‘Virusi’ vilivyotafuna sekta ya kilimo, ufugaji 2020
- Kirusi kikuu ni mabadiliko ya tabianchi kwa Tanzania Bara na kwa Zanzibar, wizi wa mazao.
- Upatikanaji wa ardhi, ukosefu wa masoko na pembejeo nao ulitikisa.
- Kilimo cha umagiliaji na matumizi ya teknolojia ya kisasa kuwa mkombozi kwa wakulima.
Dar es Salaam. Licha ya ukuaji wa sekta ya kilimo kwa mwaka 2020, sekta hiyo bado inakabiliwa na changamoto lukuki ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, ambazo zisipotafutiwa ufumbuzi wa kudumu zitaathiri maendeleo ya wakulima siku zijazo.
Ripoti ya Sampuli ya Sensa ya Kilimo kwa mwaka 2019/20 kuhusu mazao, sekta ya mifugo na ufugaji wa samaki iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) hivi karibuni imeeleza kuwa, kwa mwaka 2020, sekta ya kilimo imerekodi ukuaji wa asilimia 5 huku ikichangia asilimia 15.4 katika pato la Taifa (GDP).
Sambamba na kilimo, sekta ya mifugo imekuwa kwa asilimia 5 na kuchangia asilimia 7.1 ya pato lote la Taifa mwaka jana.
Mchango huo ungekuwa wa kiwango cha juu zaidi endapo changamoto mbalimbali zingefanyiwa kazi kwa wakati na hivyo kuwaongezea wakulima tija.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa sekta ya kilimo na ufugaji kwa mwaka 2019/20 ilitatizwa na changamoto 22.
Changamoto iliyosumbua zaidi wakulima ilikuwa ni mabadiliko ya tabianchi ambayo kwa mujibu wa ripoti hiyo ilichangia silimia 17.8 ya changamoto zote zilizojitokeza katika kilimo.
Mabadiliko ya tabia yaliyojitokeza kipindi hicho ni pamoja na kubadilika kwa mwenendo wa unyeshaji wa mvua ambapo baadhi ya maeneo yalipa mvua nyingi na kusababisha mafuriko kwenye mashamba.
Pia maeneo mengi yalikosa mvua na hivyo kuathiri uzalishaji wa mazao hasa yale yasiyostahimili ukame.
Wakati wakulima wakikabiliana na mabadiliko ya tabianchi, pia walikuwa na kibarua kigumu cha kumudu gharama za uwekezaji katika shughuli za kilimo na ufugaji.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kukosekana kwa uwekezaji wa kutosha katika shughuli za kilimo kulichangia asilimia 15.6 ya changamoto zote za kilimo katika kipindi hicho.
Uwekezaji unaotajwa hapa ni upatikanaji wa pembejeo za kilimo na mtaji wa kutosha kuendesha shughuli hizo.
Sehemu ya mashamba ya michikichi katika Mtaa wa Mgumile mkoani Kigoma likiwa limezingirwa na maji baada ya ziwa kufurika kutokana na mabadiliko ya tabianchi yaliyosababisha kina kuongezeka.. Picha| Nuzulack Dausen/ Nukta Africa.
Changomoto nyingine ili kutopatikana kwa ardhi kwa asilimia 13.5, bei duni za mazao ya kilimo (asilimia 7.2) pamoja na magonjwa na wadudu kwa asilimia 6.7.
Changamoto hizo tano pekee ni zinaunda asilimia 60.8 ya changamoto 22 ambazo ziliitikisa sekta ya kilimo 2019/20.
Migogoro ya umiliki wa ardhi, ukosefu rutuba ya udongo, wizi wa mazao na ukosefu wa mbegu bora, pia ulichangia katika kupunguza kasi ya uzalisashaji.
Ripoti hiyo iliyotolewa Agosti mwaka huu, imeeleza kuwa changamoto mabadiliko ya tabia nchi iliwapata zaidi wakulima wa Tanzania Bara kuliko wa Zanzibar.
Kwa Bara, mabadiliko ya tabia nchi yaliathiri kilimo na ufugaji kwa asilimia 18.1 huku kwa Zanzibar ikiwa ni asilimia 4.8.
Kilichosumbua zaidi Tanzania visiwani ni wizi wa mazao ambao ulitokea kwa asilimia 20.8 ikifuatiwa na upatikanaji wa ardhi (asilimia 12) ikifuatiwa na uharibifu wa wanyamapori na ndege (asilimia 11) na wadudu pamoja na magonjwa kwa asilimia 11.
Ili kuhakikisha kilimo kinakuwa endelevu na kuwanufaisha wakulima, suala la mabadiliko ya tabianchi linapaswa kupewa uzito unaostahili kwa kutafuta njia mbadala kukabiliana.
“Ufugaji na kilimo kinachozingatia hali ya hewa vinatakiwa kupewa uzito unaostahili.” imesomeka sehemu ya ripoti hiyo ya NBS.
Piia inashauriwa kuwekeza katika teknolojia ya kisasa, kilimo cha umwagiliaji na upatikanaji wa mbegu bora zinazostahimili mabadiliko ya tabianchi.
Latest
