Zingatia haya unaponunua taa za nyumbani

June 10, 2020 1:46 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Hakikisha unatazama ubora na mada wa matumizi ya taa hizo ili kuepuka hasara.
  • Kila taa ina mahali pake pa matumizi.
  • Unaponunua taa zingatia jina na umaarufu wa kampuni unayonunua.

Dar es Salaam. Baada ya kupata mwangaza wa bure mchana kutwa, usiku ni muda wa kutafuta “switch” za taa ili uweze kuangaza sehemu ambayo kwa muda huo imegubikwa na giza.

Mwanga hutusaidia kwa mambo mengi hasa kutufanya tuwe salama dhidi ya hatari tunayoweza kuipata wakati wa giza. 

Hata hivyo, yapo mambo ya kuzingatia unaponunua taa zinazotumia umeme wa nyumbani au ofisini ili kuhakikisha zinakuwa na ufanisi mzuri wakati wa kutumia. Uzingatie nini unaponunua taa?

Kampuni iliyotengeneza taa

Mhandisi wa masuala ya nishati kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Baraka Kanyika ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) moja ya vitu muhimu ni umaarufu wa kampuni “brand” iliyotengeneza taa unayoichagua.

Endapo unaenda kununua taa na ukakuta kuna “brand” fulani ipo takriban kila duka unalopita, hilo sio jambo la kupuuza kwani umaarufu wake ni lazima una sababu.

“Kuna taa zingine ambazo wafanyabiashara wanaziingiza kwa kuwa zimekataliwa nchi fulani. Mtu akienda Kariakoo akakuta taa ya Tronic inauzwa bei kubwa na akikutana na hiyo inauzwa bei ndogo, atachukua hiyo licha ya kuwa haina ubora,” amesema Kanyika.

Muda itakaowaka taa hiyo

Jambo lingine ni muda ambao taa itawaka ambapo katika boksi la kila taa unaponunua linakuwa na muda ambao taa hiyo itawaka.

Kwa mujibu wa tovuti ya imore taa nyingi huwaka kuanzia saa 1,000 sawa na takriban siku 41 na zingine hadi saa 3,000 (Sawa na miezi minne).  

Tovuti hiyo imesema taa za Phillips huwaka hadi saa 25,000 sawa na miaka miwili na mienzi 8 na hivyo kufaa kwa mtu ambaye hapendelei kununua taa kila mara.

“Chagua brand anayokupa masaa mengi zaidi,” ameshauri Kanyika.

Kuna taa maalumu kwa ajili ya kila eneo. Kuna taa ya kuweka katika bustani, ya kuweka chumbani na hata koridoni. Picha| 1001 Gardens.

Sehemu utakapoiweka taa

Naye fundi umeme kutoka kampuni ya vifaa vya umeme ya Susuma Traders ya mkoani Morogoro Daniel Susuma amesema jambo lingine la kuzingatia ni sehemu unapoiweka hiyo taa unayoinunua.

Wakati watu wengi wanadhani taa yoyote inaweza kukaa popote, Susuma amewashauri waanze kufikiri tofauti.

“Kuna taa maalumu kwa ajili ya kila eneo. Kuna taa ya kuweka katika bustani, ya kuweka chumbani na hata koridoni,” amesema Susuma. 

Mdau huyo ameshauri kuwasiliana na wataalamu na hata kuuliza pale unapoenda kufanya manunuzi ya taa ili kupata ile inayoitaka. 

“Unataka taa ukaweke jikoni. Chumba hicho hata kiwe na ukubwa wa mita tatu kwa tatu, bado kitafaa taa yenye mwanga mdogo na siyo taa kama utakayoiweka getini kwako kwa ajili ya ulinzi,” amesema  Susuma.


Zinazohusiana


Zingatia unene wa mfuko wako

Mtaalam huyo amesema zipo taa ambazo ni za mapambo na kama unahitaji pambo hilo kwa ajili ya sebule yako, unatakiwa ujipange kwa sababu gharama za manunuzi ni kubwa na wakati mwingine taa hizo hutumia umeme mwingi.

Unapotaka taa iwe na urembo, lazima utanunua yenye urembo, endapo lengo lako ni mwanga tu, utanunua tu taa ya kawaida.

“Niliwahi kukutana na taa inauzwa Sh750,000 na zipo zenye bei zaidi,” amesema Susuma.

Pia kiasi cha mwanga ambao unauhitaji katika sehemu utakapoweka hiyo taa nacho ni muhimu kuzingatia kabla hujanunua taa. 

Mathalan, kwa maeneo ya getini na uzio, ni lazima uweke taa zenye mwanga mkubwa ili kuwapata mwanga wa kutosha utakaosaidia ulinzi wa nyumba.

“Kama unanunua taa kwa ajili ya ulinzi, huwezi ukanunua taa yenye mwanga hafifu. Lazima utanunua yenye mwanga mkali. Lakini kama unanunua taa ya korido kuona mende akipita na tukipita tusigongane, unaweka taa yenye mwanga mkubwa wa nini?” amehoji Susuma.

Jumanne ijayo, usikae mbali na ukurasa huu kwani tutazungumzia vitu vya kuzingatia unaponunua swichi kuu au almaarufu kama “Main Switch” kwa ajili ya nyumba yako.

Enable Notifications OK No thanks