Bunge la Kenya laidhinisha kumuondoa madarakani Naibu Rais Rigathi Gachagua

October 8, 2024 9:29 pm · Esau Ng'umbi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya wabunge 281 kupiga kura ya ndio.

Dar es Salaam. Bunge la Kenya limepiga kura ya kumuondoa madarakani Naibu Rais wa nchi hiyo Rigathi Gachagua kutokana na mashtaka 11 aliyotuhumiwa nayo ikiwemo kuihujumu serikali, kuhusika katika ufisadi, ukaidi, na  kuendesha siasa za migawanyiko ya kikabila 

Jumla ya wabunge 281 wamepiga kura ya ndio huku wabunge 44  wakipiga kura ya hapana na kura moja ya kutokuwa na uamuzi wowote.

Spika wa Bunge la Kenya Moses Wetangula aliyekuwa akitangaza matokeo hayo amesema hatua inayofuata ni kumtaarifu Spika wa Bunge la Seneti ndani ya siku mbili zijazo ambapo Gachagua atakuwa na nafasi ya kujitetea kabla ya Bunge la Seneti kuamua hatma ya makamu huyo wa Rais wa kwanza kupigiwa kura ya kuondolewa madarakani.

Hatua hiyo ni baada ya Mbunge wa Kibwezi Magharibi, Mwengi Mutuse kuwasilisha hoja ya kumuondoa Gachagua madarakani kutokana na sababu 11 alizoainisha Septemba 26, 2024 na kisha hoja hiyo  kuungwa mkono na wabunge 291, ikiwa ni zaidi ya idadi ya chini ya wabunge 117 inayotakikana kuruhusu mjadala huo.

Sababu nyingine zilizotajwa na Mutuse kumuondoa Gachagua ni pamoja na kujikusanyia utajiri unaokadiriwa kuwa shilingi bilioni 5.2 katika kipindi cha miaka miwili dhidi ya mshahara wake wa jumla ya dola 93,000 kila mwaka tuhuma ambazo makamu huyo wa Rais alizikanusha kwenye mkutano wake na wanahabari jana Oktoba 7, 2024 akisema sehemu kubwa ya pesa zake zinatokana na urithi wa mali za kaka yake.

Gachagua alifika mbele ya Bunge la kitaifa majira ya saa kumi na moja jioni ya leo Jumanne Oktoba 8 ili kujitetea dhidi ya mashtaka yake ambapo utetezi wake aliouwasilisha kwa saa mbili  haukufua dafu baada ya kujadiliwa na wabunge.

Uamuzi huo wa Bunge la Kenya unakuja wakati ambao kwa siku za hivi karibuni kumeripotiwa kutokuwepo kwa maelewano mazuri kati ya Gachagua na bosi wake Rais wa Kenya William Ruto.

Mpasuko kati ya Ruto na Gachagua umekuwa ukionekana waziwazi katika siku za hivi karibuni nchini Kenya, huku makamu huyo wa rais akisema ametengwa katika shughuli za kiserikali akidai yeye na wasaidizi wake wameondolewa katika shajara ya taarifa muhimu za Rais.

Hata hivyo, wakati wa ibada Kitaifa ya Maombi jijini Nairobi iliyofanyika Oktoba 6, 2024 Gachagua alimuomba msamaha Rais William Ruto kwa makosa ambayo huenda amefanya bila yeye kufahamu ambapo alifafanua baadae kuwa msamaha huo haumaanishi kuwa ana hatia juu ya mashtaka yanayomkabili.

Huo ni uamuzi wa kwanza na wa kihistoria kwa Bunge la Kenya kumuondoa kiongozi wa juu kabisa wa nchi baada ya Rais.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks