Necta yawafutia matokeo wanafunzi 151 wa darasa la nne, kidato cha pili 2024
- Ni baada ya kufanya udanganyifu na kuandika matusi.
- Yatangaza vita na watakaohujumu matokeo hayo.
Arusha. Wakati mamia ya wanafunzi wa darasa la nne na kidato cha pili nchini wakifurahia matokeo yao, hali ni tofauti kwa wanafunzi 151 waliofutiwa matokeo yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo udanganyifu.
Dk Said Mohamed, Katibu Mkuu wa Necta aliyekuwa akitangaza matokeo hayo leo Januari 4, 2025 jijini Dar es Salaam amesema wanafunzi 100 waliofanya Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne (SFNA) wamefutiwa matokeo yao kwa udanganyifu na watano kwa kuandika matusi.
“Kati ya wanafunzi 100 wawili walifanya udanganyifu kwa kusaidiana ndani ya chumba cha mtihani, wanafunzi 98 ni watoro wa muda mrefu shuleni hivyo walimu wakuu waliwapanga wanafunzi wenzaio wa darasa la tatu, darasa la tano na darasa la sita kuwafanyia mtihani kwa manufaa yao binafsi,” amesema Dk Mohamed.
Aidha, Necta imebainisha kuwa imefuta matokeo yote ya wanafunzi 46 waliofanya mtihani wa Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili (FTNA), kati ya hao 41 ni wale waliofanya udanganyifu huku watano wakiandika matusi katika karatasi za kujibia.
Matokeo hayo yamefutwa kwa mujibu wa kifungu cha 5 (2) (i) cha Sheria ya Necta sura ya 107 kikisomwa pamoja na kifungu ch 30(2) (b) cha Kanuni za Mitihani mwaka 2016 ambazo zinakataza vitendo vyovyote vya udanganyifu wakati wa mitihani.
Idadi hiyo ya waliofutiwa matokeo katika mitihani ya SFNA na FTNA kwa mwaka huu imepungua kulinganisha na ile iliyoripotiwa katika matokeo ya mwaka 2024.
Januari 7, mwaka 2024 Necta ilitangaza kufuta matokeo ya wanafunzi 223 kwa udanganyifu na kuandika matusi ambapo 178 walifanya udanganyifu na watatu walioandika matusi katika karatasi za kujibia katika mitihani ya darasa la nne.
Wanafunzi wengine 28 waliofanya upimaji wa kitaifa wa kidato cha pili walifutiwa matokeo kwa udanganyifu huku 14 wakiyakosa matokeo yao kwa mwaka huo kwa sababu ya kuandika matusi katika karatasi za kujibia.
Kwa mujibu wa Necta kupungua kwa wanafunzi wanaofutiwa matokeo kunatokana na jitihada mbalimbali zinazofanywa na baraza hilo ikiwemo kutoa elimu kwa wasimamizi, wanafunzi na walimu.
Hata hivyo Necta imesema haitasita kuwachukulia hatua wote watakaohujumu matokeo hayo.
“Takwimu za udanganyifu zimepungua kwa miaka ya karibuni, wakati huu ambapo nchi ipo katika mabadiliko na maboresho makubwa katika sekta ya elimu hatuwezi kuvumilia watu wanaopanga kuhujumu elimu yetu, hatua kali zitachukuliwa kwa wote watakaoajaribu kuhujumu mitihani ya Taifa,”amesema Dk Mohamed.
Katika hatua nyingine Necta imeifungia Shule ya sekondari ya Good will iliyopo Arusha kwa makosa ya kujaribu kuwarubuni wasimamizi, askari polisi na kutengeneza mazingira ya kuwapa majibu ya mtihani wanafunzi.
Necta imesema kituo kitafungiwa kwa muda wote na inaangalia uwezekano wa kuifutia leseni huku waliohusika wakichukuliwa hatua.