Uzingatie nini unapojenga nyumba za kisasa aina ya “contemporary”?
- Inashauriwa kutokuwa mchoyo wa malighafi.
- Watumie mafundi wenye uzoefu wa kujenga nyumba za kisasa.
Dar es Salaam. Bila shaka umeziona nyumba ambazo kimuonekano, bati halionekani. Wataalamu wanaziita nyumba hizo “contemporary”.
Kinachozipa nyumba hizo umaarufu ni muudo wake, kwenda na wakati na unafuu wa gharama za ujenzi.
Kujenga nyumba hizo, inamaanisha umepunguza matumizi ya bati ambayo kama mjenzi hajajipanga, atabaki akitoa jasho pamoja na gharama ya mbao za kuezekea nyumba.
Kukupatia mwanga wa kinachozungumziwa, mtoa huduma kwa wateja kutoka kampuni ya kutengeneza mabati iliyopo Dar es Salaam, Alaf amesema, mtu akitaka mabati ya vigae, yanauzwa kwa mita. Na gharama yake ni Sh21,000 kwa mita moja.
“Kwa kawaida, bati za kawaida za geji 30 ni Sh459,000 ambapo zinakuwa bati 16 kwenye bando,” amesema mtoa huduma kwa wateja kutoka Alaf wakati wa mazungumzo ya simu na Nukta Habari (www.nukta.co.tz).
Kwa mtu atakayechagua kujenga nyumba za contemporary, inamaanisha atapunguza gharama za mabati.
Licha ya kuwa ni nyumba nzuri kimuonekano, nyumba hizi zinaweza kugeuka jipu endapo hazitojengwa kwa kuzingatia viwango ikiwemo kupata fundi anayeziwezea.
Niliwahi kumsikia mtu akilalamika kuwa nyumba hizo ni mbaya kwa kuwa ya kwake sasa inavuja licha ya kuwa haijafikisha hata mwaka mmoja.
“Bati limewekwa vibaya. Hapa ninatakiwa kubadilisha ceiling board (dali) na ndiyo kwanza mwaka haujaisha tangu nyumba ikamilike,” amesema mkazi wa jijini Dar es Salaam, Timoth Mapinda.
Jambo hilo linatuleta kwenye mada ya leo. Uzingatie nini unapoamua kujenga nyumba kama hizo? Madini yote hata hapa:
Nyumba hizi zinapunguza gaharama za mbao na mabati. Picha| CAAN Design.
Pata fundi mzoefu
Mara nyingi kukwepa gharama kwa kutafuta fundi wa “bei chee” husababisha wamiliki wa nyumba kuingia kubwa za matengenezo.
Vitu kama kutafuta fundi wa kufanya kazi yako kwa gharama nafuu ni sababu ya baadhi ya kazi zako kufanywa kwa kulipuliwa.
Kwa mujibu wa Mbunifu wa majengo, Jeremia Buzinza, ukipata ramani kutoka kwa mtaalamu, inamaanisha imechorwa kwa kuzingatia viwango vya ujenzi, hivyo unahitaji fundi mwenye ueledi kupata matokeo kama yaliyopo kwenye ramani.
Buzinza amesema ni vyema kumuuliza mbunifu wa jengo lako kama anafahamiana na fundi anayeweza kukupa matokeo mazuri ya ujenzi wa nyumba yako.
“Malighafi ya kutokubania ni nondo kwenye Renta ni muhimu sana kuzisuka na si kuzilaza,” amesema Buzinza.
Usibanie malighafi
Baadhi ya watu hubania vitu kama mabati, saruji na mbao ambazo fundi anahitaji kwa ajili ya kukamilisha ujenzi. Hiyo ni sababu ya baadhi ya mafundi kufanya kazi bora liende na aachane na wewe.
Ili kuepukana na changamoto zinazoweza kukukausha waleti yako kwa kufanya marekebisho kila siku, inashauriwa kumpatia fundi mahitaji anayohitaji.
“Wateja wenyewe wanapenda vitu vya gharama ndogo sana hii hupelekea kukwepa wataalam wakiogopa gharama, mwisho wa siku mambo yanakuwa mabaya,” amesema Buzinza.
Amesisitiza kutumia wataalam ili kuwa na uhakika wa matumizi ya malighafi ulizonunua.
Soma zaidi
- Unayoweza kufanya kudhibiti matumizi makubwa ya umeme nyumbani
- Toolboksi: Teknolojia inayowaunganisha vijana na fursa za ufundi stadi Tanzania
- Zingatia haya unaponunua taa za nyumbani
Ajiri kampuni ya ujenzi ifanye kazi
Kutokuwa na uhakika na mafundi wako nao ni mtihani. Unaweza kuhofia vifaa vya ujenzi kuibiwa ama kutokutumika vizuri. Ili uepukane na hayo yote, ni bora uajiri kampuni ya ujenzi.
Kwa mujibu wa Mhandisi Buzinza, kuajiri kampuni kuna faida nyingi ikiwemo uhakika wa kazi yako kufanyika kwa ubora.
Kwa kuwa kampuni huwa na historia katika fani ya ujenzi, utapata nafasi ya kuona baadhi ya kazi za nyuma kujiridhisha na utendaji kazi wa watu unaotarajia kuwaajiri.
“Endapo hata nyumba ikijengwa vibaya una uwezo wa kuishtaki kampuni ukalipwa fidia. Ni tofauti na kupata janja janja,” amesema Buzinza.
Changamoto ilipo
Mtaalamu huyo amesema kinachosumbua zaidi kwenye ujenzi wa nyumba hizo ni mfumo wa kutoa maji kwenye paa.
“Mfumo wa kutoa maji juu kidogo upo “complicated” kama mtaalamu hana huo utaalamu, ni lazima itavuja tu,” amesema Buzinza.
Latest