakuwaje?" amehoji Dk Kijaji kupitia taarifa iliyotolewa na wizara hiyo.


Zinazohusiana: Dk Mpango atoa onyo kali watumishi TRA


Dk Kijaji amesema hatasita kuchukua hatua hizo kwa wafanyakazi wengine wa TRA popote walipo nchini wanaojihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili.

Watendaji wa TRA nchini kote wametakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya kazi, kukadiria kodi kwa haki,  watumie lugha nzuri kwa wateja wao na kutoa elimu kwa umma kuhusu haki na wajibu wa wafanyabiashara katika masuala ya kodi badala ya kuwakadiria kodi kubwa isiyolipika.

"Ni lazima tuwalee wafanyabiashara hawa wadogo na ndio watakaotulipa kodi kubwa huko mbeleni badala ya kuwaumiza tangu wanapoanza biashara zao na ni lazima tuangalie viwango vyetu vya kodi tunavyotoza," amesisitiza Dk Kijaji.

Meneja wa TRA mkoa wa Dodoma, Thomas Masese ameahidi kutekeleza maagizo hayo na kufanya uchunguzi wa kina kuhusu suala hilo ambapo amerejea wito kwa watumishi wa mamlaka hiyo mkoani humo, kufanya kazi zao bila kuwanyanyasa wafanyabiashara pamoja na kutohusisha na vitendo visivyofaa ikiwemo kuomba rushwa.

Siku za hivi karibuni, viongozi waandamizi wa Serikali wamekuwa wakiwaonya mara kwa mara watumishi wa TRA kutotumia vibaya mamlaka yao kutoza kodi kubwa wafanyabiashara na kuwabambikizia viwango vikubwa vya tozo.

Related Post