Vifo, majeruhi wa ajali barabarani waendelea kupungua Tanzania

August 26, 2020 3:41 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Vifo vinavyotokana na ajali za barabarani vimepungua kwa zaidi ya mara nne katika kipindi cha miaka minne iliyopita. 
  • Wadau wa usalama barabarani wapendekeza maboresho ya sheria yatakayosaidia kupunguza zaidi vifo na majeruhi.
  • Serikali yasema itapeleka muswada bungeni kuboresha ili kuongeza usalama barabarani.

Dar es Salaam. Vifo na majeruhi wa ajali za barabarani wameendelea kupungua kwa miaka minne mfululizo tangu mwaka 2015/16 nchini Tanzania, huku wadau wa usalama wa barabara wakichagiza mabadiliko ya sheria yatakayosaidia kumaliza kabisa madhira hayo. 

Ajali za barabarani ambazo matokeo yake ni majeraha, ulemavu, umaskini na vifo kwa sehemu kubwa husababishwa na makosa ya kibinadamu kama ulevi, mwendokasi; uchakavu au ubovu wa vyombo vya usafiri na kimazingira.

Takwimu za matukio ya usalama barabarani kwa mwaka 2015/16 hadi 2019/20 (Julai 2019 hadi Machi 2020) zilizotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani mwaka huu zinaonyesha kuwa vifo na majeruhi wa ajali  hizo wamekuwa vikipungua kwa viwango tofauti kila mwaka tangu mwaka 2015/16

Mwaka 2015/16, wizara hiyo ilirekodi vifo 3,413 lakini vimeshuka hadi vifo 1,084 vilivyorekodiwa kati ya Julai, 2019 hadi Machi, 2020 ikiwa ni sawa na pungufu ya zaidi ya mara tatu ndani ya kipindi cha miaka minne iliyopita. 

Sambamba na kupungua kwa vifo, takwimu hizo zinazopatikana pia katika hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya mwaka wa fedha wa 2020/21, zinaonyesha kuwa watu waliojeruhiwa kutokana na ajali hizo nao wamezidi kupungua kila mwaka.

Mwaka 2015/16 watu 9,825 walijeruhiwa katika ajali za barabarani nchini Tanzania lakini takrian miaka minne baadaye idadi yao ilipungua hadi 2,129 Machi 2020. 

Kupungua kwa idadi ya majeruhi na vifo vinavyotokana na ajali huenda ni matokeo ya kupungua kwa matukio ya ajali za barabarani katika kipindi hicho ambapo katika kipindi cha Julai, 2019 hadi Machi, 2020 yamerekodiwa matukio ya ajali 1,920 kutoka matukio 9,698 mwaka 2015/16. 

Waziri wa Mambo ya Ndani George Simbachawene amesema kupungua kwa ajali za barabarani kumechangiwa na kampeni ya “Utatu” inayohusisha Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) na jamii inayolenga kudhibiti vitendo vya rushwa na kuongeza uadilifu wa askari wa usalama barabarani. 

“Vilevile, elimu kwa jamii imetolewa kwa njia mbalimbali juu ya matumizi sahihi ya barabara na madhara yatokanayo na kutotii Sheria za Usalama Barabarani,” amesema Simbachawene katika hotuba ya bajeti iliyowasilisha zaidi ya miezi miwili iliyopita.   

Nini suluhisho la kudumu la ajali za barabarani?

Wadau wa usalama barabarani kikiwemo Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) wameendelea kupaza sauti zao kuhimiza uboreshwaji wa Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 ili kupunguza kwa kiasi kikubwa vifo na ulemavu unaosababishwa na ajali za barabarani.

Msimamizi wa kampeni ya #SafiriSalama inayoendeshwa na umoja wa asasi za kiraia, Gladness Munuo amesema wanahamasisha marekebisho ya sheria hiyo ili kukidhi mahitaji ya sasa watumiaji wa barabara ambayo yasipowekewa sheria, kanuni madhubuti yanaweza kusababisha athari kwa watumiaji hao.

“Watumiaji barabara wameongezeka na vyombo vya moto pia vimeongezeka hilo linaleta changamoto ya utumiaji wa barabara,” amesema Munuo kutoka TAMWA. 

Ajali za barabarani siyo tu zinasababisha ulemavu na vifo, bali ni chanzo cha umaskini wa kipato. Picha|Gazeti la Rai.

Munuo anasema maboresho ya sheria hiyo yako katika maeneo matano muhimu ikiwemo kuhakikisha ufungaji wa mikanda kwa abiria wote wa magari ikilinganishwa na sasa ambapo dereva ndiye anayebanwa na sheria hiyo kuvaa mkanda. 

Wadau hao wa usalama barabarani wanapendekeza kuwa uvaaji wa kofia ngumu uwe wa lazima kwa watumiaji wote wa bodadoda; udhibiti wa mwendokasi; na kupunguza kipimo cha ulevi kwa madereva ili kuwadhibiti kabisa madereva wanaotumia vilevi wakiwa wanaendesha vyombo vya moto. 

Kwa mujibu wa Taasisi ya Mabalozi wa Usalama Barabarani Tanzania (RSA Tanzania), kiwango cha pombe katika mwili wa dereva kinachoruhusiwa ni miligramu 80 kwenye kila mililita 100 za damu, yaani 80mg/100mls.

Iwapo dereva atakuwa na kiwango cha ulevi zaidi ya kiwango hicho, atakuwa ametenda kosa na atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria huku kanuni za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) zikipiga marufuku kabisa kwa dereva wa magari ya mizigo na abiria kuwa na kilevi mwilini. 


Zinazohusiana:


Wazazi au walezi wenye magari binafsi walazimishwe na sheria kuwaweka watoto wao kwenye vizuizi (viti maalum vyenye mikanda) wakiwa kwenye gari ili kuwafanya wawe salama wakati wote wa safari. 

Licha ya umuhimu wa kuwa na viti maalum vya watoto kwenye magari, Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 haijaweka wazi kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa kumlinda mtoto dhidi ya hatari yoyote inayoweza kutokea kwenye gari. 

“Ajali nyingi Tanzania zaweza kuzuilika iwapo waendesha vyombo vya moto watafuata taratibu.  Mfano, kutokuwa na mwendo kasi, kutoendesha vyombo wakiwa wametumia kilevi,kukagua vyombo vya moto kabla havijakwenda barabarani, miundombinu iwe rafiki na vibao vya alama husika viwepo,” Munuo ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz).

Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya Ajali za Barabarani ya mwaka 2017 inaonyesha kuwa watu milioni 1.25 hufariki  dunia kwa ajali kila mwaka ambapo watu milioni 20 hadi milioni 50 hubaki na majeraha na ulemavu wa aina mbalimbali huku waathirika wakubwa wakiwa watembea kwa miguu na madereva. 

Akizungumzia mabadiliko ya sheria, Simbachawene amesema wapo kwenye mchakato wa kuifanyia mabadiliko sheria hiyo ya usalama barabarani ambapo kinachosubiriwa ni kuipeleka bungeni.

“Mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Usalama Barabarani yanasubiri ridhaa ya Serikali na baada ya hatua hiyo muswada husika utawasilishwa Bungeni,” amesema Simbachawene. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW