Wafahamu Watanzania 6 waliong’ara mwaka 2024

January 1, 2025 9:00 am · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni Ramadhani Brothers, Dk Faustine Ndugulile, Aidan Msigwa na Dk Zarau Wendeline Kibwe. 
  • Yupo pia Sativa na Dk Gladness Salema.

Dar es Salaam. Mwaka huu wa 2024 zimeandikwa historia mpya kwa baadhi ya Watanzania waliofanya mambo makubwa, ndani na nje ya nchi.

Historia hizo zimeandikwa katika nyanja mbalimbali ikiwemo sanaa, siasa za kikanda, uongozi, muziki na shughuli za kibiashara.

Katika makala hii tumekuletea orodha ya baadhi ya watu waliovuka mipaka ya kawaida na kung’aa kwa mafanikio yaliyovutia wengi. Huenda simulizi zao zikakupa nguvu ya kuanza mwaka 2025 kwa kishindo katika kuzifikia ndoto zako. Twende pamoja!

  1. Ramadhani brothers

Hili ni kundi la wasanii wa michezo ya sarakasi linaloundwa na Fadhili Ramadhani na Ibrahim Jobu lililojipatia umaarufu kutokana na ustadi wao wa hali ya juu katika maonyesho ya sarakasi yanayojumuisha mazoezi ya viungo, usawa wa mwili sambamba na mbinu za kuvutia za maonyesho.

Kupitia kundi hili Tanzania imeandika historia ya kupata ushindi waliotwaa kwenye shindano la ‘America’s Got Talent’ na kujinyakulia kitita cha Dola za Marekani 250,000 sawa na Sh637.5 milioni baada ya kuwavutia majaji.

Hii imekuwa ni mara ya kwanza kwa Watanzania kushinda mashindano ya aina hii, hatua inayozidi kuitangaza nchi kimataifa. Baada ya ushindi wao, ndugu hao walieleza mpango wa kutumia zawadi yao kuwekeza katika ununuzi wa vifaa vya mazoezi ili kujiweka fiti zaidi.

Kundi hili limeonesha kuwa Tanzania ni taifa lenye vipaji vya kipekee huku ushindi wao ukitoa ujumbe wa matumaini kwa wasanii wengine nchini kuwa na ndoto kubwa ya kuipaisha sanaa ya Kitanzania kufikia viwango vya kimataifa.

Ramadhani Brothers wakionesha umahiri wao wa kipekee katika sarakasi kwenye jukwaa la ‘America’s Got Talent,’ wakivutia maelfu ya watazamaji duniani kwa ustadi wao. Picha |NBC Insider

Kabla ya ushindi huu, mwaka 2022 walifika fainali ya msimu wa 10 wa Australia’s Got Talent kwa kupata ‘Golden Buzzer’, yaani kitufe maalum ambacho jaji hukibonyeza ili mshiriki apite moja kwa moja hadi hatua za juu kutoka kwa jaji Kate Richie.

Pia mwaka 2022, walifika fainali ya msimu wa 17 wa France’s Got Talent. 2023, wakafika nusu fainali ya msimu wa 13 wa Romania’s Got Talent na kushiriki kwenye mashindano ya Got Talent All-Stars nchini Hispania ambapo pia walifika Fainali.

  1. Hayati Dk Faustine Ndugulile

Wananchi wa Kigamboni walimfahamu kwa muda mrefu kama mwakilishi wao bungeni, lakini umaarufu wake uliibuka zaidi mwaka huu baada ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika.

Kuteuliwa kwake Agosti 28, 2024, jijini Brazzaville, Congo, kuliipa Tanzania sifa kubwa kimataifa na kuwa Mwafrika wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kushika nafasi hiyo ya heshima, akiwashinda wagombea wenye uzoefu kutoka Rwanda, Niger, na Senegal.

Dk. Ndugulile (55) alikuwa daktari bingwa mwenye shahada ya udaktari wa madawa na uzamili katika mikrobiolojia na chanjo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Alihudumu katika nyadhifa muhimu serikalini, ikiwemo Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (2020-2021) na Naibu Waziri wa Afya (2017-2020). 

Utaalamu wake pia unaonekana katika uandishi wa machapisho 10 yanayohusu magonjwa ya kuambukiza, usugu wa dawa, na sera za afya. Kati ya kazi zake zilizotamba ni utafiti wa mwaka 2022 kuhusu kampeni ya kitaifa ya Furaha Yangu, iliyolenga kuhamasisha wanaume nchini Tanzania kutumia huduma za upimaji na matibabu ya VVU.

Rais Samia Suluhu Hassan aliongoza kampeni ya kumsaidia kupata nafasi hiyo na kumsifu baada ya ushindi wake, akimuelezea kama kiongozi aliyewakilisha nchi kwa heshima na ambaye Afrika ingefaidika kwa ujuzi wake.

Hata hivyo, mshumaa wa Dk. Ndugulile ulizimika ghafla mnamo Novemba 27, 2024, alipofariki dunia nchini India akiwa katika matibabu, miezi mitatu tu baada ya kuchaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa WHO. Kifo chake kilileta simanzi kubwa, si tu kwa Tanzania, bali kwa bara zima la Afrika, ambako alionekana kama nyota angavu aliyejitolea kuboresha afya ya jamii.

  1. Aidan Msigwa 

Hivi sasa ameandikwa kwenye orodha ya mabilionea baada ya kupiga dili moja la kulala maskini na kuamka tajiri, wakati ni mtafiti na mchimbaji mdogo wa dhabahu.

Msigwa ni mchimbaji mdogo wa dhahabu kutoka Chunya, mkoa wa Mbeya, aliyekuwa akimiliki leseni za uchimbaji na utafutaji madini katika maeneo mbalimbali wilayani humo, pamoja na mtambo wa uchenjuaji wa madini.

Ameweka alama mnamo Septemba 17, 2024 baada ya kusajili na kuuza kilo 111.82 za madini ya dhahabu, zenye thamani ya Sh20.11 bilioni, kwenye Soko la Madini la Chunya mkoani Mbeya.

Kwa mujibu wa tovuti ya Wizara ya Madini, mauzo ya dhahabu hiyo yameipatia Serikali mrabaha wa Sh1.2 bilioni, ada ya ukaguzi ya Sh201 milioni na kama malipo ya ushuru wa huduma kwa Halmashauri ya Sh60.34 milioni, wakati Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imepokea Sh402.31 milioni kama kodi ya zuio.

Dhahabu yenye jumla ya kilo 111.82 na thamani ya Sh20.11 bilioni iliyouzwa na Aidan Msigwa katika Soko la Madini la Chunya, Mbeya. Picha |Wizara ya Madini

Wakati akipiga bumu hilo Msigwa alikuwa mmiliki wa leseni ya uchimbaji mdogo (PML) na utafutaji madini (PL) katika maeneo mbalimbali ndani ya wilaya hiyo, akimiliki pia mtambo wa uchenjuaji wa dhahabu.

Afisa madini mkazi mkoa wa kimadini Chunya, Inj Laurent Mayalla akampa maua yake na kusema anapaswa kuigwa kwa uzalendo aliouonesha kuuzia kiasi hicho cha dhahabu sokoni badala la kuitorosha.

  1. Dk Zarau Wendeline Kibwe

Huyu ni mtaalamu mbombezi wa uchumi aliyeziba pengo la miaka 54 tangu Mtanzania Christopher Kahag (1968 hadi 1970), kuhudumu kwenye nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia akichaguliwa kisimamia Kanda Namba Moja ya Afrika inayojumuisha nchi 22.

Dk Kibwe ameanza kutumika kama kiongozi mpya kwenye ofisi hiyo Oktoba 25, 2024 wakati wa mkutano wa mwaka wa kundi la kwanza la nchi za Afrika wa Benki ya Dunia, Washington, Marekani.

Kabla ya kuchaguliwa kwake, mbobezi huyu mahili katika masuala ya uchumi na fedha amehudumu kwa zaidi ya miaka saba katika bodi ya Benki ya Dunia kama Naibu Mkurugenzi Mtendaji, Mshauri na Mshauri Mwandamizi. 

Safari yake ya taaluma ilianzia nyumbani kwa kuhitimu shahada ya kwanza ya sayansi katika uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe mkoani Morogoro.

Baada ya hapo alikwenda Taasisi ya Taifa ya Mafunzo ya Sera (GRIPS) iliyopo Tokyo, Japan na kuhitimu shahada ya uzamili katika uchumi wa maendeleo na umahiri katika sera za umma, pamoja na shahada ya uzamivu katika uchumi wa maendeleo.

Ikiwemo Tanzania, Dk Kibwe anahudumia nchi za Botswana, Burundi, Eritrea, Eswatini, Ethiopia, Gambia, Kenya, Lesotho, Liberia, Malawi, Msumbiji, Namibia, Rwanda, Shelisheli, Sierra Leone, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Uganda, Zambia, na Zimbabwe.

  1. Dk Gladness Salema

Amekuwa kielelezo cha nafasi ya juu ya wanawake katika uongozi na diplomasia ya kikanda baada ya kushinda nafasi ya ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kwa kishindo. 

Dk. Salema, aliyekuwa Mhadhiri Mwandamizi wa Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSB) amejishindia nafasi hiyo Septemba 5 kwa kupata kura 254 za ndiyo kati ya kura 274 katika uchaguzi uliofanyika Bungeni, Dodoma. 

Alipata shahada ya kwanza ya sayansi katika teknolojia ya chakula kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na kusomea shahada mbili za uzamili kwenye uongozi wa biashara (MBA) na afya ya umma (MPH), na kisha shahada ya uzamivu (PhD) katika masuala ya usafirishaji kutoka Chuo Kikuu cha Molde, Norway.

Atahudumu katika nafasi hiyo hadi 2027 akiziba nafasi ya Dk Shogo Mlozi aliyefariki dunia Juni 13.

Anaiwakilisha nchi katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) linaloundwa na Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Somalia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

  1. Edgar Mwakabela (Sativa)

Watumiaji wengi wa jukwaa la X hasa wanaopenda kubeti wamemfahamu kabla ya hadhira kubwa zaidi kumfahamu baada ya tukio lililohusisha utekeji wake.

Umaarufu wake ulianza Juni 23, 2024 baada ya picha zake kusambaa mtandaoni akiripotiwa kuwa ametekwa na watu wasiojulikana. 

Baada ya siku nne za kusakwa, alipatikana mkoani Katavi akiwa na majeraha kwenye maeneo mbalimbali ya mwili huku Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Kaster Ngonyani, akithibitisha kuwa alipatikana ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi asubuhi ya Juni 27, 2024.

Edgar Mwakabela (28), maarufu kama ‘Sativa,’ akifanya mahojiano baada ya kufanyiwa upasuaji wa taya katika Hospitali ya Wilaya ya Mpimbwe, Katavi . Picha |Mwananchi

Wakati wa matibabu yake Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alimchangia kiasi cha Sh35 milioni sambamba na michango kutoka kwa makundi mbalimbali yakajitokeza.

Jina lake limezidi kusikika masikioni mwa watu baada ya Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu aliyechukua fomu ya kugombea uenyekiti wa chama hicho kuweka wazi kuwa amelipiwa Sh1.5 milioni na Sativa kama gharama za kuchukua fomu hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks