Vodacom, Mastercard zaangazia biashara ya mtandaoni kupitia Virtual Card

September 11, 2018 6:18 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom PLC Hisham Hendi (katikati), Rais wa Divisheni ya Kusini mwa Jangwa la Sahara wa Mastercard Raghav Prasad (kushoto) na Mkuu wa Fedha na Soko la Kimataifa wa benki ya Bank ABC Barton Mwasamengo wakitangaza uzinduzi wa huduma mpya ya M-Pesa Virtual Card jana jijini hapa. Picha|Vodacom.

  • Wazindua huduma itakayoweza wanunuzi wa bidhaa na huduma mtandaoni kufanya malipo kupitia M-Pesa mahali popote ulimwenguni.
  • Huduma hiyo mpya itazisaidia pia kampuni hizo kunasa zaidi wateja wanaofanya miamala katika biashara ya mtandaoni.

Dar es Salaam. Wanunuzi wa bidhaa mtandaoni huenda sasa wakapata machaguo zaidi ya ulipaji baada ya Shirika la huduma za kifedha la Mastercard na Vodacom Tanzania PLC kuanzisha mfumo wa malipo wa ‘virtual card’ unaoruhusu kulipia huduma au bidhaa popote ulimwenguni kwa kutumia simu ya mkononi.

Katika huduma hiyo mpya iliyozinduliwa jana (Septemba 10, 2018) jijini hapa, watumiaji wa Vodacom M-Pesa watakuwa na uwezo wa kulipia bidhaa au huduma zozote ulimwengu ambazo zinaruhusu malipo mtandaoni kwa kupitia mfumo wa ulipiaji wa Mastercard kama tovuti ya Amazon au eBay.

Ili kulipia, watumiaji hao wa M-Pesa watalazimika kutengeneza kadi hiyo na kupata taarifa za siri kuhusu Mastercard kupitia huduma hiyo ya kadi inayopatikana kwa sasa kupitia mfumo (menu) ya M-Pesa. Vodacom imeeleza kuwa itawezesha mfumo huo wa malipo katika programu ya M-Pesa (app) kwa wale wanaotumia simu janja (smartphone).


Inayohusiana: NMB yaingiza sokoni huduma tatu za kidijitali kwa mpigo


“Uzinduzi na ufanyaji kazi wa virtual card kupitia M-Pesa utaleta mapinduzi katika kuwezesha Watanzania kufanya manunuzi mtandaoni na kuondosha vikwazo ikiwamo kuwa na akaunti ya benki na pia kupunguza hatari ya mteja kuweka taarifa zake za kibenki mtandaoni,” amesema Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom, Hisham Hendi.

Hendi amesema kuwa kupitia M-pesa, yenye wateja milioni 8.2 na wakala zaidi ya 100,000, wanunuzi wa bidhaa na huduma mtandaoni wanaweza kufanya malipo hayo hadi kwenye tovuti za kimataifa kupitia mfumo huo mpya ulioundwa kwa kushirikiana na benki ya biashara ya BancABC.

Hatua hiyo ya ushirikiano na Mastercard itaisadia Vodacom kuongeza wigo wa watumiaji kwa kuwa hadi kufikia Juni 2018 ilikuwa na asilimia 41 ya wateja wote wanaotumia simu za mkononi kupata huduma za kifedha (mobile money subscription) kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Rais wa Mastercard wa Mastercard wa ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara Raghav Prasad amesema uendelezaji wa kusambaza teknolojia iliyovumbuliwa katika biashara za kimtandao unatoa fursa kubwa zilizomo katika huduma jumuishi za kifedha na kwamba watu wengi zaidi wataweza kufanya malipo bila kuwa na pesa mkononi.

“Malipo ya aina hii yanategemewa kuwa zaidi ya asilimia 60, hii inathibitisha kwamba kwa baadaye huduma jumuishi za kifedha bila shaka zitakuwa kwenye simu zetu za mikononi ambazo tunakuwa nazo kila mahali,” amesema Prasad.

Enable Notifications OK No thanks