Usiyofahamu kuhusu Bitcoin, faida,hasara zake

January 3, 2025 4:52 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni ni mfumo wa malipo ya moja kwa moja kati ya muuzaji na mnunuaji.
  • Tanzania bado inafanya tafitiya matumizi yake.

Dar es Salaam. Huenda umewahi kusikia kuhusu Bitcoin, sarafu ya kidijitali iliyojipatia umaarufu maeneo mbalimbali duniani kutokana na namna ilivyobadili mifumo ya malipo ya bidhaa au huduma pamoja na kuchochea umiliki wa mali kidijitali.

Matumizi ya sarafu hii katika nchi za dunia ya tatu ikiwemo Tanzania hayajapigiwa sana chapuo, huenda ni kutokana na kukosekana kwa uelewa wake pamoja na kutokuwepo kwa mahitaji ya lazima ya kutumia Bitcoin jambo linalopunguza kasi hata ya kuweka taratibu za kisheria za matumizi yake.

Makala hii inaangazia kwa undani historia ya sarafu ya Bitcoin na namna inavyoweza kutumika katika nyanja mbalimbali za uchumi.

Bitcoin ni nini ?

Bitcoin ni mfumo wa malipo ya moja kwa moja kati ya muuzaji na mnunuaji ambayo hayadhibitiwi na mamlaka yoyote kama benki kuu, mamlaka za mapato au taasisi yoyote ya Serikali.

Kwa mtazamo wa kimatumizi, Bitcoin ni sarafu ya kidijitali yenye thamani ya pesa taslimu inayotumika kuuza ama kununua bidhaa mtandaoni.

Mfumo huu wa malipo unatajwa kuwa uligunduliwa na Sakoshi Nakamoto (utambulisho bandia) mwaka 2009, kwa mujibu wa tovuti ya Bitcoin.

Sarafu ya kidijitali (cryptocurrency) ni aina ya fedha ambayo ni mbadala wa njia za kawaida za malipo iliyoundwa kwa kutumia teknolojia ya blockchain inayoufanya mfumo huo kuwa salama.

Bitcoin ni sarafu ya kidijitali yenye thamani ya pesa taslimu inayotumika kuuza ama kununua bidhaa mtandaoni. Picha | Getty Images

Ifahamu teknolojia ya Blockchain

Kwa mujibu wa kituo cha mafunzo cha Binance, Blockchain ni teknolojia ya uhifadhi wa data  inayowezesha sarafu za kidijitali kama Bitcoin, kufanya miamala bila kutegemea benki au taasisi za kifedha, na kuhakikisha usalama wa taarifa zote kwa watumiaji.

Teknolojia ya blockchain inatoa faida ya mfumo unaojulikana kama Decentralization System, yaani mfumo ambao hakuna taasisi yeyote ya fedha inayoongoza miamala, na hivyo kupunguza gharama na kuongeza kasi ya miamala.

Teknolojia ya blockchain haihusishi sarafu ya Bitcoin peke yake, kuna sarafu nyingine kama Ethereum na Tether ambazo  zinaweza tumika kununua, kutunza na kubadilishana na mali zingine.

Kupitia blockchain vijana wanaweza kushiriki katika sekta mbalimbali kama biashara za kidijitali, uwekezaji, na hata kuunda miradi yao ya ubunifu.

Jinsi unavyoweza kunufaika na Bitcoin

Kuna njia nyingi ambazo zinaweza kukufanya unufaike na Bitcoin lakini wao wenyewe wanashauri njia nzuri zaidi ya kunufaika na Bitcoin ni kwa kuwekeza. 

Kama vile unavyoweza kununua hisa katika soko la hisa, unaweza kununua Bitcoin kwa bei fulani na kuuza baadaye wakati bei inapopanda.

Faida ya nyingine ya kununua sarafu za kidijitali ni kuwa thamani yake hupanda au kuporomoka kutokana na uhitaji wakati fedha za kawaida hupungua thamani kutokana na kuongezeka kwa mfumuko wa bei.

Aidha, Bitcoin  husaidia watu kutunza thamani. Kwa mfano kama ulinunua  Bitcoin mwaka 2009, basi thamani yake ya Bitcoin ulizonunua zitakuwa zimepanda kwa zaidi ya  asilimia 20,000,000% kwa kuwa ndio bidhaa au mali inayopanda thamani kwa kasi zaidi duniani kwa mujibu wa google.

Kwa upande mwingine, wajasiriamali na wafanyabiashara wanaweza kutumia Bitcoin kama njia ya kupokea malipo kutoka kwa wateja. 

Hii inawawezesha kupata malipo kwa haraka, bila hitaji la benki au taasisi za fedha zinazoshughulikia miamala ya pesa.

Kwa biashara ambazo zinahudumia wateja kimataifa, Bitcoin inatoa faida ya kutuma na kupokea malipo bila kujali mipaka ya nchi au tofauti za sarafu, huku ikiwa na gharama ndogo za miamala ikilinganishwa na njia za jadi za malipo.

Kwa upande mwingine, wajasiriamali na wafanyabiashara wanaweza kutumia Bitcoin kama njia ya kupokea malipo kutoka kwa wateja.  Picha | Bitcoin.

https://bitcoin.org/en/faq#how-difficult-is-it-to-make-a-bitcoin-payment

Kama vile unavyoweza kufanya biashara na sarafu za kigeni, Bitcoin na sarafu zingine za kidijitali pia zinapatikana kwenye soko la biashara watumiaji wanaweza kununua sarafu kwa bei ya chini na kuuza kwa bei ya juu ili kufaidika na tofauti hiyo ya bei.

Biashara hii inahitaji ujuzi na ufahamu wa soko, kwa kuwa thamani ya sarafu za kidijitali inabadilika kwa kasi na mara nyingi hufuata mwelekeo wa soko kihisia. 

Kwa hiyo kufanya biashara ya Bitcoin inaweza kuwa njia nzuri ya kupata faida kwa wale wanaojua namna ya kusoma mabadiliko ya bei na kufanya maamuzi kwa haraka.

Kwa kuwa sarafu za kidijitali zinakuwa maarufu, fursa za kuanzisha biashara zinazohusiana na teknolojia hii pia zinapanuka. 

Biashara kama vile kubadilishana Bitcoin (exchanges), huduma za pochi za Bitcoin, na hata makampuni yanayotoa huduma za ushauri kuhusu sarafu za kidijitali zinaweza kuwa sehemu ya kuzalisha kipato.

Kwa wajasiriamali, kuanzisha biashara zinazohusiana na Bitcoin na sarafu za kidijitali kunaweza kuwa na faida kubwa kutokana na ongezeko la umaarufu wa teknolojia hii.

Tanzania na Bitcoin

Pamoja na faida nyingi za Bitcoin Tanzania bado haijachukua hatua madhubuti kuchochea matumizi yake ingawa Serikali imekuwa ikihamasisha matumizi ya pesa mtandao kuliko pesa ya mkononi.

Juni 13, 2021 akiwa jijini Mwanza Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliitaka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kujitayarisha kwa matumizi ya sarafu mtandaoni, akisema wakati wa sarafu mtandaoni umefika, hivyo, ni muhimu kuanza maandalizi kuruhusu mabadiliko hayo.

Rais Samia alisema BoT inapaswa kuanza maandalizi muhimu ya mabadiliko ya hatua katika mtazamo wa ulimwengu juu ya benki, ikichagua sarafu za mtandaoni kama mustakabali wa fedha.

“Tumeshuhudia kuibuka kwa safari mpya kupitia mtandao.Najua kuwa mataifa mbalimbali ikiwemo Tanzania hawajakubali au kuanza kutumia njia hizi.

 Lakini wito wangu kwa Benki Kuu ni kwamba mnatakiwa kuanza kufanyia kazi maendeleo hayo. Benki Kuu inapaswa kuwa tayari kwa mabadiliko na sio kukutwa hamjajiandaa,” alisema Rais Samia.

Hata hivyo,  tayari BOT imesema kwa kwa sasa inaendelea na hatua ya utafiti wa uanzishwaji wa matumizi ya sarafu za kidijitali za Benki Kuu (Central Bank Digital Currency).

Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande alipokuwa akijibu swali la aliyekuwa Mbunge wa Kigamboni, hayati Dk.Faustine Ndugulile, aliyeuliza Serikali ina mpango gani wa kuanza kwa matumizi ya Sarafu za Kidijitali (Central Bank Digital Currency) hapa nchini. 

Chande alisema kuwa Benki Kuu imebaini uanzishwaji wa sarafu za kidijitali za Benki Kuu (Central Bank Digital Currency), unahitaji kuanzishwa kwa uangalifu na umakini bila kuleta athari hasi katika mifumo ya malipo iliyopo nchini na pia kuweza kutatua tatizo halisi la malipo ambapo kwa sasa bado mifumo iliyopo nchini inakidhi hali halisi ya uwezeshaji mwananchi kutuma fedha na kufanya malipo. 

‘‘Soko letu bado linahitaji kuendelea kuboreshwa katika kuimarisha mifumo iliyopo kwa kutumia vyanzo vinavyopatikana kwa urahisi na wananchi wengi (simu za kawaida) tofauti na matumizi ya Sarafu za Kidijitali zinazoitaji matumizi ya simu janja (smartphones),’’ alisema Chande. 

Pamoja na faida nyingi za Bitcoin Tanzania bado haijachukua hatua madhubuti kuchochea matumizi yake. Picha | Wizara ya Fedha

Hatari unazoweza kukumbana nazo kupitia Bitcoin

Hata hivyo, ukiachilia mbali faida ambazo mtu anaweza kuzipata kupitia teknolojia hii na kuna baadhi ya changamoto ikiwemo kutoweza kufuatilia fedha zako pale zinapopotea ama kuibiwa kwasababu taarifa za miamala hazipitii kwenye taasisi yeyote ya fedha na hakuna bima rasmi katika uendeshaji wa huduma hiyo.

Aidha, changamoto nyingine inaweza kutokana na uelewa finyu kuhusiana na mfumo huo wa malipo hivyo ni vyema kabla ya kuamua kuitumia ni vyema kujielimisha kwanza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks