VTS: Vifaa vya kudhibiti ajali vinavyoogopwa na madereva waluwalu

August 13, 2018 5:12 pm · Zahara
Share
Tweet
Copy Link
  • VTS imekuwa lazima kwenye mabasi ya mikoani ili kudhibiti mwendokasi.
  • Elimu kuhusu matumizi ya VTS inabidi izidi kutolewa kwa madereva.
  • Madereva wataka maslahi yao yazidi kuboreshwa wakati matumizi ya teknolojia nayo yakiongezeka kudhibiti ajali.
  • Kifaa kimoja hufungwa kwa wastani wa gharama ya Sh450,000.

Dar es Salaam. Katika jitihada za kudhibiti ajali za barabarani zinazotokana na makosa ya kibinadamu au mazingira, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) imeanzisha mfumo wa kufunga vifaa vya kielekroniki vinavyosaidia kufuatilia mwenendo wa endeshaji wa magari maarufu kama Vehicle Tracking System (VTS) katika mabasi ya masafa marefu.

Mabasi yote ya mikoani sasa yanalazimika kufunga vifaa hivyo vya VTS ambavyo taarifa zake zote hutumwa kwa Sumatra kwa ajili ya kudhibiti mwendo wa madereva waluwalu katika safari zao.

“Tumeweka VTS katika mabasi ya mkoani ili kuweza kufuatilia vizuri wanaoendesha magari zaidi ya mwendo unaotakiwa,na ni mfumo mzuri kwa kuwa unasaidia katika kupunguza ajali zinazochangiwa na mwendokasi,” anasema Salumu Pazzy, Ofisa Mwandamizi wa Mawasiliano wa Sumatra.

Baada ya taarifa za mwendokasi kukifikia kituo cha udhibiti mwendo cha Sumatra (Control centre) hupelekwa moja kwa moja ofisa mfawidhi wa mamlaka hiyo katika mkoa husika kwa ajili ya kulikamata na kulitoza faini basi hilo lililozidisha mwendo.

Pazzy anasema ofisi yake imekamata mabasi mengi ambayo yamezidisha mwendo kupitia teknolojia hiyo japo hakuweza kuitaja kwa haraka idadi ya magari hayo yaliyokamatwa hadi sasa.

Waandishi wa Nukta wameshuhudia hivi karibuni madereva wakionywa na mlio wa ving’ora vinatolewa vifaa hivyo ili kuhakikisha madereva wanatembea katika mwendokasi wa kilomita 80 kwa saa.

Baada ya kuonywa na ving’ora hivyo, madereva wamekuwa wakipunguza mwendo kwa kuwa hugeuka kero kwa abiria ambao baadhi huwa hawajui kwanini mlio huo hutokea.

                                Mabasi ya kwenda mkoani yakiwa katika Stendi Kuu ya Mabasi ya Ubungo. Picha|Rockycity24

VTS inafanyaje kazi?

Mkuu wa Idara ya Tehama wa Kampuni ya Fleet Track, Joshua Mshanga anasema  VTS  inayofungwa katika gari hutumia kifaa maalum ‘chip’ kama cha simu ambacho kinakusanya taarifa kwa kutumia setilaiti. Kampuni ya Fleet Track hujiusisha na ufungaji wa VTS kwenye magari.

Teknolojia hiyo kwa mujibu wa Mshanga inasaidia kuhifadhi taarifa hizo hata katika sehemu ambazo hakuna mtandao.

                                                 Vifaa maalumu vya kielektroniki vya kupimia mwendokasi wa magari maarufu kama Vehicle Tracking System ( VTS). Vifaa hiyo hupiga king’ora ndani ya basi pale dereva anapozidisha mwendokasi ulioanishwa na kanuni za usalama barabarani. Picha|Fleet Track. 

Utaratibu uliopo nchini ni kwamba dereva hatakiwa kuendesha mwendokasi wa zaidi ya kilomita 80 kwa saa. 

Hata hivyo, Mshanga ameeleza kuwa kipimo cha juu kimewekwa kuwa kilomita 85 ili kuruhusu madereva pale wanapotaka kuyapita magari yaliyo mbele yao wka mujibu wa kanuni za usalama barabarani. Baada ya kupita mwendokasi wa kilomita 85 kwa sasa kifaa hicho huanza kupiga king’ora. 


Inahitaji kiasi gani kufunga VTS?

Mshanga anasema kuwa VTS hufungwa kwa Dola za Marekani 200 (Sh454,000) kwa magari binafsi na mtumiaji kulipia Sh20,000 kwa magari ndani ya nchi na Dola za Marekani 25 (Sh56750) kwa magari yanayotoka nje ya nchi kama gharama za uendeshaji kwa mwezi.

“Mabasi haya ya mkoani wanatakiwa kulipa Sh60,000 kwa mwezi kwa ajili ya kutumia kifaa hicho” anasema Mshanga.

Baadhi ya wamiliki wameeleza kuwa VTS inasaidia kupunguza ajali za barabarani, kumkumbusha dereva pale anapoendesha kwa mwendokasi na kinapunguza matumizi makubwa ya mafuta katika gari. Ukiachana na Sumatra, wamiliki wa magari nao wanaeleza kuwa hufuatilia taarifa za mwendokasi wa vyombo vyao kwa njia ya mtandao.



Madereva waluwalu huaribu VTS

Licha ya wamiliki wa mabasi kupokea vizuri vifaa hivyo,  baadhi ya madereva waluwalu hawavifurahii na wamebuni mbinu za kuviharibu ili kutofuatiliwa mwendo wanaoendesha magari hayo na kuzuia kupigwa faini.

“Madereva wengine hawana elimu ya kutosha kuhusu VTS huwa wanazifungua au wanamwagia tindikali ili kuviharibu lakini mifumo yetu huwa inatupa taarifa kama kwenye gari fulani wamefanya uharibifu wa kifaa tulichokuifunga,” anamalizia Joshua.

Baadhi ya madereva wa mabasi makubwa wameiambia Nukta ufungaji wa ving’amuzi hivyo ni hatua nzuri ya kuzuia ajali japo mazingira ya kazi nayo huchochea kuongezeka kwa ajali hizo.

“Sisi tumelipokea vizuri kwa kuwa Serikali imeamua kuona ndiyo suluhisho la ajali. Lakini tunaomba mazingira ya kazi ya madereva na maslahi yao yaboreshwe maana madereva wasipokuwa katika hali nzuri hata kifungwe nini bado ajali zinaweza endelea kutokea,” anasema Kombo Lusambo kutoka Umoja wa Madereva Tanzania (Uwamata).

Sumatra inaeleza kuwa wanaendelea kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika matumizi ya VTS kudhibiti mwendo.

“Ukiondoa na changamoto ndogondogo zilizopo VTS inasaidia kupunguza ajali na tunataka kufunga hadi kwenye magari makubwa ya mizigo,” anamalizia Pazzy.

Enable Notifications OK No thanks