Ushuru wa mazao ya misitu wawaweka matatani viongozi Tanga, Njombe

September 26, 2019 1:30 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua nguzo za umeme zilizorundikana kwenye kiwanda cha Qwihaya General Enterprises Company LTD cha Mafinga zikisubiri wanunuzi. Kiwanda hicho cha nguzo kilitembelewa na Waziri Mkuu, Septemba 26, 2019. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda hicho, Leonard Mahenda,  wa tatu kushoto ni Meneja Uzalishaji wa kiwanda hicho, Fred Ngwega  na wa nne kusho ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Happy. Picha| Ofisi ya Waziri Mkuu.


  • Imesema inafuatilia sababu za mikoa ya Tanga na Njombe kutotekeleza sheria ya kutoza asilimia tano ya ushuru unaotokana na mazao ya misitu.
  • Viongozi watakaobainika kutotekeleza sheria hiyo kuchukuliwa hatua. 
  • Wafanyabiashara watakaobainika kukwepa ushuru kulipishwa upya.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemwagiza Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara afuatilie sababu za mikoa ya Tanga na Njombe kutotekeleza sheria ya kutoza asilimia tano ya ushuru unaotokana na mazao ya misitu.

Amesema makampuni yanayonunua nguzo lazima yahakikishe yanazingatia sheria ya nchi ikiwemo ulipaji wa kodi na kampuni zote zilizonunua nguzo bila ya kulipa kodi zifuatiliwe na zilipe kodi yote waliyoikwepa.

“Naibu Waziri Tamisemi hakikisha unakwenda mkoani Njombe na uaanze kuzungumza na Mkuu wa Mkoa, tunataka kujua kwa nini hawajaanza kutekeleza sheria ya kutoza asilimia tano ya ushuru unaotokana na mazao ya misitu hali iliyosababisha wanunuzi kumbilia huko na kuacha kununua mazao hayo katika mkoa wa Iringa,” amesema Majaliwa. 

Majaliwa alikuwa akizungumza leo (Septemba 26, 2019) wakati alipotembelea kiwanda cha kutengeneza nguzo za umeme cha Qwihaya kilichoko wilayani Mufindi akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi mkoani Iringa.

Amesema Serikali itawabana wafanyabiashara wote walionunua nguzo kwenye mikoa hiyo ambao hawajalipa asilimia tano ya ushuru unaotokana na mazao ya misitu ili waweze kulipa kiasi chote walichokikwepa..

“Tunataka tujue ni nani huyo anayewakataza wasilipe kodi na tuangalie ana mahusiano gani na viongozi wa mkoa huo. Ukaangalie makampuni hayo yana mahusiano gani na viongozi hao hadi wasilipe kodi na tutajua kama kampuni hizi ni zao au za ndugu zao,” amesisitiza Majaliwa. 


Zinazohusiana: 


Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Serikali inahitaji kodi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na haoni sababu ya mikoa hiyo kushindwa kutoza kodi iliyowekwa kwa mujibu wa sheria. 

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Happi alimweleza Waziri Mkuu kuwa wateja wa mazao ya misitu wameanza kupungua na kwenda mikoa ya Tanga na Njombe kwa kuwa katika mikoa hiyo haijaanza kutekeleza sheria ya kutoza asilimia tano ya ushuru unaotokana na mazao ya misitu, hivyo ameiomba Serikali iwasaidie.

Sheria ya Misitu ya mwaka 2002 na mwongozo wa uvunaji wa mazao ya misitu wa mwaka 2007 unamtaka mfanyabiashara wa mazao ya misitu kulipa tozo mbalimbali ikiwemo asilimia tano (5%) ya ushuru utakaoingia kwenye mfuko maalumu wa misitu. 

Enable Notifications OK No thanks