Necta yatangaza matokeo ya darasa la nne, kidato cha pili ufaulu ukiongezeka
- Ufaulu waongezeka kwa asilimia 2.9 kwa mitihani ya darasa la nne na asilimia 0.1 kwa kidato cha pili.
- Zaid ya nusu ya wanafunzi wa kujitegemea wa kidato cha pili wafaulu.
Arusha. Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili (FTNA) pamoja na matokeo ya Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne (SFNA) ambapo ufaulu umeongezeka kiduchu kwa ngazi zote mbili.
Dk Said Mohamed, Katibu Mkuu wa Necta aliyekuwa akitangaza matokeo hayo leo Januari 4, 2024 jijini Dar es Salaam amesema kuwa ufaulu wa jumla kwa matokeo ya darasa la nne umeongezeka kwa asilimia 2.9.
“Jumla ya wanafunzi 1,320,227 kati ya 1,530,805 wenye matokeo sawa na asilimia 86.24 wamefaulu kwa kupata madaraja ya A, B, C, D na hivyo wanapata fursa ya kuendelea na darasa la tano kwa mwaka huu 2025,” amesema Dk Mohamed.
Jumla ya watahiniwa milioni 1.6 walisajiliwa kufanya upimaji huo wa kitaifa uliofanyika Oktoba mwaka huu wakiwemo wasichana 839,515 sawa na asilimia 51 na wavulana 793,764 sawa na asilimia 49.
Kati yao watahiniwa milioni 1.5 ndiyo waliofanya mtihani huo huku wengine 123,068 sawa na asilimia 6 wakishindwa kufanya mitihani hiyo kutokana na sababu mbalimbali.
Wakati wastani wa ufaulu ukiongezeka kwa matokeo ya darasa la nne, hali inafanana na matokeo ya ufaulu wa kidato cha pili ambao umeongezeka kiduchu kwa asilimia 0.1.
Jumla ya wanafunzi 869,743 walisajiliwa kufanya mitihani huo Novemba mwaka huu kati yao wasichana wakiwa 470, 331 sawa na asilimia 54 na wavulana 399,412 sawa na asilimia 46.
“Wanafunzi 680,574 kati ya 796,825 wenye matokeo sawa na asilimia 85.41 wamefaulu na hivyo wamepata fursa ya kuendelea na masomo kwa kidato cha tatu,” amesema Dk Mohamed.
Kati yao wasichana 367,457 sawa na asilimia 54 na wavulana 313,117 sawa na silimia 46.
Kwa mujibu wa Dk Mohamed takwimu za ufaulu huo zinaashiria kuwa juhudi zaidi za ufundishaji na ujifunzaji zinatakiwa kuongezwa ili kuongezwa ili kuinua kiwango cha ubora wa ufaulu.
Aidha, Necta imetangaza matokeo ya kidato cha pili kwa wanafunzi wa kujitegemea ambapo zaidi ya nusu ya wanafunzi 7527 waliosajiliwa kufanya mtihani huo wamefaulu.
“Watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu na kupata sifa ya kufanya mtihani wa kidato cha nne ni 4,205 ambao ni asilimia 56 ya wale waliofanya upimaji huu.” amesema Dk Mohamed.
Kwa matokeo hayo watahiniwa hao wanapata nafasi ya kufanya mitihani ya kidato cha nne kwa mara ya kwanza tangu Serikali ifute mitihani ya QT.