Uzushi: Mashabiki wa Simba hawataanza kutumia kipimo kipya cha Corona
- Wizara ya Afya yasema haijatangaza kipimo kipya cha Corona.
- Yawataka mashabiki wa mpira wa miguu kupuuza uzushi huo unaosambaa mtandaoni.
Dar es Salaam. Kama ni mtumiaji wa mitandao ya kijamii hasa WhatsApp nchini Tanzania, huenda umekutana habari picha inayosema kipimo kipya cha Corona kitaanza kutumiwa na mashabiki wa timu ya Simba.
Fahamu kuwa habari hiyo haina ukweli wowote na ni uzushi unaolenga kuleta taharuki kuhusu janga la COVID-19 hasa kwa mashabiki wa mpira wa miguu nchini.
Habari hiyo ambayo iko kwenye mfumo wa habari mpasuko (breaking news) imeambatana na picha ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Doroth Gwajima na kuwekwa maneno yanayosema “Waziri Gwajima: Kipimo kipya cha Corona kuanza kwa mashabiki wa Simba”.

Habari hiyo inadaiwa kutolewa na blogu maarufu nchini ya Millard Ayo na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
Hata hivyo, habari hiyo haina ukweli wowote kwa sababu Dk Gwajima hajatoa tamko kama hilo katika siku za hivi karibuni.
Pia Wizara ya Afya kupitia ukurasa wake wa Twitter tayari imekanusha habari hiyo huku ikiwataka Watanzania kuipuuza kwa sababu siyo ya kweli.
Taarifa ya uzushi, ipuuzwe. pic.twitter.com/V6Czx9ETOl
— Wizara ya Afya Tanzania (@wizara_afyatz) February 2, 2021
Hata timu ya Nukta Fakti ilipotembelea tovuti na mitandao ya kijamii ya Millard Ayo kujiridhisha kama imeripoti habari hiyo, haijafanikiwa kupata habari ya namna hiyo kuhusu kipimo hicho.
Kuthibitisha kuwa taarifa hiyo ni ya uongo, haijataja aina ya kipimo ambacho mashabiki wa Simba wataanza kupimwa.
Lakini hivi karibuni, China imetangaza kuanza kutumia kipimo kipya cha haja kubwa (Anal swabs) kuwapima watu kama wana maambukizi ya COVID-19, kwa sababu kina ufanisi mzuri.
Kipimo hicho kimeibua mjadala mpana kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii huku baadhi yao wakisema kinaogopesha kwa sababu kinatumika katika maeneo nyeti ya mwanadamu.
Njia nyingine zinazotumika kubaini virusi vya Corona kwenye mwili wa binadamu ni pamoja na kipimo kinachopitishwa kwenye pua, kooni na damu.
Katika kipindi hiki cha mlipuko wa janga la Corona, wananchi wanashauriwa kupata taarifa sahihi kuhusu ugonjwa huo kupitia mamlaka za afya ikiwemo Wizara ya Afya ya Tanzania na Shirika la Afya Duniani (WHO).