Unayoweza kufanya kudhibiti matumizi makubwa ya umeme nyumbani

April 11, 2020 7:37 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Watu wengi hulalamika umeme majumbani kuisha haraka pasipo kujua sababu.
  • Kati ya sababu hizo ni pamoja na matumizi ya vifaa vya zamani na ukosefu wa uelewa juu ya vifaa bora vya umeme.
  • Wadau wameshauri kubadilisha mfumo wa nyaya walau kila baada ya miaka mitatu.

Dar es Salaam. Mara nyingi watu wamekuwa wakilalamika juu ya matumizi makubwa ya umeme kwenye nyumba kuliko vile wanavyotarajia, lakini hawafahamu sababu za matumizi hayo kuwa makubwa.

Wapo watu wanaacha taa zikiwaka mchana kutwa ama kusahau kuzima feni na televisheni na usahaulifu mwingine huku wakisahau ukweli wa kwamba sababu za matumizi makubwa ya umeme ni nyingi na zinasababishwa na makosa ya kila siku.

Nukta (www.nukta.co.tz) inakuletea baadhi ya makosa ambayo unaweza usiwe unayafahamu kama yanasababisha umeme wako kuisha mapema kuliko inavyotakiwa.

  1. Matumizi ya vifaa vya zamani

Watu wengi hununua vifaa vilivyotumika au maarufu kama mtumba bila kujua kuwa, kutolewa kwa toleo jipya kila mara ni ishara ya kuwa teknolojia hiyo imepitwa na wakati na kwamba teknolojia mpya imekuja na maboresho. 

Vifaa vingi vya umeme vya zamani, vimetengenezwa na teknolojia ambapo baadhi vinatumia umeme mwingi. Mbali na teknolojia, baadhi ya vifaa hivyo vinakuwa vimechoka baadhi ya sehemu zake na hivyo kusababisha matumizi makubwa ya umeme.

  1. Kutumia vifaa vya bei ndogo au bandia

Baraka Kanyika ambaye ni Mhandisi wa masuala ya nishati kutoka Shirika la Umeme (Tanesco) amesema watu wengi hununua vifaa vya bei ya chini ambavyo mara nyingi matumizi yake ya umeme ni makubwa.

“Niliwahi kutembelea duka moja nikaona “Microwave” (kipashio cha chakula) kinauzwa bei ndogo kweli nikajiuliza mbona hii microwave ni cheap (bei rahisi) hivi? kukiangalia, kinatumia umeme mwingi mno,” amesema Kanyika.

Kanyika amesema mbali na vitu hivyo kuuzwa kwa bei ndogo, hata hali yake ya kudumu siyo ya kutegemea kwani vingi vinaharibika mapema.

  1. Mfumo wa taa majumbani

Baadhi ya nyumba dari lipo mbali na sakafu kiasi cha kuhitaji taa nyingi zenye mwanga mkubwa ili kutosheleza. Umbali wa dali unaathiri mwanga kwani kadri taa inapokuwa mbali, mwanga wake unapungua

Mhandisi Kanyika ameelezea hali hiyo akisema “chukulia mfano chumba cha oparesheni, kama taa ipo mita kumi juu utahitaji taa kubwa na yenye uwezo wa kutoa mwanga mwingi na hivyo kutumia umeme mwingi.”

Endapo rangi ya ndani ya nyumba siyo ya kuwaka kama nyeupe ni lazima mtu atahitaji taa nyingi. Picha| Popart decorations.

Mbali na umbali wa dari, aina ya taa unazotumia pia ina mchango kwenye matumizi ya umeme, Julius Mbungo mwasisi wa programu tumishi ya Toolboksi amesema taa zenye mwanga wa njano zimetengenezwa na teknolojia inayozifanya zitumie umeme mwingi ikilinganishwa na taa zenye mwanga mweupe. 

“Kama umeweka taa za njano basi usishangae kutumia umeme mkubwa kwani teknolojia yake ipo hivyo,” amesema Mbungo.

Rangi ya nyumba yako pia inaweza kuchangia matumizi makubwa ya umeme. Kanyika amesma endapo rangi ya ndani ya nyumba siyo ya kuwaka kama nyeupe ni lazima mtu atahitaji taa nyingi na hivyo kurudi kwenye matumizi makubwa ya umeme.

  1. Mfumo wa waya wa aridhini (Earth) 

Watu wengi hutumia fundi kanjanja kuweka mfumo huu bila kujua kuwa mfumo huu ni kati ya mifumo muhimu inayohitaji umakini mkubwa. Kanyika amesema endapo mfumo huu hautawekwa vizuri ni lazma mfumo huu utasababisha umeme mwingi kupotea ardhini.


Zinazohusiana


Ufanyeje kuepuka matumizi makubwa ya umeme?

Weka mipango ya muda mrefu unapotaka kujenga au unapokarabati nyumba ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuokoa gharama kubwa za umeme.

Kanyika amesema inaanzia tangu nyumba inapoanza kujengwa yaani tangu ramani ya nyumba hadi ujenzi wa nyumba unapokamilika unahusiana na matumizi ya umeme.

“Kama ukijenga nyumba ambayo unajua kwamba utatumia kiyoyozi, vifaa vya ujenzi vitakavyoendana na viyoyozi vinatakiwa kutumika. Mfano madirisha yenye fremu za plastiki badala ya fremu za aluminiamu,” amesema Kanyika.

Aluminiamu inapata joto haraka muda wa mchana na hivyo kuingiza joto ndani na kufanya kiyoyozi kufanya kazi kwa muda mrefu kupoza chumba na hivyo kutumia umeme mwingi.

Tumia vifaa vya nyumbani vilivyo buniwa kubana matumizi. Picha| Click energy.

Badilisha mfumo wa nyaya walau kila baada ya miaka mitatu, kwa mujibu wa Mbungo, watu wengi wanasahau kuwa baada ya kipindi fulani, mfumo wa umeme wa nyumba yote unatakiwa kubadilishwa kwani nyaya pia huchoka na hivyo kuvujisha umeme.

“Nyaya zinachoka. Kuna muda unafika nyaya zinaanza kuwa na “leakage” (kuvuja) na umeme unapotea,” amesema Mbungo

Tumia vifaa vya nyumbani vilivyo buniwa kubana matumizi. Siyo vifaa vya umeme tu, vifaa vya maji na vifaa vya kupikia na mapambo pia vinauhusiano na umeme.

Kanyika amesema bomba la maji linalomwaga maji mengi lin uhusiano na maji yanayopandishwa kwenye tanki kwa umeme. Pia maji yanayotolewa kisimani na pampu ya umeme ambayo mara nyingi inatumia muda mrefu na umeme mwingi.

Angalia uwezo wa kutumia umeme kila unaponunua kifaa cha umeme. Endapo unanunua pasi ya umeme, usiangalie muundo, jina au uzito. Jaribu kuangalia uwezo wake wa kutumia umeme kwani pasi zinatofautiana. Hauna haja ya kununua pasi inayofaa matumizi ya hoteleini au kiwandani kwa matumizi ya nyumbani.

Enable Notifications OK No thanks