Utafiti: Zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania hawali mlo kamili

October 8, 2024 6:22 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni asilimia 31.4 pekee ya Watanzania hula mlo kamili.
  • Zaidi ya nusu ya wakazi wa Dar es Salaam watajwa kula mlo kamili.

Dar es Salaam. Wakati wataalamu wa afya wakisisitiza kula mlo kamili unaojumuisha makundi yote muhimu ya chakula kama wanga, protini, na mafuta, ili kuupa mwili virutubisho vinavyohitajika na kuuwezesha kufanya kazi kwa ufanisi ikiwemo kujikinga na magonjwa tafiti zinaonesha zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania hawali mlo kamili.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Hali ya Usalama wa Chakula iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ni asilimia 31.4 pekee ya Watanzania ndio wanakula mlo kamili.

Hii inamaanisha kwamba katika watu 10 ni watu watatu pekee ndio wanakula mlo kamili unaojumuisha asilimia 10-15 ya protini, asilimia 15-30 ya mafuta na asilimia 55-75 wanga kwa mujibu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO  pamoja na Shirika la Chakula Duniani (FAO)

Aidha, Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) inatafsiri mlo kamili ni chakula kitokanacho na mchanganyiko kutoka makundi sita ya chakula ambayo ni mbogamboga, matunda, mafuta, vyakula vyenye asili ya wanyama, vyakula jamii ya kunde, karanga na mbegu zenye mafuta pamoja na vyakula vya asili ya nafaka, mizizi yenye wanga na ndizi za kupikwa.

Ni muhimu kuzingatia kiwango cha chakula unachotaka kula wewe na familia yako. Picha Canva.

Watu wa vijijini hatarini.
Hata hivyo, Ripoti ya Hali ya Usalama wa Chakula kwa Tanzania Bara kulingana na Takwimu za Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi 2017/18 inaonesha idadi ya wati wanaokula mlo kamili vijijini ni pungufu mara mbili ya watu wanaokula mlo kamili mjini.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo asilimia 22.7 ya watu wa vijijini ndio wanaokula mlo kamili huku ile ya mijini ikiwa ni asilimia 44.6, ambapo Dar es Salaam inafanya vizuri zaidi kwa angalau zaidi ya nusu ya watu wake yaani asilimia 62.6 kula mlo kamili.

Hii ina maana kwamba ni watu wawili tu kati ya 10 ndio hula mlo kamili vijijini, tofauti na mjini ambako watu wanne ndio hula mlo kamili, licha ya kuwa maeneo ya vijijini ndio wazalishaji wakuu wa mazao ya chakula.

Aidha, utafiti huo umebainisha kuwa asilimia 16.6 ya watu maskini ndio wanaopata mlo kamili huku wasio maskini wanaokula mlo kamili ni asilimia 36.8 jambo linaloashiria elimu zaidi kuhusu faida na maandalizi ya mlo kamili kwa jamii kwa kuwa halihusiani na hali ya kiuchumi pekee.

Wastani unaonesha Watanzania wanakula zaidi vyakula vya wanga kwa asilimia 68.9 ikifuatiwa na mafuta kwa asilimia 15.7 na protini kwa asilimia 12.3.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks