Wafahamu wakuu wa wilaya walioondolewa kwenye mkeka mpya
- Yupo Jery Muro, Mhandisi Richard Henry Ruyango pamoja na Josephat Paul Maganga aliyekuwa Mpwapwa.
- Kuondolewa kwao kumetoa nafasi ya kuongezeka kwa wakuu wa wilaya wanawake.
Dar es Salaam. Huenda siku ya leo ikaisha kwa huzuni na machungu kwa wakuu wa wilaya waliotenguliwa nyadhifa zao akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro mara baada ya Rais wa Tanzania kuteua wakuu wa wilaya wapya 37.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu Zuhura Yunus leo Januari 25, 2023 imeeleza kuwa pamoja na kuteua wakuu wa wilaya wapya, Rais Samia amewahamisha vituo wakuu wa wilaya 48 na kuwabakisha 55 kwenye vituo vyao.
Mabadiliko kama haya Rais Samia aliyafanya kwa mara ya kwanza Juni 19, 2021 ambapo aliteua wakuu wa wilaya wapya, kuwabadilishia baadhi vituo na wengine kuwabakisha kwenye vituo vyao.
Miongoni waliondolewa ni pamoja na Sophia Mjema aliyeteuliwa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) huku wengine mustakabali wao ukiwa haujawekwa wazi.
Ifuatayo ni orodha ya wakuu wa wilaya ambao nafasi zao zimechukuliwa na wakuu wa wilaya wapya walioteuliwa na wao kuondolewa kwenye wadhifa huo.
Wa kwanza ni Nurdin Hassan Babu ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Longido ambaye nafasi yake imechukuliwa na Marko Henry Ng’umbi, John Ernest Pallingo aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Sikonge ameondolewa katika wadhifa huo na nafasi yake imechukuliwa na Simon Kemori Chacha.
Zinazohusiana
- Panga pangua ya Rais Samia kwa wakuu wa wilaya hii hapa
- Rais Samia atengua uteuzi Mkuu wa Wilaya Mbarali, wakurugenzi wanne
Mhandisi Richard Henry Ruyango aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru amempisha Emanuel Kaganda Mtatifikolo, Wilson Samwel Shimo aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Geita naye amempisha Kanali Boniphace Magembe.
Wengine waliowekwa pembeni ni Charles Francis Kabeho, Martha John Mkupasi kutoka Chato, Jamuhuri David William aliyekuwa Nyang’wale, Toba Alnason Nguvila aliyekuwa Muleba pamoja na Rashid Mwaimu Mohamed aliyekuwa Kyerwa.
Wengine ni Josephat Paul Maganga aliyekuwa Mpwapwa, Juliet Banyula Nkebanyi aliyekuwa Karagwe pamoja na Dunstan Dominick Kyobya aliyekuwa mkoani Mtwara.
Hivi sasa Sara Ally Msafiri anampisha Nickson Simon John kwenye kiti cha ukuu wa wilaya Kibaha, huku Jasinta Venant Mboneko akiachia kiti hicho wilayani Shinyanga na Ghaibu Buller Lingo akiondolewa kwenye ukuu wa wilaya ya Pangani.
Wengine ambao hawapo kwenye orodha hiyo ni pamoja na Zainab Rashid Mfaume Kawawa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Sezaria Veneranda Makota (Mbulu), Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi Ismail Twahir Mlawa aliyekuwa Kyela.
Suleman Mwenda aliyekuwa Iramba na Kemirembe Lwota aliyekuwa wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera nao wameondolewa katika nyadhifa zao.
Wengine walioondolewa katika mkeka mpya ni Dk Yahya Ismail Nawanda aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Dk Charles Mhina (Bariadi), Gabriel Zakaria Olemegili (Busega), Festo Kiswaga (Kahama) na Polotet Kamando Mgema aliyekuwa Songea.
Sophia Mjema, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM ambaye awali alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha. Pichal Haki Ngowi
Naye Mathayo Francis Masele wa Malinyi hivi sasa kampisha Sebastian Waryuba aliyekuwa na Tano Seif Mwera amemwachia kiti cha ukuu wa wilaya ya Kalambo Lazaro Killian Komba.
Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Martin Stephen Ntemo sasa atampisha Zephania Stephen Sumaye huku P 8189 Col. Ahmed wa Kibiti akimwachia kijiti Kanali Joseph Samwel Kolombo.
Uteuzi wa Andrea Awesso Tsere aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Ludewa ulitenguliwa siku moja kabla ya orodha mpya ya wakuu wa wilaya huku Reuben Ndiza Mfune aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbarali amemwachia wadhifa huo Kanali Denis Filangali Mwila.
Cosmas Isuna Nshenye aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, P 8819 Col. L. E Thomas (Nyasa) na Siriel Mchembe aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni nao ni miongoni mwa walioondolewa katika nyadhifa zao.
Katika orodha mpya ya wakuu wa wilaya walioteuliwa kuna ongezeko kiasi la wakuu wa wilaya wanawake ambapo mpaka sasa Tanzania itakuwa na jumla ya wakuu wa wilaya wanawake 40 kati ya 140.
Latest
