Wabunge CCM walioshindwa kutetea majimbo yao kura za maoni 2025
- Wengi wao wamehudumu zaidi ya muhula mmoja bungeni
Dar es Salaam. Mchakato wa kura za maoni katika nafasi za udiwani na ubunge ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) umehitimishwa rasmi jana Agosti 4, ambapo katika kila jimbo, jina moja limependekezwa na wajumbe ili kupeperusha bendera ya chama hicho.
Hata hivyo, Nukta Habari imebaini kuwa baadhi ya wabunge waliokuwa wakitetea nafasi zao bungeni wameondolewa katika hatua ya kura za maoni licha ya kupita kwenye uteuzi wa awali.
Hii inamaanisha iwapo Kamati Kuu ya CCM haitafanya mabadiliko kabla ya majina kupelekwa rasmi kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) wabunge hao wanaomaliza muda wao, utumishi wao kwenye majimbo utakoma rasmi.
Hawa hapa ni baadhi ya wabunge wa sasa waliotemwa na wajumbe wa CCM kwenye kura za maoni.
Hamis Kigwangalla 2010 – 2025
Mmoja wa wabunge hao ni Dk. Hamis Kigwangalla ambaye amekuwa Mbunge wa Nzega Vijijini tangu mwaka 2010.
Dk. Kigwangalla amewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, ikiwemo Naibu Waziri wa Afya na Waziri wa Maliasili na Utalii, kwa sasa ameshindwa kufua dafu kwa Neto Kapalata ambaye ameshinda kura za maoni.
Deo Sanga 2010 – 2025
Mwingine ni Deo Sanga, ambaye kwa mara ya kwanza alichaguliwa kuwa mbunge mwaka 2010.
Sanga amehudumu kama mbunge kwa zaidi ya miaka 15 katika Jimbo la Makambako. Katika kura za mwaka huu, Daniel Chongolo, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, ameibuka mshindi.
Charles Kimei 2020 -2025
Katika hatua nyingine, Dk. Charles Kimei, ameshindwa kufua dafu kwenye kura za maoni.
Kimei ambaye ni mtaalamu wa masuala ya fedha na uchumi, alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mbunge wa Vunjo mwaka 2020. Hata hivyo, ameangushwa na Enock Koola katika kura za maoni mwaka 2025.
Vunjo inaendelea kuweka rekodi ya kuwa jimbo linaloweka sura mpya kila baada ya muhula wa uchaguzi ambapo hakuna mbunge aliyefanikiwa kuongoza kwa vipindi viwili mfululizo.
Jesca Msambatavangu 2020 – 2025
Aidha, Jesca Msambatavangu ambaye amekuwa Mbunge wa Iringa Mjini tangu mwaka 2020 akimbwaga Peter Msigwa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema naye ameangukia pua katika kura za maoni.
Fadhili Ngajiro ndiye aliyepata kura nyingi zaidi za wajumbe kuliwakilisha jimbo hilo kupitia CCM kwenye uchaguzi wa 2025 ambapo kama kamati kuu ikiridhia safari yake ya ubunge itakuwa imeishia hapo.
Stela Manyaya 2010 – 2025
Stela Manyaya ambaye kwa mara ya kwanza aliingia bungeni mwaka 2005 kama Mbunge wa Viti Maalum huku akiwahi kushika nyadhifa kadhaa serikalini ikiwemo Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia mwaka 2015.
Manyanya ameangushwa na John Nchimbi kuwania nafasi ya ubunge jimbo la Nyasa katika kura za maoni.
Kundo Mathew 2020 – 2025
Kwa upande wa jimbo la Bariadi vijijini Kundo Mathew ambaye amekuwa Mbunge tangu 2020 na kuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, mwaka huu, ameondolewa na wajumbe waliompa ushindi Masanja Kadogosa, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC).
Issa Mtemvu 2020 – 2025
Issa Mtemvu, ambaye ni mtoto wa aliyewahi kuwa mbunge Temeke, Abbas Mtemvu alishinda kwa mara ya kwanza mwaka 2020 jimbo la Kibamba.
Mwaka huu, Angela Kairuki, aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Tamisemi, amepitishwa na wajumbe.
John Kanyasu 2015 – 2025
Aidha, John Kanyasu aliyechaguliwa kuwa Mbunge mwaka 2015 na kuhudumu katika nafasi ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii. Ameshindwa kufua dafu kwa Chacha Wambura kwenye kura za maoni jimbo la Geita Mjini.
Innocent Bilakwate 2015 – 2025
Katika hatua nyingine, Innocent Bilakwate ambaye amekuwa Mbunge wa Kyerwa tangu mwaka 2015, mwaka huu wa 2025 ameshindwa kufua dafu kwa Khalid Nsekela ambaye ameshinda kura za maoni za CCM jimboni humo.
Hassan Mtenga 2020 – 2025
Katika orodha hii Hassan Mtenga hajabaki nyuma, Mtenga ambaye aliingia bungeni mwaka 2020 katika mbio za ubunge jimbo la Mtwara Mjini kwa mwaka 2025 Mtenga amezidiwa kete na Joel Nanauka ambaye ameshinda katika kura za maoni.
Baada ya kura za maoni zilizopigwa na wajumbe, majina ya waliopitishwa yatawasilishwa kwa Kamati Kuu ya CCM kwa maamuzi ya mwisho kabla ya kupelekwa kwa Tume ya Uchaguzi.
Hivyo kama kamati Kuu haitafanya mabadiliko yeyote kwenye majina hayo basi waliochaguliwa wataipeperusha bendera ya CCM katika majimbo yao katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Latest
